Rais Samia ametupa nguvu mpya-Wadau wa habari

NA DIRAMAKINI

WADAU wa habari mkoani Lindi wameonesha kuguswa na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ilivyokubali kutoa nafasi ya kupokea mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 ili iweze kukidhi matarajio ya wanataaluma kuliko ilivyo sasa ambapo mahitaji yao mengi yaliwekwa kando.

"Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali, imeonesha nia njema sana. Kwa sababu unaweza wewe ukawa unaongoza watu, lakini watu hawa wana mahitaji yao, ni vizuri ukasikia kauli zao wenyewe wanasemaje, na unazipima. Kwanza upokee halafu uzipime, kwa sababu wao ndiyo wanafahamu kila kitu huku chini.

"Kwa mfano waandishi wa habari wao ndiyo wanafahamu madhila na changamoto ambazo wanakutana nazo,lakini hata suala la uwezo, wanahabari wanafahamiana wenyewe. Hivyo, wanaweza kusema na kupendekeza kile ambacho wanaamini kikifanyiwa kazi kinaweza kuleta matokeo bora kwa ustawi bora wa taaluma ya habari nchini;

Hayo yamesemwa leo Novemba 26, 2022 na Katibu wa Lindi Press Club, Bw.Ahmad Mmow wakati akizungumza na DIRAMAKINI kuelezea namna ambavyo wanaguswa na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya vyombo vya habari nchini.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira njema na wanatarajia baada ya maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 pia maboresho mengine yatafuatia katika Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018).

"Amekuja Mheshimiwa Rais Samia amepokea yale maoni, na inawezekana yapo mengi tu ambayo mwanzoni hayakusikilizwa, sheria ikapitishwa kibabe na unakumbuka ilileta shida sana, lakini nguvu zikatumika, lakini leo hii Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeonesha usikivu wa hali ya juu.

"Hii ndiyo dhana nzima ya Serikali sikivu, Serikali inakuwa mstari wa mbele kuyasikiliza maoni ya wadau wakiwemo wanahabari kabla ya kufanya maamuzi au kutunga sheria.

"Tunatarajia maboresho ambayo yatafanyika hivi karibuni, yataleta tija na kuondoa kabisa ukakasi ambao ulionekana hapo awali, hivyo kuongeza taharuki na usumbufu katika taaluma ya habari nchini,"amesema Mmow.

Akizungumza katika kikao cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI), kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 21,2022,Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye alisema kuwa, Serikali imepokea mapendekezo ya wadau na sasa wanayafanyia kazi.

“Serikali inaendelea na mchakato wa mabadiliko ya sheria na sasa tunayafanyia mapitio ya mwisho ya mapendelezo ya marekebisho ya sheria,”alisema Mheshimiwa Nape.

Pia Mheshimiwa Waziri Nape alisema kuwa, hatua inayofuata baada ya kikao hicho, ni uandishi wa mapendekezo hayo na kisha kupelekwa kwa watunga sheria.

”Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili.Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016,” alisema Mheshimiwa Nape.

Wakati huo huo, Katibu wa Lindi Press Club, Bw.Ahmad Mmow amesema, tasnia ya habari nchi licha ya kupitia katika changamoto kadhaa imeendelea kuimarika, na wengi licha ya kutokuwa na taaluma ya habari wamekuwa wakipitia mikononi mwa vyombo hivyo na kuandaliwa kuwa viongozi na wenye ujuzi mkubwa.

"Tuchukulie mfano mdogo wa ndugu yetu Hassan Ngoma ambaye leo hii ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, alikuwa pale Clouds, yeye akusomea uandishi wa habari, lakini alichukuliwa pale Clouds kwa maandalio maalum, na Serikali ilimpenda kwa sababu alikuwa na uwezo, watu wengi ndivyo walivyo katika taaluma hii, wengi wana uwezo mzuri sana na hawakusomea uandishi wa habari, lakini wanafanya vizuri sana na wana vipaji vikubwa.

"Unaweza ukawa unapiga kelele kwa sababu ya vyeti, lakini hilo suala lazima liangaliwe kwa sababu kuna watu ambao wametoka vyuo, lakini uwezo wao ni mdogo, lakini unakuta mtu kafanya kazi ya uandishi wa habari kwa miaka mingi, ana uwezo mkubwa, weledi na ufanisi ambao unaleta matokeo mazuri katika taaluma, hivyo heshima ya taaluma hii ni kubwa, changamoto inakuja tu pale ambapo wakati mwingine wadau hawapewi nafasi ya kutoa moni yao vya kutosha kama huko nyuma,"amesema.

Naye mwanahabari Fatuma Maumba amesema, ni jambo la heri kuona Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Samia imekuwa sikivu kwa wadau wa habari.

"Tunatarajia pia, sheria itaangalia namna ambavyo itawapa nafasi wanataaluma ambao wamekaa kazini kwa muda mrefu na wana uwezo wa kufanya kazi yao kwa weledi kutekeleza majukumu yao bila vikwazo. Pia,ni matarajio ya wengi kuona vyombo vya habari katika Taifa letu vinakuwa na kutengeneza mapato ambayo yatawezesha kulipa malimbikizo ya madeni pamoja na kutoa mishahara ya uhakika kwa wafanyakazi wao,"amesema Maumba.

Pia amesema kuwa, kwa kuwa Serikali imeonesha nia njema kwa tasnia ya habari ni vema pia na wanahabari kuendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha wanaripoti taarifa sahihi na za uhakika ili kuweza kusaidia kuharakisha maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

"Kikubwa zaidi tuzidi kuzingatia maadili ya taaluma hii ya habari, tuwe wasikivu, wavumilivu na wafuatiliaji wa mambo kwa usahihi. Hatua itayotuwezersha kutekeleza majukumu yetu kitaaluma kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi,"amesema Maumba.

Tangu aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka jana, Mheshimiwa Rais Samia aliudhirishia ulimwengu kuwa, tasnia ya habari ni muhimu kwa ustawi bora wa maendeleo ya jamii na Taifa.

Aidha, alianza kwa kuitaka Wizara ya Habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa huko nyuma huku akisisitiza wahusika wafuate sheria, jambo ambalo lilifanyiwa kazi hatua kwa hatua.

Pia, alitaka kanuni ziweke wazi makosa na adhabu zake ili kusiwe na ubabe kwa kuwa Serikali inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni, lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, wafungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari, na kanuni ziwe wazi tusifungie vyombo vya habari kibabe,” Rais Samia aliagiza Aprili, mwaka jana katika hafla ya kuwaapisha makatibu na manaibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

Aidha, miezi kadhaa baadaye Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho sheria za habari ambazo zinaonekana kuwa kikwazo katika taaluma hiyo.

Mheshimiwa Rais Samia aliyasema hayo Mei 3, mwaka huu wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,"alielekeza Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news