Qatar kutupa karata yake ya kwanza kwa Ecuador leo

NA DIRAMAKINI

MICHUANO mikubwa zaidi duniani (Kombe la Dunia 2022) katika soka inaanza leo Jumapili huku wenyeji Qatar wakianza kwa kutupa karata yao ya mechi ya ufunguzi dhidi ya Ecuador.

Mechi ya ufunguzi ya michuano hiyo ya siku 29 itaanza baadae leo Novemba 20, 2022 kwenye Uwanja wa Al Bayt wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 katika jiji la Al Khor lililopo kilomita 35 Kaskazini mwa Doha.

Timu ya taifa ya Ecuador imecheza michuano mitatu ya FIFA, lakini Qatar wanacheza mechi yao ya kwanza kwa sababu nchi mwenyeji inafuzu moja kwa moja.

Huku Ecuador wakitarajia mabao kutoka kwa wafungaji wake Enner Valencia, Moises Caicedo na Pervis Estupinan; Winga wa Al-Sadd Akram Afif na fowadi wa Al-Duhail Almoez Ali watakuwa turufu ya Qatar katika Kombe la Dunia.

Qatar wamepangwa Kundi A pamoja na Ecuador, Senegal na Uholanzi. Tukio hilo litahitimishwa kwa mechi ya fainali katika Uwanja wa Lusail Iconic wenye uwezo wa kuchukua watu 80,000 mnamo Desemba 18, mwaka huu. (Mashirika)

Post a Comment

0 Comments