Rais Dkt.Mwinyi atoa wito nyumba za ibada

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kushindana katika kufanya mambo ya heri ikiwemo ujenzi wa misikiti.
Ustadhi Ali Hassan Abdalla akisoma risala ya Kamati ya Masjid Mubarak Kiboje Muembeshauri Wilaya ya Kati Unguja wakati wa ufunguzi wa Msikiti huo uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi na kujumuika na wananchi wa kijiji hicho katika Sala ya Ijumaa iliyofanyika msikiti hapo. (Picha na Ikulu).

Alhaj Dkt.Mwinyi amesema hayo Oktoba 7, 2022 huko Kiboje Mkoa Kusini Unguja wakati alipofungua Msikiti wa Ijumaa wa Al-Mubarak, hafla iliyokwenda sambamba na Ibada ya Sala ya Ijumaa msikitini hapo.

Amesema, hatua inayoendelea kuchukuliwa na waumini na kujenga misikiti mizuri na ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya nchi, ni jambo kubwa na la heri linalofaaa kuendelezwa na waumini kwa kuzingatia fadhila kubwa zinazopatikana kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Pia amesema, ujenzi wa misikiti una njia nyingi, hivyo akawataka waumini wasio na uwezo kushiriki kwa namna yoyote ile, ili nao waungane na wafadhili katika kupata fadhila hizo.

Aidha, amesema kuna umuhimu kwa Waislamu mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa misikiti hiyo kushiriki kikamilifu katika Ibada za sala, hususani za jamaa pamoja na kudumisha umoja miongoni mwao.

Alhaj Mwinyi amesisitiza haja ya misikiti kutumika katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kupitia makundi mbalimbali kama vile wajane, walemavu, yatima na wagonjwa.

“Misikiti ina kazi nyingi za kheri, mbali na kutumika kwa ajili ya kufanya ibada pia inapaswa kutumika katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii,”amesema.
Alhaj Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuitunza na kuifanyia matengenezo misikiti ili iweze kuendeleea kubaki katika haiba yake na kudumu kwa kipindi kirefu.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru mfadhili pamoja na waumini wote waliofanikisha kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo.

Naye Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisisitiza umuhimu wa waislamu kuendeleza umoja miongoni mwao na kuwataka kuutumia vizuri msikiti huo, huku akiomba baraka nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ziushukie msikiti nuo.

Aidha, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume alitumia fursa hiyo kuwapongeza wale wanaofanya juhudi kwa namna tofauti ya kujenga misikiti kwa kigezo cha kupata fadhila nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuashiria kuufungua Msikiti wa Masjid Mubarak Kiboje Muembeshauri Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Mapema, katika risala yao, kwa niaba ya waislamu wa msikiti huyo iliyosomwa na Ustadhi Ali Hassan Abdalla alisema, msikiti huo umejengwa chini ya Ufadhili wa Sheikh Ahmeid Nassor Al- Riami, ambapo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 200 hadi kukamilika kwake, ukiwa na uwezo wa kuswaliwa na waumini 400 kwa wakati mmoja.

Alisema pamoja na mambo mengine, mfadhili huyo analenga kujenga madrasa, maduka, ofisi pamoja na nyumba kwa ajili ya Mwalimu wa Madrasa katika eneo hilo la msikiti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news