RC Shigella aipa NHC eneo Geita kwa ajili ya uwekezaji

NA MWANDISHI WETU 

MKUU wa Mkoa wa Geita,Mheshimiwa Martin Shigella amesema atalipatia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo bure kwa ajili ya kujenga jengo kubwa la biashara ili kuweza kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa mkoa huo kwa wakati mmoja.
Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhe.Martin Shigella akifurahia jambo na Bi. Domina Rwemanyila, Afisa Habari wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ofisini kwake leo.

Amesema kuwa, kwa sasa katika mji wa Geita kuna uhitaji wa jengo kubwa la biashara ambalo litakuwa na huduma mbalimbali ambazo zitapatikana kwa wakati mmoja.

Pia amesema, jengo hilo litasaidia kupunguza adha kwa wananchi ya kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kwa ajili ya kupata huduma na kuongeza kuwa jengo hilo litakuwa kitega uchumi kizuri kwa NHC na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Shigella ameyasema hayo leo Oktoba 6, 2022 ofisini kwake wakati wa mahojianao na mwandishi wetu aliyetaka kujua lengo na madhumuni ya kuwa na Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini kila mwaka na tija wanazopata wananchi wa Geita na mikoa jirani kupitia maonesho hayo.

"Kwanza niwapongeze sana NHC kwa kazi kubwa mnayofanya ya kuendeleza makazi nchini na kujenga majengo makubwa ya biashara, hii inaoensha dhahiri kuwa mnaunga mkono jitihada za Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mnaongeza makazi kwa wananchi.

"Kwa kipekee tena,nimpongeze sana ndugu yangu Nehemiah Mchechu kwa kuteuliwa tena kuiongoza NHC, mimi binafsi nina imani naye katika utendaji kazi wake, kwani ninamfahamu vyema ni mtu makini sana, lakini nimuombe alete timu yake ije ichangamkie fursa ya uwekezaji katika mji wetu, kwani niko tayari kupitia halmashauri kuwapatia eneo bure ili mje muwekeze maana mji wa dhahabu huu unakuwa kwa kasi kubwa sana,”amesema Mheshimiwa Shigella

Ameongeza kuwa, Mkoa wa Geita unakuwa kwa kasi kubwa sana kutokana na kwamba unapokea wageni wengi wakubwa kwa wadogo wakiwemo wafanyabiashara wa madini ambao wakati mwingine inaonekana kwao ni kero kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Shigella amesema,kama NHC itaweka jengo kubwa hapa la biashara litasaidia kupunguza kadhia hii na hivyo kuweza kuwasaidia wananchi pia kupata huduma kwa urahisi katika eneo moja ambalo litakuwa na huduma za kibenki, maduka makubwa ya biashara na nyinginezo.

Katika hatua nyingine, Mhe.Shigella ameiomba NHC kuendelea na mpango wake wa kujenga nyumba za makazi katika mji wa Geita kufuatia uhitaji wa nyumba hizo kuwa mkubwa kwa sasa kutokana na watumishi wengi wa kwenye migodi ni wageni, hivyo uhitaji wa nyumba ni mkubwa.

“Mji wa Geita kuna wachimbaji wengi wa madini wakubwa kwa wadogo ambao wengi wao wanahitaji kupata nyumba za makazi, hivyo basi NHC mnaweza kuja kuzungumza na wachimbaji hawa mkaona ni kwa namna gani mnaweza mkawasaidia kwa kuwapatia makazi bora, kwani baadhi yao wanahangaika sana kupata nyumba za gharama nafuu nami najua NHC inatoza gharama ndogo sana katika bidhaa zake hivyo tuwasaidie hawa ili waweze kuepukana na kadhia ya nyumba,”amesema Mheshimiwa Shigella.

Amesisitiza kuwa, mradi wa SAMIA HOUSING SCHEME (SHS) ambao utaanza kutekelezwa katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam na baadaye kusambaa sehemu mbalimbali nchini, mradi huo unaweza pia kutekelezwa katika mji wa Geita kwa kujenga walau nyumba kadhaa ili Geita nao wanufaike na mradi huo ambao unaonekana una lengo la kuwasaidia watu wenye kipato cha chini na kati.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Geita amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa kushiriki katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini kwa mwaka wa pili mfululizo na kusema kwamba ushiriki wa NHC unatoa fursa kwa wananchi kulifahamu vyema shirika lao na kufahamu miradi ambayo inatekelezwa kwa sasa.

Shirika la Nyumba la Taifa kwa mara ya pili mfululizo linashiriki Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZA Bombambili mjini Geita yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo “Madini na Fursa za Uchumi, Ajira kwa Maendeleo Endelevu”.

Post a Comment

0 Comments