CHINA WANAOMBOLEZA:China ilipofikia, Zemin alichangia

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Novemba 30, 2022 Rais wa zamani wa Jamhuri ya Watu wa China, Jiang Zemin ambaye aliongoza Taifa hilo kupitia mabadiliko kisiasa mwishoni mwa mwaka 1980 amefariki dunia.

Rais huyo mstaafu Zemin ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China kuanzia 1989 mpaka 2002 alichukua madaraka kutoka kwa Zhao Ziyang na kuliongoza taifa hilo lenye watu wengi zaidi duniani amefariki akiwa na umri wa miaka 96.

Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Kamati ya Kudumu ya Bunge la Kitaifa la Watu wa Jamhuri ya Watu wa China (PRC), Baraza la Jimbo la PRC, Kamati ya Kitaifa ya Watu wa China. Mkutano wa Ushauri wa Kisiasa, na Tume Kuu za Kijeshi za CPC na PRC zimethibitisha kifo hicho.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, kiongozi huyo mstaafu anaondoka duniani huku akiwa na mchango mkubwa kwa Taifa hilo ambalo limepiga hatua kubwa kiuchumi duniani, endelea;


1:Kafa Jiang Zemin, China wanaomboleza,
Ni rais wa zamani, nchi aliiongoza,
Amekufa kwa amani, kwa miaka kajiweza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

2:Mhandisi wa mitambo, urais aliweza,
Mambo hayakwenda kombo, jinsi aliituliza,
Na kote kupigwa kumbo, vema alikumaliza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

3:Tiananmen Square, maandamano fululiza,
Yale yalileta shere, hata watu kuumiza,
Kule kutengwa kwa bure, yeye alikumaliza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

4:Moja tisa nane saba, ndani alijiingiza,
Kamati Kuu si haba, chamani lijituliza,
Baadaye na mikopo, kuishika akaanza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

5:Meya kule Shanghai, ndiko kazi alianza,
Zhao Ziyang hafai, maandamano kukweza,
Nafasi ikamdai, Zemin wakamkweza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

6:Atachokumbukwa sana, ni kwa chama kueneza,
Kilivyojibana sana, makali akapunguza,
Jinsi yeye aliona, wigo akauongez,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

7:Kule kwa wahafidhina, Zemin lijituliza,
Na tena tulimuona, maendeleo aweza,
Alisaidika sana, upinzani kupunguza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

8:Kwao wakomunisti, mapya aliyaingiza,
Nguvu kazi weze keti, chamani na kuongoza,
Na wenye mitaji eti, chamani kuwaingiza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

9:Ni kwa siasa za nje, sana sana aliweza,
China kujiunga nje, WTO liweza,
Na uchumi nje nje, China ilijiongeza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

10:Hii Hong Kong pia, Zemin aliiweza,
Wakoloni iachia, na China kujisogeza,
Nchi moja yasalia, kivyake kijiongoza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

11:Elfu mbili na mbili, pembeni lijituliza,
Huko aliko mahali, kazi aliendeleza,
Neno lake la akili, uzito lilipenyeza,
China ilipofikia, Zemin alichangia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news