TEA yaweka kambi siku tano DUCE kupitia maadhimisho na maonesho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) inashiriki katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu wazima katika viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) kwa lengo la kuonesha mchango wa elimu isiyo katika mfumo rasmi kwa jamii.
Mnufaikwa wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF)kupitia Sekta ya Uchukuzi akitoa elimu kuhusu matengenezo ya pikipiki na bajaji aliyopata kupitia ruzuku ya mfuko huo.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 17, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano cha Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maadhimisho hayo yanafanyika sambamba na maonesho ambapo yameanza rasmi leo Oktoba 17 hadi Oktoba 21.
Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa, TEA inashiriki maadhimisho na maonesho hayo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ambao unalenga kutoa mafunzo ya Ujuzi na Stadi za Kazi katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni Ujenzi, Utalii na Huduma za Ukarimu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Kilimo na Kilimo Biashara, Uchukuzi pamoja na Nishati.

"Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ni sehemu ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta Tija katika Ajira (ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza ujuzi nchini (NSDS) chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na inafadhiliwa na Serikali pamoja na Benki ya Dunia (WB),"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Pia kwa mujibu wa taarifa hiyo, zaidi ya wananchi 36,870 wamenufaika na ruzuku ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi ili kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.

Awamu ya kwanza ya SDF ilianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo taasisi 15 zilifadhiliwa kwa jumla ya shilingi Bilioni 3.1 wakati katika awamu ya pili taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 zikitumika kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news