Rais Dkt.Mwinyi:Licha ya changamoto za kidunia, Zanzibar imepiga hatua sana

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua, mbali na changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia.
Dkt. Mwinyi amesema hayo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu aliojipangia wa kukutana na waandishi wa habari kila mwisho mwezi na kujibu maswali mbalimbali, tukio linalokwenda sambamba na miaka miwili ya uongozi wake.

Ameeleza kuwa, pamoja na changamoto za kuwepo kwa Ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukrane, Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua, hususani kupitia Sekta ya Utalii na kusema kumekuwepo ongezeko kubwa la watalii wanaozuru nchini.

Amesema kukua huko kwa uchumi pia kumechangiwa na kuongezeka kwa makusanyo katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, akibainisha taasisi hiyo imekusanya zaidi ya shilingi Bilioni 6.7 katika kipindi cha kuanzia mwezi wa Julai hadi Septemba, 2022, sambamba na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Shirika la Bandari ambazo vimekuwa katika kiwango bora cha kukusanya kodi.

Amesema, mapato katika Shirika la Idara ya Bandari yameongezeka kutokana na kuwepo mfumo bora wa makusanyo; hata hivyo akaelezea tatizo kubwa linaloikabili Bandari hiyo ya Malindi kuwa ni kukosekana ufanisi kwa vile imekuwa na Gati moja na hivyo akabainisha azma ya Serikali ya kumpata mwekezaji ili kuiendesha kwa ufanisi.

Dkt. Mwinyi amesema, Sekta ya Uwekezaji nayo imepata mafanikio makubwa, ambapo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 181 yenye thamani ya zaidi ya Dola Bilioni tatu, huku wastani wa wananchi 11,289 wakitarajiwa kupata ajira.

Aidha, Dkt. Mwinyi alisema Serikali inakusudia kufanikisha miradi mbalimbali katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, ukiwemo mradi wa Ujenzi wa Bandari Mangapwani, Ujenzi wa barabara kuu Unguja na Pemba, Ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Karume Pemba pamoja na ujenzi wa barabara za ndani utakaonza mwezi Disemba , 2022 utakaohusisha ujenzi wa ‘Fly over’ katika maeneo ya Mwanakwerekwe na Round About ya Amani.
Amesema, Serikali inatambua kuwepo kwa mfumko wa bei za bidhaa na kuathiri maisha ya wananchi wa kawaida, na kubainisha kuwa jambo hilo linaikabili dunia nzima ikiwemo nchi zilizoendelea.

Amesema hali hiyo inatokana na kupanda kwa bei za chakula pamoja na mafuta, kunakotokana na majanga ya Kilimwengu na akatumia fursa hiyo kuelezea baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza makali, ikiwemo kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma, kuangalia pensheni za wastaafu, kuweka fidia katika mafuta pamoja na kutoa huduma bora bandarini ili kuharakisha utoaji wa bidhaa.

Dkt. Mwinyi amewatoa hofu wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ya kupoteza ajira zao kwa madai ya kuwepo kwa Kampuni ya DNATA.

Amesema Kampuni ya DNATA inashughulikia masuala ya mizigo katika jengo la Terminal III pekee na kubainisha azma ya Serikali ya kuipa kazi kampuni hiyo kuwa inalenga kupata kampuni yenye ujuzi na kutoa huduma bora.

Amesema, kampuni hiyo imeleta ufanisi mkubwa katika kuhudumia uwanja huo, kiasi ambacho Uwanja wa huo umekuwa ukiongoza kati ya viwanja vyote viliyopo nchini kwa kuingiza wageni wengi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amesema, Serikali inatafuta mwekezaji kwa ajili ya kukiendeleza Kiwanda cha Maziwa cha Azam kilichopo Fumba kinachomilikiwa na Said Salim Bakhressa baada ya kusimamisha uzalishaji na kufungwa, ikiwa ni hatua ya kunusuru bidhaa za wazalishaji wa ndani.

Vile vile, amesema Serikali inaangalia namna ya kubadili mfumo wa adhabu kwa makosa ya usalama barabarani ya papo kwa papo, kwa kigezo cha kuwa mfumo uliopo hivi sasa sio bora.

Akigusia juu ya ziara yake ya hivi karibuni nchini Oman, Dkt. Mwinyi amesema Serikali inakusudia kuwarejeshea nyumba zao wananchi wanaoishi Oman ambao waliishi Zanzibar na hatimaye kuondoka, hali ya kuwa nyumba hizo hazikutaifishwa na Serikali; pale watakapothibitisha kwa kuwa na nyaraka halali.

Mapema, Dkt. Mwinyi aliwashukuru wananchi kwa kuendeleeza amani, umoja, na mshikamano, jambo lililoiwezesha serikali kuendeleeza malengo yake ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news