TEA yatoa ushauri kwa taasisi za elimu, shule za msingi nchini

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi. Bahati Geuzye ameshauri taasisi za elimu ikiwa ni pamoja na shule za msingi kuwashirikisha wahitimu wake (alumni) katika kukusanya na kuchangia raslimali za kuboresha miundombinu ya elimu ya shule husika.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA ametoa ushauri huo katika shule ya msingi Chamwino ya jijini Dodoma, tarehe 13 Oktoba, 2022 alipokuwa mgeni ramsi katika mahafali ya 19 ya wahitimu wa elimu ya msingi.

Amesema, Shule ya Msingi Chamwino ambayo imeanzishwa miaka ya 1950 itakuwa na wahitimu wengi wanaohudumu katika fani mbali mbali, hivyo ni vyema shule ikawashirikisha katika jitihada za kukusanya raslimali za kuboresha miundombinu ya shule.

Akizungumza na wahitimu, Mkurugenzi Mkuu wa TEA amewakumbusha kila mmoja wao kudhamilia kwa dhati kupata elimu na maarifa zaidi.“Serikali imeweka mazingira mazuri zaidi kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi masomo ya kidato cha tano na sita, hivyo, kila mmoja wa wahitimu ana fursa nzuri ya kupata elimu,” amesema.

Pia amesisitiza wahitimu kuzingatia mafundisho na malezi bora kutoka kwa walimu, wazazi na walezi na kuepuke makundi yanayoweza kuwaingiza kwenye vitendo vya kihalifu na vitendo vinavyoenda kinyume na maadili na tamaduni za kitanzania.

Awali katika risala yao wahitimu wameomba TEA kuboresha miundombinu ya elimu kwa kukarabati pamoja na kutoa ufadhili wa ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, uzio wa shule pamoja na kuchimbiwa kisima cha maji ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TEA amesema watashirikiana na uongozi wa chuo katika kutafuta suluhu za changamoto hizo kwa kadri.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news