Tanzania yatwaa tuzo katika Maonesho ya Utalii nchini Korea

NA MWANDISHI WETU

BANDA la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata tuzo ya kuwa Banda lenye Ubunifu wa Kipekee katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii nchini Korea Kusini yajulikanayo kama ‘Busan International Travel Fair (BITF)’ yaliyofanyika jijini Busan kuanzia Oktoba 13 hadi 16, 2022.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 17, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika maonesho hayo ya kimataifa, na ya pili kwa ukubwa nchini Korea Kusini, wadau wa utalii kutoka katika nchi zaidi ya 30 walishiriki kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Mwaka huu Tanzania ilikuwa nchi pekee kutoka barani Afrika kushiriki katika maonesho hayo na kuweza kujinyakulia tuzo hiyo.

Aidha, sambamba na Ubalozi wa Tanzania Seoul,kampuni tatu za utalii kutoka Tanzania Bara na Visiwani, zilishiriki katika maonesho hayo. Kampuni hizo ni pamoja na ZARA Tanzania Adventures, SAFANTA Tours & Travel, na CHOUM Tours & Safari.

Tuzo hii ni ya pili kwa mwaka huu 2022, ambapo awali mwezi Julai 2022 katika Maonesho ya Utalii ya Seoul (Seoul International Travel Fair – SITF 2022), Banda la Tanzania lilitunukiwa tuzo ya “Best Marketing Award”.

Katika Maonesho hayo Ubalozi wa Tanzania Seoul, Bodi ya Utalii na wadau wengine walishiriki kikamilifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news