Tuache usiri, tufunguke elimu ya Ukimwi-DC Ngoma

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Mhe. Hassan Ngoma ameiasa jamii kubadili mitazamo juu ya utoaji wa elimu kuhusu masuala ya UKIMWI kwa vijana nchini ili kusaidia katika mapambano ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi leo Novemba 26, 2022 wakifuatilia mkutano huo.(Picha na OWM).

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na vijana walioshiriki katika mkutano wa mwaka wa Vvjana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe na wanawake vijana uliofanyika katika ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi leo Novemba 26, 2022.

Mkuu huyo wa wilaya amesema, wazazi na walezi hawanabudi kubadili mitazamo iliyopo juu ya vijana wao na kuamini ni wadogo, pengine hawafai kupewa elimu ya masuala ya UKIMWI bila kujua mazingira yanayowazunguka ni hatarishi.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma akizungumza na vijana wakati wa mkutano wao katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Desemba Mosi, 2022 mkoani Lindi.

"Tunakosea sana kuona vijana hawa ni watoto hii si sahihi, ukweli ni kwamba ni wakubwa kimatendo na mwamko wao kuhusu umuhimu wa kulinda afya zao ni mdogo sana," amesema Mhe.Ngoma.

Ameongezea kuwa, kukosekana kwa uwazi katika malezi umechangia kuharibu tabia za watoto, kwani wameendelea kujiingiza katika matendo maovu bila wazazi kujali.
Mshiriki wa Mkutano wa mwaka wa vijana, viongozi wa dini na wadau wanaotekeleza miradi ya vijana balehe akiwasilicha hoja wakati wa mkutao huo.

Aidha, ameeleza miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI kwa vijana ni matumizi yasiyo sahihi ya simu za mikononi.
 
Mkuu huyo amesema, matumizi hayo yanachangia ongezeko la vishawishi vya kingono kwa vijana hivyo kupelekea kuzima ndoto zao.

Ameongezea kuwa kukosekana kwa taarifa za tahadhari katika familia zetu kumewafanya vijana kutokuwa na hofu juu ya uwepo wa ugonjwa huu.
"Hali ya maambukizi imeongezeka kwetu sababu watu wamekosa hofu kuhusu madhara ya uwepo wa virusi vya UKIMWI wakijitia moyo kwa uwepo wa kinga na matumizi ya dawa za kuzuia mimba,"amesema Mhe.Ngoma.

Pia ametoa rai kwa vijana kuchukua mikakati madhubuti ikiwemo ya kubadili mitazamo na tabia.

"Namna pekee ya kutoka hapa ni kubadili tabia, na hii ni kazi ya familia zetu na viongozi wa kidini.Viongozi wa dini waendeleee kueleimisha tuone namna ya kuvunja ukimya,"amesistiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini Dkt. Leonard Maboko akizungumza wakati wa kongamano hilo.

Pia ameongezea kuwa, kuwepo na mikakati sahihi inayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia katika mapambana hayo.

"Malengo hayatatimia kama mikakati ni dhaifu, hatuwezi kuwa na njia zile zile za mapambano bila kuwa na strategies mpya zinazoendana na mabadiliko haya ya kiteknolojia,"amesema.

Post a Comment

0 Comments