Idadi ya watoto katika vituo vya utayari yazidi kuongezeka

NA MWANDISHI WETU

IDADI ya watoto waliokosa fursa ya kusoma elimu ya awali katika Mkoa wa Rukwa, Simiyu na Pwani imezidi kuongezeka katika Vituo vya Utayari wa kumuondaa mtoto kwenda shule sababu kubwa ikitajwa kuwa ni muitikio mkubwa wa jamii kuhusiana na mpango huo.
Hadi kufikia Novemba 4, 2022 Mkoa wa Pwani una zaidi ya watoto 1200 ,Mkoa wa Simiyu una watoto zaidi ya 1600 huku Mkoa wa Rukwa ukiongoza kwa kuwa na zaidi ya watoto 2000 katika Vituo vya Utayari.

Hayo yamebainishwa na washiriki wa Mafunzo ya SRP kutoka katika Mikoa ya Pwani, Rukwa na Simiyu yaliyomalizika Novemba 4, 2022 jjini Dodoma.

Akizitaja sababu za ongezeko hilo Afisa Elimu Taaluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, John Mpamwa amesema ongezeko hili limesababishwa na muitikio mkubwa wa wazazi kwa kuchukua hatua na kuwapeleka watoto katika Vituo vya Utayari ili waweze kuandaliwa kwaajili ya kuanza darasa la kwanza hapo mwakani.
Kwa upande wake Mratibu wa Shule bora kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Winfrid Chilumba amesema ongezeko hilo ni moja ya mafanikio ya awali ya Mpango wa Utayari.

Ameeleza kuwa sio tu idadi ya watoto imeongezeka lakini pia watoto wenye umri zaidi ya miaka sita waliokosa fursa ya kusoma elimu ya awali wamejitokeza kwa wingi katika Vituo ukizingatia mpango huu ulilenga hasa watoto wenye miaka minne hadi sita.
Naye Mtaalam Kiongozi anayesimamia eneo la ujifunzaji na ufundishaji kutoka katika Mradi wa Shule Bora, Vicent Katabarwa amesema Mikoa hiyo mitatu imetumika kama Mikoa ya majaribio , lengo likiwa baada yakuona mafanikio katika mikoa hiyo mpango wa utayari utatekelezwa katika Mikoa Mingine ambayo Shule Bora inahudumia.
Amesema tathmini ya utekelezaji wake itafanyika katika ngazi tatu, moja Halmashauri husika itafanya ufatiliaji kuona jinsi watoto wanavyojifunza,pili viongozi wa Kitaifa watatembelea Vituo vya Utayari na kufanya tathmini, na tatu ni idadi ya wanafunzi watakaoanza darasa la kwanza mwaka 2023 ambao wamepitia katika Mpango wa Utayari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news