Kundi la kifo: Uhispania yawadhalilisha Costa Rica kwa mabao 7-0 ndani ya Al Thumama

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya Hispania imefanya vyema kwenye mechi yao ya awali katika Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 linaloendelea nchini Qatar.

Pablo Martín Páez Gavira (Gavi) wa Uhispania akishangilia baada ya kufunga bao la tano akiwa na Aymeric Laporte. (REUTERS/Dylan Martinez).

Ni baada ya leo Novemba 23, 2022 kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Al Thumama wakiwachabanga Costa Rica,mchezo uliotuma ujumbe kwa pande zinazoungwa mkono kushinda taji hilo.

Kundi E lilipewa jina la 'kundi la kifo' kabla ya fainali hizo, lakini Uhispania haitakuwa na hofu kuelekea pambano lao dhidi ya Ujerumani baada ya kupeleka maumivu Costa Rica, na kupata ushindi wao mkubwa zaidi kuwahi kutokea wa Kombe la Dunia katika mchakato huo.

Ushindi wa La Roja unawaweka kileleni mwa Kundi E mbele ya Japan ambao waliwashangaza mabingwa mara nne Ujerumani mapema kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa.

Dani Olmo alifunga bao la 100 la Uhispania ndani ya dakika 11 kwenye Kombe la Dunia kwa bao la kwanza, huku magoli mawili ya Ferran Torres dakika ya 31 kwa penalti na lile la dakika 54 yakifuatiwa na mabao ya Marco Asensio aliyepata bao dakika ya 21, Pablo Martín Páez Gavira (Gavi) dakika ya 74, Carlos Soler dakika ya 90 na Alvaro Morata dakika ya 92 yakiwahakikishia vijana wa Luis Enrique kuwa, safari yao ni nyepesi wakikaza buti.

Uhispania imekuwa timu ya sita baada ya Brazil, Ujerumani, Italia, Ufaransa na Argentina kufikisha mabao 100 kwenye Kombe la Dunia.

Uhispania itacheza tena na Ujerumani kwenye Uwanja wa Al Bayt siku ya Jumapili, huku Costa Rica ikiwa na matumaini ya kuzinduka dhidi ya Japan kwenye Uwanja wa Ahmad Bin Ali siku hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news