Doha Metro, Lusail Tram wasafirisha abiria milioni 2.4 kwa siku nne Kombe la Dunia

NA DIRAMAKINI

KATIKA siku nne za kwanza za mashindano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 yanayoendelea nchini Qatar, usafiri wa treni za mwendokasi unaosimamiwa na Doha Metro ikiwemo Lusail Tram zimesafirisha abiria 2,442,963 katika maeneo mbalimbali, hasa kuelekea viwanja vya michezo, maeneo ya burudani na maeneo mengine.

Doha Metro imerekodi ongezeko kubwa la watumiaji wake wakati wa siku nne za kwanza za mashindano, ambapo jumla ya abiria waliosafirishwa kupitia mifumo yao kutoka kituo kimoja kwenda vituo mbalimbali ilifikia abiria 2,351,244.

Katika takwimu zake za kila siku, Kampuni ya Reli ya Qatar (Qatar Rail) iliripoti kuwa jumla ya watumiaji wa Lusail Tram ilifikia takribani abiria 91719 wakati huo huo, ambapo idadi hiyo inatafsiri ufanisi na uwezo wa mitandao ya kisasa ya usafirishaji ambayo hapo awali ilibinafsishwa na serikali ili kupata ufanisi mkubwa na kuondoa changamoto za hapa na pale wakati wa usafirishaji mashabiki wa soka, raia na wakaazi.

Jumla ya watumiaji wa treni za mwendo kasi wakati wa ufunguzi wa mashindano Novemba 20, 2022 ilifikia takribani abiria 544,962, ambapo vituo vya West Bay, Souq Waqif na DECC vilishuhudia idadi kubwa ya waliojitokeza, wakati idadi ya watumiaji katika siku iliyofuata ilifikia takribani abiria 529,904 wengi wap walitumia vituo vya Msheireb, Souq Waqif na DECC, huku idadi ya watumiaji ikifikia abiria 650,881 Jumanne iliyopita.

Vituo vya Lusail, DECC na Souq Waqif viliongoza orodha ya vituo vilivyotumika zaidi, huku idadi hiyo ikifikia abiria 625,497 siku ya Jumatano.

Kwa upande wa Lusail Tram, idadi ya watumiaji wa treni katika siku ya kwanza ilifikia abiria 21906, abiria 21187 katika siku ya pili, abiria 23291 katika siku ya tatu na abiria 25335 jana. Ili kuhudumia idadi kubwa ya wageni na mashabiki, Qatar Rail ilinuia kuongeza saa za kazi kwa njia tatu za treni.

Aidha, kwa mujibu wa vyombo vya ndani vya habari nchini Qatar, tangu kuzinduliwa kwa mashindano hayo na hadi leo, Doha Metro na Lusail Tram zimekuwa zikichangia kurahisisha usafirishaji wa mashabiki kati ya viwanja mbalimbali na maeneo ya matukio, na hivyo kuwa vyombo bora vya usafiri ambavyo vinatoa huduma bora na kwa ufanisi wa hali ya juu.

Post a Comment

0 Comments