Waziri Prof.Mkenda:Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili itajengwa Kigoma

NA MATHIAS CANAL-WEST

SERIKALI kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ina mpango wa kuanzisha Kampasi ya MUHAS mkoani Kigoma.
Kampasi hiyo itajengwa katika Halmashauri ya Ujiji mkoani Kigoma katika eneo la ekari 47.3 ambalo linapakana na eneo litalojengwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi.

Aidha,kampasi hiyo inatarajiwa kuwa na miundombinu itakayotoa mazingira bora ya ufundishaji na kujifunzia, utafiti pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Prof.Adolf Mkenda ameyasema hayo leo Oktoba 17,2022 wilayani Kasulu wakati wa ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mkoani Kigoma.

Waziri Mkenda amesema kuwa, serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia imetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 45.5 kwa ajili ya MUHAS. 

Kati ya fedha hizo, amesema kiasi cha dola za Marekani milioni 15 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika kampasi ya Kigoma.
Kadhalika, Waziri Mkenda amemshukuru Rais Samia kwa kuzindua majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga ambayo ni moja kati ya miradi iliyotekelezwa na Wizara ikiwa ni Mkakati wa Serikali wa kuboresha Mazingira ya utoaji wa Elimu ya Ualimu nchini.

Prof.Mkenda amesema kuwa,ujenzi huo umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu nchini (Teachers Education Supports Project-TESP).
Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga ulianza tarehe 26/03/2019 na ulikamilika tarehe 22/04/2022. 

Ujenzi umetekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT Kanda ya Magharibi chini ya Usimamizi wa Mshauri Elekezi Bureau for Industrial Cooperation (BICO) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, kazi ya utengenezaji na uwekaji wa Samani katika majengo haya inaendelea.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa, mradi huo umegharimu jumla ya Shillingi za Kitanzania 14,142,554,960.53 ambapo Sh.12,591,407,901.26 ni kwa ajili ya ujenzi wa majengo na sh. 1,551,147,059.27 ni kwa ajili ya utengenezaji na uwekaji wa samani na utakuwa na uwezo wa wa kuchukua wanachuo 800.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news