Rais Dkt.Mwinyi:Zanzibar na India zitatanua wigo mkubwa wa biashara

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakusudia kuangalia maeneo ya kuingiza vipato ambapo wafanyabiashara wa India watashirikiana na Zanzibar kuendeleza sekta hiyo kwa maslahi ya wananchi wa nchi mbili hizo.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi amesema hayo Oktoba 7, 2022 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na ujumbe wa ngazi za juu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya India, ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Idara ya Ushirikiano kati ya India na Bara la Afrika, Dammu Ravi.

Amesema, Serikali itaangalia kwa kina maeneo yanayoweza kuingiza vipato ambapo wafanyabiashara wa India watashirkiana na kufanya kazi pamoja na wenzao wa Zanzibar ili kuendeleza sekta hiyo na kuleta maslahi kwa wananchi wa nchi mbili hizo.

Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali imekuwa ikifanya kila juhudi kutekeleza dhana ya Uchumi wa Buluu, hivyo akaiomba nchi hiyo kuanzisha Kituo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuzingatia uwepo wa soko kubwa hapa nchini kwa vile Zanzibar ni nchi ya kutoa huduma, hatua aliyosema itazalisha ajira.

Amesema pia kuna umuhimu wa kufungua hospitali maalum hapa nchini kwa ajili ya watalii ambao wamekuwa wakizuru kila mwaka kwa kiwango kikubwa.

Aidha, amepongeza azma ya India ya kufungua Tawi la Hospitali ya Apollo hapa nchini katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam, hatua itakayosaidia kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora za matibabu.
Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kupongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, pamoja na misaada mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo nchi hiyo imekuwa ikiisadia Zanzibar, ikiwemo miradi ya huduma za maji safi na salama ambapo kwa kiasi kikubwa itapunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Idara ya Ushirikiano Kati ya India na Bara la Afrika, Dammu Ravi, amesema Serikali ya India inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda uliopo kati yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo za biashara.

Amesema, India ina wataalamu wa kutosha katika sekta ya Uchumi wa Buluu, hivyo akaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kubainisha maeneo ambapo Taifa hilo litaweza kuisaidia.
Aidha, Katibu huyo amesema nchi hiyo inalenga kupanua wigo wa ushirkiano kwa kuongeza fursa za masomo kupitia nyanja mbalimbali.

Amesema wakati akiwa nchini alipata fursa ya kutembelea miradi mitatu ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali kupitia ufadhili wa nchi hiyo na hivyo akaharakisha utekelezaji wake ili awamu nyingine ya miradi ya maji iweze kufanyika.

Katibu huyo amebainisha hatua zinazochukuliwa na India ili kufanikisha ujenzi wa hospitali kubwa katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam, ikiwa ni Tawi la Hospitali kubwa nchini humo ya Apollo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news