Mtanzania Kili Paul atikisa India

NA GODFREY NNKO

MTANZANIA Kili Paul ambaye amekuwa miongoni mwa vijana wachache nchini wanaotumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ameendelea kuitangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vilivyo huku akionesha kwa umahiri kipaji chake kwa kutengeneza maudhui yanayoendana na filamu na nyimbo za Kihindi.
Kili Paul ambaye ana miaka 26 amekuwa akishirikiana na dada yake Neema Paul ambaye ana miaka 23 kutengeneza maudhui hayo kwa njia ya simu huku wakiyarusha katika mtandao wao wa kijamii wa Instargram na kwingineko.

Wawili hao, kwa maana ya dada na kaka kutoka mkoani Pwani wamekuwa wakifanya hivyo huku wakivalia kulingana na utamaduni wao wa Kimasai, wanatekeleza majukumu hayo wakati huo huo wakiendelea kuchunga ng'ombe na kulima ili kujipatia riziki ya kila siku katika maisha.

Aidha, Kili Paul ambaye kwa sasa yupo nchini India ameendelea kuwa gumzo baada ya mapokezi yake kuwa na mvuto zaidi yakijumuisha rika mbalimbali za watu nchini humo.
Kijana huyo wa Kitanzania anatarajia kuonekana katika Kipindi cha Big Boss India (BBI) ambacho huwa kinavutia mamilioni ya watu kutokana na ukubwa wake na aina ya maudhui ambayo huwa yanarushwa.

BBI huu ni msimu wake wa 16 tangu kuanzishwa kwake huku Muigizaji wa filamu nchini India, Salman akiendelea kuwa msimamizi wa kipindi hicho.
Runinga ya Colors TV ya nchini India ambayo huwa inaonesha kipindi hicho, imeendelea kutoa vionjo mbalimbali kuhusu uwepo wa Kili Paul na ushiriki wake katika kipindi.

Awali, Kili Paul akiwa Mumbai nchini humo alikuwa mmoja wa watu maarufu walioalikwa katika hafla ya Meta Creator Day toka kampuni kubwa ya kimataifa la Meta ambayo mwanzo ilikuwa inajulikana kama Facebook.

Katika hafla hiyo Kili Paul alikutana na staa mwingine wa Bollywood, Ranveer Sigh ambapo mashabiki walirusha video zikionekana mitandoani Kili na Ranveer wakiwa wanacheza pamoja na kukumbatiana huku mashabiki wakionesha kufurahishwa na wawili hao.

Waziri Mkuu India

Jumapili ya Februari 27,2022 Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi aliwasifu vijana hao kwa maana ya Kili Paul na Neema Paul, kwa kuimba wimbo wa taifa wa India Siku ya Jamhuri na kutoa heshima ya kipekee kwa mwimbaji mkongwe Lata Mangeshkar aliyefariki.

Mangeshkar ambaye alifariki Februari 6, 2022 mjini Mumbai akiwa na umri wa miaka 92, alikuwa ni mwakilishi wa utamaduni ambaye alitengeneza jina lake kupitia Bollywood licha ya kuonekana katika filamu chache tu.

Nyota yake iling'aa na kumfanya awe maarufu katika sekta ya filamu inayokuwa kama mwimbaji anayeimba nyimbo za filamu, sauti yake ikisikika na kuigizwa na wacheza filamu nyota wa Bollywood, kazi aliyoifanya kwa zaidi ya nusu karne.

Aidha, kwa miongo Lata Mangeshkar ambaye alifananishwa na ndege wa usiku wa Bollywood alikuwa ni mwimbaji ambaye alipendwa na kutafutwa na wengi zaidi.

Pia waigizaji wengi walitaka aimbe nyimbo zao. Rekodi zake wakati huo huo, ziliuzwa zaidi na aliimba nyimbo zipatazo 30,000 akiimba kwa mitindo mbalimbali na katika jumla ya lugha ya 36.

Waziri Mkuu Mondi alisema hayo kuhusu ndugu hao wa Kitanzania wakati wa toleo la 86 la kipindi chake cha ‘Mann ki Baat’.

"Siku hizi, ndugu wawili wa Kitanzania, Kili Paul na dada yake Neema, wako kwenye habari nyingi kwenye Facebook, Twitter na Instagram, na nina hakika na wewe pia, lazima umesikia kuwahusu. Wana mapenzi, hamu ya muziki wa Kihindi na kwa sababu hii pia wanajulikana sana.

"Mbinu yao ya kuchezesha midomo (lip-syncing) inaonesha jinsi wanavyofanya kazi kwa bidii. Hivi majuzi, video yake akiimba wimbo wetu wa Taifa ‘Jana Gana Mana’ katika maadhimisho ya Siku ya Jamhuri ilisambaa.

"Siku chache zilizopita, pia alitoa pongezi za heshimwa kwa Lata dhidi kwa kuwasilisha wimbo wake. Ninawathamini sana hawa ndugu wawili Kili na Neema sana kwa ubunifu wao wa ajabu,”aliongeza Mheshimiwa Mondi.

Heshima Maalumu

Pia Februari 21, mwaka huu Kili Paul alitunukiwa heshima maalumu na Ubalozi wa Jamhuri ya India nchini Tanzania.
Katika chapisho kwenye ukurasa wa Twitter, Balozi wa India nchini Tanzania, Binaya Pradhan, alishiriki picha za ziara ya Kili Paul kwenye ofisi ya Ubalozi wa India.

"Leo tulikuwa na mgeni maalum katika Ubalozi wa India nchini Tanzania.Msanii maarufu wa Tanzania Kili Paul amevutia mamilioni ya watu nchini India kwa video zake za kuchezesha midomo kwa nyimbo maarufu za filamu za India,"Balozi Pradhan alitweet.

Maamuzi ni yako

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam, wameieleza DIRAMAKINI kuwa, ubunifu wa vijana ni nyenzo muhimu ya kuwakomboa kiuchumi. Wamesema, iwapo vijana wataaachana na mawazo ya utegemezi na kutaka kutumia wasivyotafuta wanaweza kwenda mbali kama walivyofanya Kili Paul na dada yake Neema Paul.

"Tumekuwa na vijana ambao hawapendi kuumzia ubongo wao na kuja na wazo la kuwavusha, wanatamani kupata kwa njia rahisi ili waweze kutimiza matamanio yao ya kustarehe na wakati mwingine kulala tu, ndugu zetu hao kina Kili Paul na Neema wameonesha uthubutu na hakika wamedhirisha kuwa, ubunifu unalipa,"amesema Mussa Yusuph mkazi wa Tabata Magengeni jijini Dar es Salaam katika mahojiano na DIRAMAKINI.

Naye, Elizabeth Amos mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam ameieleza DIRAMAKINI kuwa, vijana hao wawili wameonesha mfano wa kuigwa, hivyo umefika wakati wengine kufuata na kuiga yote yaliyo mema ili kuziendea ndoto zao.

"Hatuwezi kuwa na kizazi tegemezi tu, tunapaswa kuwa na kizazi ambacho kimejipa jukumu la ubunifu kwa ustawi bora wa jamii zao na Taifa kwa ujumla, tukiwa wabunifu na kuja na fursa zinazotukomboa kiuchumi, ni rahisi kusonga mbele kiuchumi, tena itakuwa vigumu kusikia watu wanalalamika mara ajira hakuna au maisha magumu.

"Ugumu wa hayo yote unatokana na namna ambavyo tumejiweka sisi, vijana tujitambue na tusonge mbele,"amesema Elizabeth huku akijitolea mfano kuwa, yeye baada ya kuhitimu chuo na kukosa fursa ya ajira alijiingiza katika ujasiriamali na sasa anaweza kujitengea na hata kutoa ajira japo kidogo kwa wengine.

Hata hivyo, wengi waliozungumza na DIRAMAKINI walisisitiza kuwa, pale ambapo vijana wanaibuka na bunifu zao ambazo zinaleta matokeo bora kwa ustawi wao, jamii na Taifa, Serikali kupitia taasisi zake inapaswa kuwaunga mkono na kuwapa hamasa mapema ili waweze kuziendea ndoto zao.

"Serikali inapaswa kuendeleza bunifu za vijana hao,kuna baadhi ya taasisi watumishi wake wamekuwa kikwazo, wakishirikishwa mawazo ya kibunifu ya vijana wamekuwa chanzo cha kuwakatisha tamaa, hii inachangia wengi kushindwa kusonga mbele, hivyo kwa umuhimu kila anayeonesha bidii aungwe mkono, ubunifu wake upewe heshima, kuendelezwa na kuungwa mkono kadri iwezekanavyo,"amesema Daniel Julius mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news