BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 53

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... Mama alionekana kuwa mbogo, kwa mara ya kwanza kijana akawa muoga mbele ya mama yake. Mama alikuwa kafura mfano wa mbogo, alianza kwa kusema " Mwanangu kumbuka wewe ni uzao wangu..."

Endelea

Wewe ndiye mtoto wa kiume pekee uliyesalia katika familia yangu. Napenda nikupe siri iliyofichika moyoni mwangu, sijawahi kumsimulia mtu yeyote katika maisha yangu" alipofika hapo yule mama mshirika mwenzetu alianza kulia, kitendo hiki kilimuumiza kwa kiwango cha juu kijana wake.
Katika maisha yake hakutegemea kumuona mama yake akiwa katika hali hiyo, na yeye akaanza kutokwa na machozi. Baada ya hapo mama aliendelea, "Mwanangu wewe si mtoto pekee wa kiume niliofanikiwa kuwazaa maishani mwangu. Wapo watoto wengine watatu kabla yako niliowazaa. Wakati huo sikuwa nikiishi mji wa Majengo bali nilikuwa nikiishi mji wa Kazuramimba.

Baada ya hapo tuliamua kukimbia eneo hilo na kuja kuishi maeneo haya ya mji wa Majengo. Toka hapo hatukuwahi kupotelewa na mtoto, ndipo tulipokupata wewe na dada zako watano.

Hata hivyo baada ya kuchunguza kwa kina tuligundua kuwa watoto wetu watatu waliuliwa na ukoo wa huyo binti uliye na mahusiano" alipofika hapo alikohoa kidogo huku akimuangalia mwanae Kho ! Kho ! Khooo! Kisha akaendelee ".

Mwanzoni mimi na baba yako hatukuamini, lakini baada ya kuchunguza kwa kina kupitia waganga mbalimbali tulibaini kuwa bibi yake na binti huyu ndiye aliyehusika.

Hili halina shaka hata kidogo kwani waganga walituonesha hilo, mbaya zaidi waganga hao waliwahi kutuhakikishia kuwa uchawi huo ungerithishwa kwa huyu binti.

Siku zote mzazi mwema hupenda maendeleo ya mwanae, hivyo sipendi kukupoteza mwanangu kipenzi. Baada ya miaka kadhaa kupita familia ya huyu binti walihama mji wa Kazuramimba na kuja kuishi majengo.

Toka hapo hakujawahi kuwepo mahusiano mema baina ya familia yao na familia yetu. Nakuhakikishia kuwa binti huyo ni mchawi, nahofia maisha yako mwanangu" mama huyo alihitimisha kwa kilio cha uchungu mbele za mwanae.

Kijana huyo aliumia sana kusikia maneno hayo toka kwa mama yake. Kwa kiasi kidogo maneno hayo yalikuwa na ukweli ila sehemu kubwa yalikuwa yamejaa uongo. Ulikuwa ni uongo mkubwa uliotengenezwa na mama huyo, hakutaka kuusema ukweli kuwa yeye na binti huyo ni wachawi.

Kijana alikasirika na kuamua kuachana na binti huyo, kwa kiasi fulani mama alifanikiwa kumweka sawa. Kwa kuwa maneno hayo yalimuingia vya kutosha kijana huyo, aliamua kumtafuta binti huyo ili amueleze ukweli kabla hajaachana naye.

Jioni yake kijana alifanikiwa kuonana na yule binti, kulingana na hasira alizokuwa nazo kijana huyo alisema kila kitu bila kuogopa.

Yule binti aliamua kumuuliza mpenzi wake, " Kwani kama yeye ni mchawi ni jambo gani alilokuwa akilihofia? Kijana akamwambia katika maisha yake asingeweza kuishi na mchawi".

Yule binti akauliza tena, "Kwani katika maisha yake kijana huyo hajawahi kuishi na wachawi? Yule kijana akajibu " Hakuwahi kuishi na mchawi".

Basi yule binti akamwambia kijana huyo kuwa, "Mbona mama yake na kijana na yeye alikuwa ni mchawi? Kwa nini kijana hakuwa amekimbia nyumbani kwao?" Maneno hayo yalileta ugomvi baina ya kijana huyo na mpenzi wake.

Mabishano yao yakatamatika kwa kutaka kijana ahakikishiwe kuwa, mama yake pia alikuwa ni mchawi.

Binti huyo alikwenda nyumbani kwao na kuchukua dawa ya kuonea wachawi, aliileta na kumelekeza kijana huyo kanuni na taratibu za kuzingatia kabla na baada ya kujipaka.

Kijana aliichukua dawa hiyo na kuelekea kwao. Wakati huo moyoni alikuwa na sononeko kuu, moyo ilimzuia kufanya kitendo alichokuwa amekusudia juu ya mama yake mzazi.

Upande mwingine wa moyo wake ulimsisitiza kutaka kuhakikisha endapo kweli mama yake alikuwa ni mchawi.

Upande wa kuhakikisha ndiyo ulioshinda, baada ya juma moja alijiandaa kwa taratibu alizopewa na kabla na baada ya kujipaka dawa.

Siku moja muda wa jioni aliwasha moto pale nyumbani kwao, alipoulizwa mbona kawasha mapema moto nyumbani akadai alitaka kuota kulingana na msimu huo kuwa wa baridi.

Ilipofika muda wa saa kumi na mbili kamili jioni alichukua dawa na kuiweka kwenye moto kisha dawa chache akajipaka kwenye nyusi zake.

Ghafla hali ya hewa ya pale nyumbani ilibadilika, kukawa na vitu vya ajabu ajabu vilivyokuwa vikionekana nyumbani hapo.

Aliweza kuwaona misukule wakiendelea na shughuli zao nyumbani hapo. Kulikuwa na fisi wengi ajabu waliokuwa wamefungwa kamba mithili ya mbuzi.

Bundi wa kutosha walikuwa wamekaa juu ya paa la nyumba wakiendelea na shughuli zao. Mbweha na ndege wa ajabu ajabu walikuwa wametamalaki kwenye mji mzima.

Kupitia haya tayari kijana alikuwa amekwisha amini kazi ya mama yake. Ghafla alimuona mama yake akiwa amepanda kwenye fisi akitokea ndani, kijana alijifanya kama hakuwa amemuona mama yake.

Hata hivyo mama hakuwa peke yake, walikuwa wamefuatana na mwanae wa kike mmoja. Kwa upande wao walihisi labda kijana huyo amewaona, wakaamua kurudi ndani kisha wakarudi wakiwa wameshikilia mkuki mkononi.

Mambo hayo yalifanyika mbele ya kijana huyo huku akishuhudia kila kitu japo alijifanya haoni. Walipokaribia walisimamisha fisi wao kisha wakamfuata kijana huyo aliyekuwa akiota moto.

Walimsogelea zaidi kijana huyo na kutoa mkuki huo na kutishia kumchoma. Kijana hakuonesha kushituka kwani alijifanya kama haoni kinachoendelea, baada ya hapo waliondoka huku wakiwa wamelidhika kuwa hawakuwa wakionekana kwa kijana huyo.

Toka siku hiyo kijana hakuwa na furaha moyoni mwake, alipatwa na hasira kila alipokuwa akimuona mama yake machoni mwake.

Mama yake aliamua kumuuliza kwa nini hakuwa katika hali ya amani, kijana alijibu kwa kifupi kuwa jambo lililokuwa likimuumiza ni lile alilomuelezea juu ya mchumba wake.

Hatimaye naye baba yake alimuuliza kijana kwa nini alikuwa katika hali hiyo, kijana bila uoga alimsimulia baba yake kila kitu.

Baba alitaka kuhakiki maneno ya mwanae kama ni kweli. Maana mzee amekaa na mkewe zaidi ya miaka thelathini lakini hakuwahi kuliona hilo kwa mkewe.

Kijana alimkubalia kisha akampa maelekezo namna ya kufanya, kisha alipewa dawa akafanya kama alivyoelekezwa na kijana wake.

Siku hiyo mzee aliandaa moto saa nne asubuhi, ilipofika saa kumi alikuwa uwanjani anaota bila wasiwasi. Hamu yake kubwa alitaka kumshuhudia mkewe na mwanae wakienda kuripoti kambini.

Ndugu msomaji kila siku saa kumi na mbili kamili jua linapozama, wachawi ni lazima wakaripoti sehemu husika.

Ilipofika saa kumi na mbili kamili jioni, mzee huyo aliweka dawa kwenye moto kisha akatulia. Punde si punde alisikia sauti ya fisi ya kutisha, sauti hiyo ya fisi ilimtisha mzee huyo na kutaka kukimbia.

Akajikaza kisabuni akatulia kama maji mtunguni, mara akawaona mke wake na mwanae wakiwa juu ya fisi wakielekea kuripoti kambini.

Mzee yule baada ya kujifanya anaangalia kwa siri, yeye alikuwa anaangalia waziwazi. Namna alivyokuwa akiwashangaa ndivyo walivyokuwa wanapata wasiwasi. Wakasemezana juu ya hali hiyo, wakaamua kufuata mpini wa kumtisha ili kuona kama alikuwa anawaona.

Walipomkaribia mzee yule alisimama, akachukua ukuni wa moto uliokuwa ukiwaka. Wakajaribu kumtisha kwa kumpiga na ule mpini mzee akaukwepa kisha akawatandika kwa kijinga cha moto alichokuwa ameshika mkononi.

Hapo ndipo pakatokea patashika lilipelekea mzee kupigwa mpaka kufa. Yote haya yalitokea machoni mwa kijana huyo. Baada ya kuua alipakwa dawa fulani kisha akasimama na kuanza kutembea. Ingekuwa vigumu kwa mtu yeyote kugundua kuwa yule mzee hakuwa hai bali kuna maarifa yaliyofanyika.

Ilipofika saa mbili usiku mzee alianza kulalamika kichwa kumsumbua, kichwa kiliendelea kundi mpaka akawa anatokwa damu puani, machoni na masikioni. Mama wa mji akawa analia kuliko maelezo huku akisisitiza mumewe kupelekwa hospitali.

Jirani walifika na kumpeleka kituo cha afya, lakini kabla hawajafika mzee huyo aliaga dunia. Kwa upande wa kijana alikuwa akijua kabisa kilichotokea mwanzo mpaka mwisho

Ndugu msomaji unadhani kisa hiki kinahusiana vipi na yule mganga aliyemtibu fundi? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

Jiandae kusoma simulizi ya KANISA LA KICHAWI na KABURI LA RAIS WA HOVYO simulizi hizi zitakujia mara mbili kwa kila juma

BHATASHE MUHILA
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news