LIPA KODI KWA WAKATI:Upende kuheshimiwa, na kupata tuzo nzuri

NA LWAGA MWAMBANDE

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) katika siku za karibuni imeendelea kuwaheshimisha walipakodi nchini kwa kurudisha shukrani kwao na kuitambua michango yao katika ukusanyaji mapato.

Shukurani ambazo zilienda sambamba na Maadhimisho ya Wiki ya Mlipa Kodi ambayo yalijumuisha ushiriki wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi na kutoa misaada kwa wagonjwa na wenye mahitaji maalum nchini.

Tuliona namna ambavyo, walipa kodi wengi walivyopewa heshima kubwa, ambapo TRA iliwachagua kulingana na vigezo ilivyojiwekea.

Miongoni mwa vigezo vya TRA ni pamoja kulipa kwa wakati, ushirikiano, kutokuwa msumbufu na mengineyo. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, hilo ni jambo la heri na kila mwenye nia njema na Taifa lake lazima aunge mono juhudi hizo,kwani kwa kufanya hivyo inasaidia kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya barabara, umeme, maji, afya, elimu na mingineyo, endelea;


1:Tamani kutambuliwa, mlipa kodi mzuri,
Upende kuheshimiwa, na kupata tuzo nzuri,
Kwa nje utasifiwa, biashara yako shwari,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

2:Utunzaji wa hesabu, kwamba zikae vizuri,
Lipa bila ya sababu, mapema ndiyo vizuri,
Taandikwa kwa kitabu, mlipa kodi mzuri,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

3:Muda wa kulipa kodi, shirikiana vizuri,
Usumbufu wajinadi, kutambuliwa sifuri,
Kwani huo ukaidi, mwisho wake ni kiburi,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

4:Ukiulizwa maswali, ya kodi jibu vizuri,
Fikira zisyende mbali, kama hauna habari,
Kwa vitendo na kauli, usiwe mtu wa shari,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

5:Kama unalipa kodi, mlipakodi mzuri,
Unaongeza idadi, walipakodi wazuri,
Na taifa lafaidia, kukusanya kodi nzuri,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

6:Kodi ikilipwa vema, bila subirisubiri,
Miradi yajengwa vyema, huduma zawa ni nzuri,
Twendeko twawa salama, kuziepuka hatari,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

7:Tunajenga barabara, kuboresha usafiri,
Na kuwa na reli bora, twende kasi usafiri,
Lipa kodi barabara, itekelezwe vizuri,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

8:Umeme twauhitaji, wa lazima siyo siri,
Hata ya kwetu mitaji, tuzalishie vizuri,
Kodi tunaihitaji, umeme uwe mzuri,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

9:Maji vituo vya afya, hata shule ziwe nzuri,
Kama tunapiga chafya, tiba yetu iwe nzuri,
Magonjwa ya kuogofya, yabanwe kupisha shari,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

10:Mamlaka ya Mapato, mnavyofanya vizuri,
Wanaoleta mapato, kuwatambua vizuri,
Asante kwa wenu wito, tutoe kodi vizuri,
Lipa kodi kwa wakati, ujenge taifa lako.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news