BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 58

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... Yule mganga hakuwa akituona tulianza kujiandaa kwa tukio kubwa lililokuwa likienda kumtokea. Ghafla ile pikipiki ili...

Endelea

Ilianza kuyumba, yule dereva akataka kuiweka sawa barabarani, lakini iliendelea kuyumba zaidi. Ilipofika eneo tulilokuwa tumechimbia yai na kinyesi, iliacha barabara na kufuata mti mkubwa uliokuwa pembeni.

Wakati huo pikipiki hiyo ilikuwa imeshakata breki, hivyo kulikuwa hakuna namna ya kuisimamisha. Yote hayo yalikuwa yakitokea mbele ya macho yetu, pikipiki hiyo ilikuwa na kasi ya ajabu. Iliuparamia ule mti na kuugonga vibaya, dereva wake akajibamiza na kuangukia pembeni huku yule mganga akiwa kaangukia tumbo.

Tulikimbilia kwenye eneo hilo la ajali na kumkuta mganga yuko hoi bini taabani. Kwa kuwa hakuwa akijielewa tuliamua kumpaka dawa fulani puani mwake, kisha tukamlisha dawa fulani na kuachana naye.

Siku zote wahenga walisema,ndege mjanja hunaswa na tundu bovu. Mganga huyo alikuwa kanasa, tena alikuwa kanasa kwenye tundu bovu kuliko matundu mabovu yote. Tulimfuata yule bodaboda aliyekuwa kavunjika mguu wa kushoto, tukauvunja na ule mguu wake wa kulia. Tuliushika mkono wake wa kulia tukauvunja pia, kisha tukamkamata shingo lake na kulinyonga kwa nguvu.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji si ajali zote zinazotokea huwa ni uzembe wa dereva. Ajali nyingi husababishwa na majini, mapepo na vizuka.

Ajali zingine husababishwa na wachawi kupitia mahitaji yao, wapo baadhi ya watu huunganishwa kwenye ajali kulingana na mlengwa kupanda kwenye usafiri husika.

Tulihakikisha tumekamilisha kila tambiko juu ya ajali hiyo, maana mganga huyo hakupaswa kuwa hai. Kwa kiasi kikubwa BUNDI WA GAMBOSHI alikuwa katoa mchango mkubwa kufanikisha kudhibitiwa kwa mganga huyo.

Punde si punde watu walijaa eneo la ajali, mbaya zaidi hakuna aliyekuwa akituona wakati huo japo sisi tulikuwa tukiwaona vyema.

Walipofika kwenye ajali hiyo, walianza kumsaidia kwanza yule mganga kwa kuwa alionekana kuwa hai kuliko yule dereva.

Walimchukua na kumpandisha kwenye gari lililokuwa likipita maeneo hayo. Wakati huo tulikuwa tumeshafungua nati za breki ya gari hiyo, tukiwa tumedhamiria kumtesa zaidi mganga huyo.

Dereva alikanyaga mafuta gari likakubali kuondoka kwa mwendo wa hatari, wakati huo tulikuwa tumepanda usafiri wetu tukilifuatilia gari hilo.

Gari lile lilichanganya moto kwa mwendo mkali, likavuka maeneo ya bohari za tumbaku za Matendo likaongeza zaidi mwendo.

Wakati wote huo dereva aliamini kuwa gari lake lilikuwa salama, aliendesha kwa kasi ili kumuwahisha majeruhi hospitali.

Alipofika maeneo ya Lodge ya D-Gube alikanyaga breki kuitafuta kona iliyoko maeneo hayo. Bahati mbaya breki hazikushika gari likaongeza mwendo, wakati huo tulikuwa tumempelekea picha za kutisha kwenye kioo cha mbele.

Picha hizo za kuogofya zilimfanya dereva kukosa utulivu, kitendo cha kukosa utulivu nyuma ya usukani kilipelekea dereva huyo kuhama barabarani. Gari lilikwenda kugonga kwenye nyumba iliyokuwa karibu na barabara.

Katika ajali hiyo hakuna aliyekufa zaidi ya mganga huyo kuvunjika mbavu za kifuani upande wa kulia. Wakati huo alikuwa akijitambua vyema, kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa mganga huyo.

Tuliendelea kumshikisha adabu kulingana na mambo ya hovyo aliyokuwa katufanyia kwa muda mrefu, kwa kipindi hicho kifupi tayari mganga alikuwa ameshaonja joto la jiwe. Mbavu zake za upande wa kulia zilikuwa nyakanyaka, maumivu aliyokuwa akiyasikia ilikuwa siri yake.

Wasamaria wema walifika eneo hilo la ajali na kutoa msaada, dereva wa gari alikuwa mzima kabisa ila yule mganga aliendelea kukipata cha mtema kuni.

Kwa pamoja wasamaria wema hao walimchukua mganga huyo na kumpandisha kwenye bodaboda. Akajitolea mtu mmoja aliyempakata mganga huyo ile akae vyema nyuma ya pikipiki, ile bodaboda iliondoka kwa kasi kuelekea kituo cha afya cha Bweru.

Tuliendelea kuwafuata kwa nyuma na majeruhi wao, tulivuka shule ya msingi Umoja, kwa Gloria, kwa Robart Mtusi tulipofika Bweru sokoni tulichepuka kulia tukaifuata barabara ya Madua Ngoma.

Tulipovuka mitaa miwili tulifika eneo la kituo cha afya cha Bweru, wauguzi walikuja haraka kumpokea majeruhi huyo huku tukishuhudia kwa macho yetu.

Hatukuwa na wasiwasi kwa kuwa hata hospital hapo hakuna aliyekuwa akituona, walimchukua mganga na kumuingiza ndani ya hospitali hiyo. Kwa kuwa ilikuwa ni dharura baadhi ya taratibu hazikufuatwa ili kuokoa kwanza uhai wa mganga.

Kila hatua iliyokuwa ikifanyika tuliendelea kuishuhudia pasi na shaka. Hatimaye aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji, damu zilikuwa zikimchuruzika mdomoni, masikioni pamoja na puani.

Madaktari bingwa wa upasuaji waliingia kwenye chumba cha upasuaji, wakati huo tayari tulikuwa tumeshatangulia chumbani humo.

Wauguzi walikuwa wameandaa dawa na vifaa vilivyokuwa vikihitajika katika upasuaji mkubwa huo. Tulikwenda kukagua dawa hizo tukaibaini iliyokuwa unatumika kwa ajili ya nusu kaputi. Dawa hiyo inafanana sana na mkojo wa binadamu inapokuwa ndani ya chupa.

Tuliimwaga dawa iyo na kubakiza kiasi kidogo sana kisha tukaongeza mkojo ndani ya chupa hiyo. Wakiwa kwenye harakati hizo za upasuaji, ghafla yule mganga alizinduka kutoka kwenye kuzimia.

Akawa anashuhudia kila jambo lililokuwa likifanyika chumbani humo, kabla hajapiga kelele ya kuwashitua wale madaktari tulichukua sauti yake.

Kila alipojaribu kuwasiliana na wale madaktari hawakuweza kumuelewa. Wakaamua kumchoma sindano ya usingizi, ili asinzie.

Kwa kuwa tulikuwa tumeshaichakachua dawa hiyo ya usingizi hakuweza kusinzia, akawa anawatazama kwa macho kodo.

Tukaamua kumwagia dawa ya kufumba macho, kwa kuwa lengo letu ilikuwa ni kumuua kwa mateso madaktari wangeamini kuwa amesinzia. Kwa hiyo wangefanya upasuaji huku, maumivu makali yakimpata mganga huyo.

Madaktari wakafanya upasuaji huku wakiziunganisha mbavu zilizokuwa zimevunjika, maumivu aliyokuwa akiyapata mganga huyo ilikuwa ni siri yake.

Hapa niseme kidogo, mtu yeyote anapokuwa anafanyiwa upasuaji ndani ya hospitali, chonde chonde ndugu zake wanapaswa kuwa makini. Maana huu ni wasaa tunaoutumia katika ulimwengu wa giza kufanya mambo yetu.

Tunaweza kuutumia muda huu kumchukua muhusika na kuwawekea mtu mwingine, pia tunaweza kuzima pumzi ya mgonjwa kwa kumfanyia jambo lolote baya.

Tuliendelea kumfanyia unyama mganga huyo ndani ya chumba cha upasuaji. Kwa kuwa tulikuwa tumemzidi ujanja aliamua kukaa kimya huku akipata maumivu, tukaendelea kumfanyia vioja mbalimbali pasi na shaka.

Baada ya kuridhika na unyama huo tuliamua kumuacha mganga huyo, madaktari wakamalizia ushonaji huku wakiwa wameweka historia ya upasuaji uliochukua muda mrefu.

Wakati wanamalizia kumshona tulimsogelea mganga huyo na kumnong'oneza sikioni. Tulimsimanga kwa maneno kedekede huku tukimkumbusha ujinga wake, mpaka hapo mganga alikuwa akijutia sana makosa aliyotufanyia.

Walipomaliza upasuaji walimuhamishia kwenye chumba cha uangalizi maalumu, tukaachana naye na kurudi kambini tukiwa tumedhamiria kurudi baadaye.

Tulipofika kambini wachawi wenzangu waliendelea na shughu zingine. Tayari muda huo ilikuwa ni saa kumi na mbili jioni. Nilipoachana na wachawi hao ili nielekee kwenye jumba langu langu la makao makuu ya mchawi mkuu kwa mbele yangu alishuka BUNDI WA GAMBOSHI alionekana kuwa na hasira kibao juu yangu, hii nililibaini kulingana na alivyokuwa akinitazama.

Ghafla alipaa hewani na kuninyakua kama kawaida yake kisha tukaondoka maeneo hayo ya kambi. Tulienda kutua kwenye kituo cha afya cha Bweru, baada ya kutua bundi huyo alijigeuza na kuwa binadamu.

Tuliingia ndani ya kituo hicho na kuelekea kwenye chumba maalumu cha uangalizi alichokuwa kawekwa mganga.

Mle chumbani hatukumkuta mtu mwingine tofauti na yule mganga, alipotuona akashituka mithili ya mtu aliyepiga chafya bila kutegemea.

Yule BUNDI WA GAMBOSHI akamsogelea zaidi akiwa tayari amerudi kwenye umbo lake. Alitema kitu fulani kitandani hapo kisha akanipa ishara ya kumnyanyua mganga huyo toka kitandani kwake.

Kile kitu kilichotemwa na BUNDI WA GAMBOSHI pale kitandani kilichukua umbo na sura ya mganga.

Tulimchukua mganga na kuondoka naye mpaka kambini kwetu, tulifika kambini hapo mida wa saa tatu usiku.

Mpaka hapo mganga alikuwa akijitambua vyema, japo alikuwa akisikilizia maumivu ya mbavu pamoja na mshono wa upasuaji, hatukujali.

Tulienda kutua katikati ya kiwanja cha kambini kwetu kisha yule BUNDI WA GAMBOSHI akaanza kumhoji maswali kadhaa, mganga hakujibu swali lolote hivyo tukaamua kumshughulikia.

BUNDI WA GAMBOSHI alidokoa jicho la kulia la mganga huyo na kulitoa nje. Yule mganga akawa analia kwa maumivu mengine ya jicho aliyokuwa akiyapata, yule bundi akawa anakula lile jicho la mganga alilolitoa usoni kwa mganga.

Damu zilikuwa zikitoka kwa kasi kupitia tundu la jicho lililokuwa limebakia kwa mganga. Kelele za mganga alizokuwa akizitoa hazikuzuia kuendelea kumwajibisha.

Kwa mara ya kwanza THE BOMBOM nikaingiwa na huruma, sikitegemea kumuona mganga huyo katika hali ya unyonge.

Maskini alitia huruma kuliko maelezo, hata hivyo alikuwa kachelewa hakuwa na nafasi ya kujitetea. Nilimsogelea mganga huyo na kulishika sikio lake la kushoto, kwa kasi ya ajabu nililinyofoa na kuanza kulitafuna angali libichi.

Wakati huo BUNDI WA GAMBOSHI alikuwa anamalizia kula lile jicho, ilitia huruma kumuona mganga huyo akipoteza viungo vyake mbele yetu.

Nilikwenda kumpiga teke kwenye jeraha alilokuwa kafanyiwa upasuaji, alipiga ukunga kwa maumivu aliyoyasikia maradufu. Wakati huo nilikuwa nikiendelea kutafuna lile sikio lake.

Ndugu msomaji tayari mambo yanaelekea ukingoni, mganga yupo mikononi mwa THE BOMBOM na BUNDI WA GAMBOSHI. Nini kinachofuata katika simulizi hii? Tafadhali ungana na mimi mwishoni mwa simulizi hii.

Ndugu msomaji mwisho wa Simulizi ya BUNDI WA GAMBOSHI ni mwanzo wa Simulizi ya KANISA LA KICHAWI na KABURI LA RAIS WA HOVYO.Tafadhali jiandae kusoma simulizi hizo.

ULAKOMEYE
THE BOMBOM

Post a Comment

0 Comments