Sakata la Kalynda E-Commerce Limited, BRELA yafunguka yote

NA DIRAMAKINI

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa ufafanuzi kuhusu Kampuni ya Kalynda E-Commerce Limited ya jijini Dar es Salaam.

Ufafanuzi huo unakuja ikiwa ni siku chache zimepita kwa baadhi ya wananchi kuibua malalamiko mbalimbali na tuhuma kadhaa kuhusiana na kampuni hiyo ambayo wanadai imewachezesha michezo ya upatu kinyume na kanuni, taratibu na sheria za nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Oktoba 12, 2022 na Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imefafanua kuwa,kampuni hiyo ipo kihalali na leseni iliyotolewa ni ya kufanya biashara ya masoko na mauzo ya bidhaa kwa njia ya mtandao pekee.

"Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusu kampuni inayoitwa Kalynda E-Commerce Limited baada ya kuona na kupokea malalamiko kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kuhusu uhalali wa biashara inayofanywa na kampuni hii.

"Kampuni ya Kalynda E-Commerce Limited ilisajiliwa tarehe 14 Juni, 2022 na kupewa cheti cha usajili Namba. 156483877. Kwa mujibu wa katiba ya kampuni (Memorandum and Articles of Association) shughuli kuu za kampuni ni pamoja na;

i. Uuzaji wa jumla wa vifaa vya kielectroniki na mawasiliano,
ii. Ufanyaji wa biashara ya kitekinolojia ya kimataifa mtandaoni.
Vilevile, Kalynda E-Commerce Limited ilipata Leseni ya Biashara tarehe 21 Juni, 2022 yenye Namba 20000031405 ambayo itaisha muda wake wa matumizi tarehe 20 Juni, 2023.

"Leseni iliyotolewa ni ya kufanya biashara ya masoko na mauzo ya bidhaa kwa njia ya mtandao pekee (Online Marketing and Sales).

"Wakati wa uwasilishaji wa maombi ya usajili wa Kampuni na Leseni ya Biashara taarifa zilizowasilishwa zilionesha ofisi ya Kalynda E-Commerce Limited zipo Kiwanja Na. 9, Mtaa wa Kaunda, Kata ya Msasani Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

"Hata hivyo, kumekuwa na taarifa zisizo rasmi zinazoleta taharuki kwenye jamii kuwa Kalynda E-Commerce Limited imekuwa ikifanya biashara ya Upatu “Pyramid Business” ya kukusanya fedha kutoka kwa wananchi kwa ahadi ya kupata faida ndani ya muda fulani kinyume na bidhaa au huduma iliyoombewa na kupata leseni ya biashara.

"Leseni ya Biashara ya Kalynda E-Commerce Limited inamruhusu kufanya biashara ya masoko na mauzo ya bidhaa kwa njia ya mtandao pekee (Online Marketing and Sales).

"Ufanyaji wa biashara kinyume na leseni iliyotolewa ni kosa la jinai chini ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Leseni za Biashara, Sura Na. 208.

"Wakala inapenda kutoa angalizo kwa umma kuwa kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya kibiashara na kampuni yoyote ni vema kupata uthibitisho wa uhalali na uwepo wa kampuni hiyo pamoja na biashara husika kutoka BRELA na Mamlaka nyingine za Serikali.

"Taarifa zote za Makampuni na Leseni za Biashara Kundi “A” zinapatikana kupitia tovuti www.brela.go.tz au ofisi za BRELA.

"Hivi karibu kumekuwa na matukio ya baadhi ya watu wasio waaminifu kughushi vyeti vya Makampuni, Majina ya Biashara na Leseni za Biashara kwa lengo ovu la kuwatapeli wananchi.

"Baadhi ya vyeti vilivyogushiwa ni pamoja na Kopa Fasta Company Limited, Champion Investments na Afric. Taarifa zimeshatolewa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya hatua za kijinai.

"BRELA inapenda kuukumbusha Umma kutojihusisha na Taasisi zinazofanya baishara za upatu “Pyramid Business” kwani ni kinyume cha sheria za nchi,"imefafanua kwa kina taarifa hiyo ya BRELA.

PICHA KWA HISANI YA UKURASA WA KALYNDA FACEBOOK.Inapatikana hapa>>>

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

3 Comments

  1. Mbona hawakufunguka kabla ya watu kutpigwa ama nyie huwa mnajua kutoa leseni basi hamna ufatiliaji ili kujuwa hawa tuliowapa leseni wanafanya shughuli gani? Mnakuja na blah blah wakati watanzania washaumizwa. Mjitafakari sio mnaropoka kujitetea

    ReplyDelete
  2. Tatizo umakini katika wizara husika katika kufuatilia. Vinginevyo nao walikuwa na share zao ndio maana likapita juu kwa juu

    ReplyDelete
  3. Mmeshapewa posho sio

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news