Mkurugenzi Mkuu wa TEA awauma sikio wahitimu darasa la saba nchini

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bahati Geuzye amewataka wahitimu wa darasa la saba nchini kutojihusisha na makundi yanayoweza kuwaingiza kwenye vitendo visivyofaa vya kihalifu na vitendo vinavyoenda kinyume na maadili hivyo kukwamisha ndoto zao.
Ametoa wito huo leo Oktoba 13,2022 katika mahafali ya 19 ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Chamwino ya jijini Dodoma.

Bi.Geuzye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amesisitiza kuwa, "Muepuke kujihusisha na makundi yanayoweza kuwaingiza kwenye vitendo visivyofaa vya kihalifu na vitendo vinavyoenda kinyume na maadili na tamaduni za kitanzania ambavyo vinaweza kuwaweka matatani.

"Kila mmoja wenu aone fahari ya kuwa raia mwema, mzalendo pamoja na kuwa tayari kulitumikia Taifa letu la Tanzania.

Niwakumbushe vijana wanaohitimu kwamba huu ni mwanzo tu wa safari ya kupata elimu na maarifa, kila mmoja wa wahitimu anapaswa kuwa na ndoto kubwa na kuweka dhamira ya dhati katika kupata elimu."

Bi.Geuzye amefafanua kuwa,Serikali imeweka mazingira mazuri zaidi kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi masomo ya kidato cha tano na sita.
"Hivyo, kila mmoja wa wahitimu ana fursa nzuri ya kupata elimu. Niwahimize kudhamiria kwa dhati katika suala zima la kupata elimu na maarifa. Kumbukeni usemi maarufu wa “Elimu ni Ufunguo wa Maisha” kila mmoja wa wahitimu afanye jitihada katika kupata elimu.

"Kwa kipindi hiki mnaposubiria matokeo niwaase kuzingatia mafundisho na malezi bora kutoka kwa walimu, wazazi na walezi. Muwe vijana mnaozingatia maadili na muwe msaada kwa wazazi na jamii inayowazunguka,"amewaeleza wahitimu hao.

Katika mahafali hayo, wahitimu kupitia risala yao wameomba TEA kuboresha miundombinu ya elimu kwa kukarabati pamoja na kutoa ufadhili wa ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, uzio wa shule pamoja na kuchimbiwa kisima cha maji.

"Tumesikia maombi hayo, na tunaahidi kuwa Mamlaka ya Elimu ikiwa ni taasisi ya umma yenye jukumu la kuongeza jitihada za Serikali katika kuwezesha upatikanaji wa elimu bora, tutashirikiana nanyi na kuona namna bora ya kufanikisha maombi yenu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha,"amesisitiza Bi.Geuzye.

Amewaeleza kuwa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Hii ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

TEA ilianzishwa mwaka 2001 kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao pia ulianzishwa mwaka 2001 ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa nchini.

Kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, TEA inafadhili ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ikiwemo vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, mabweni, mabwalo na majiko yake, maabara na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara na ngazi ya Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar.

Vifaa vinavyotolewa ni pamoja na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Mamlaka pia hutoa ufadhili wa miundombinu na vifaa kwa ajili ya shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

"Mfuko wa Elimu wa Taifa unaendeshwa kwa fedha zinazotengwa na Serikali kila mwaka kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wafadhili wengine yakiwemo mashirika ya umma na ya binafsi.

Napenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuhakikisha Mfuko unatengewa fedha kila mwaka.

Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kiasi cha Sh. Bilioni 8.6 zilitumika kufadhili miradi mbali mbali na katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Sh. Bilioni 8.9 zimetengwa kwa ajili ya kufadhili miradi mbali mbali ya kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu.

Aidha, nawashukuru wachangiaji na wadau wa elimu wengine wote ambao wameendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa elimu bora nchini kwa kutoa misaada ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini,"amefafanua Bi.Geuzye.

Amesema,miongoni mwa vigezo vinavyotumika kutoa ufadhili kupitia Mfuko wa Elimu nchini ni pamoja na shule kuwa na usajili unaotambulika, idadi kubwa ya wanafunzi ambapo ufadhili unatolewa kupunguza msongamano katika madarasa na kwenye matumizi ya matundu ya vyoo.

Kigezo kingine ni shule kuwa kwenye mazingira yasiyofikika kirahisi.

Miongoni mwa miradi ambayo TEA imetekeleza katika mkoa wa Dodoma katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari katika miaka ya hivi karibuni kupitia ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa amesema ni mingi.

Miongoni mwa miradi ni ukarabati wa shule nne kongwe za sekondari ikiwemo Shule ya Sekondari ya Dodoma, Kondoa wasichana, Msalato wasichana na Bihawana ambazo zilikuwa sehemu ya programu ya Serikali ya kukarabati shule kongwe za Sekondari, kiasi cha shilingi Bilioni 4.2 zilitumika katika ukarabati huo.

Pia kuna ukarabati wa miundombinu katika shule za msingi nne za jiji la Dodoma yaani Kisasa, Kizota, Medeli na Mlimwa ‘C’ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 1.9 zimetumika.

Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 mkoa wa Dodoma umepata ufadhili wa ujenzi wa shule ya mchepuo wa Kiingereza wenye thamani ya sh. milioni 750. Ujenzi wa mradi huu bado unaendelea kutekelezwa.

Wakati huo huo,katika risala ya wahitimu wameeleza kuwa kati ya wanafunzi 358 walioanza masomo yao mwaka 2016, kutokana na sababu mbalimbali waliofanikiwa kuhitimu mwaka 2022 ni 268 hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news