Ihefu FC yawapiga Yanga SC 'pira msuli'

NA DIRAMAKINI

DIMBA la Highland Estate lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya limetumika kuwapunguza kasi mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ni baada ya Ihefu FC ambao walikuwa wenyeji kuwakung'uta wageni wao Yanga SC kutoka jijini Dar es Salaam mabao 2-1.

Ushindi huo wa Novemba 29, 2022 si tu kwamba umewashangaza Watanzania wengi bali umewafanya mashabaki wa Yanga kupigwa na butwaa kwa kupoteza mechi katika mchezo wa 50.

Ihefu FC walionekana kupambana kufa na kupona, baada ya wageni wao kutangulia kwa bao lililofungwa na Yanick Bangala Litombo dakika ya tisa ya kipindi cha kwanza.

Wakati Yanga wakiendelea kujivunia bao la awali, kiungo Never Tigere aliifungia Ihefu FC bao la kusawazisha dakika ya 39,hivyo kumaliza dakika 45 za awali pande zote zikiwa zimetoka suluhu ya bao moja kwa moja.

Katika kipindi cha pili, licha ya mtanange kuanza kwa kasi, kila mmoja akitafuta namna ya kuchomoka na alama tatu, Lenny Kissu dakika ya 62 aliwapunguza kasi Yanga kwa kutumbukiza bao la pili nyavuni.

Wakati huo huo,KMC wamelazimishwa sare ya 0-0 na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni mtanage uliochezwa katika dimba la Uhuru lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambayo ina timu 16, timu tano ambazo zipo kileleni kwa sasa vinara Yanga SC ndiyo namba moja ambao wanaongoza kwa alama 32 baada ya michezo 13, wakifuatiwa na Azam FC wenye alama 32 baada ya michezo 14.
Simba SC inashika nafasi ya tatu kwa alama 31 baada ya michezo 14, nafasi ya nne inashikiliwa na Singida Big Stars FC kwa alama 24 baada ya michezo 13 huku nafasi ya tano ikishikiliwa na Geita Gold FC ambao ina alama 21 baada ya michezo 14.

Aidha, timu za mwisho kutoka chini wanaoongoza mkiani ni Dodoma Jiji FC ambao wana alama tisa baada ya michezo 13, Polisi Tanzania FC nafasi ya 15 kwa alama tisa baada ya michezo 14, Ruvu Shooting FC nafasi ya 14 kwa alama 11 baada ya michezo 14.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news