SAUTI YENYE MIKWARUZO

"Unapokuwa na cheo chochote kile katika hii Dunia tambua kuwa watu wanakiheshimu kile cheo chako na siyo wewe. Walio wengi wanajidanganya kuwa zile heshima ni zao, zile bakishishi ni zao, hilo mwanakwetu nakuuma sikio kuwa si kweli heshima na bakishishi zote ni za kile cheo unachokikalia kwa wakati huo".

NA ADELADIUS MAKWEGA

KUNA wakati fulani rais wa taifa mojawapo la Afrika alimpiga ngwara Katibu Mkuu Kiongozi wa taifa lake na kiongozi huyo kurudi zake kwake kupumzika akiugulia maumivu ya ngwara hiyo.

Katibu Mkuu Kiongozi wa taifa lolote ni mtu mkubwa sana, mwenye siri nyingi ambaye anafanya kazi kubwa za maamuzi na kwa karibu mno na rais kuliko mtu yoyote yule.

Huyu bwana alipopigwa mweleka alitulia nyumbani kwake kwa siku kadhaa huku nafasi hiyo akitafutwa mtu mwingine wa kuendeleza kulipiga kasia.

Siku moja vijana wakatumwa kwenda nyumbani kwake,“Tumetumwa tuje kuchukua magari kwa kuwa wewe umefutwa kazi na hauna ruhusa ya kuyatumia tena magari hayo. Pia unawajibu wa kuondoka katika nyumba hii mara moja ili atakayeteuliwa aje kuishi hapa.”

Bingwa aliyepigwa ngwara akiyasikilizia maumivu ya kutenguliwa, maneno hayo ya vijana hawa yalikuwa sawa na kuichukua sindano ya moto na kuichoma katika kidonda kibichi. Mwanakwetu huo ndiyo ukubwa na kila jambo lina tamu na chungu zake, hapa sasa wakati wa machungu umewadia.

Mtu anayeagizwa kutekeleza jambo ni mtu mzuri sana pale unapokuwa na nafasi ya wewe kumtuma kufanya hivyo, kwa mtu mwingine lakini mtu huyo huyo unaweza kumchukia milele pale anapotumwa kutekeleza jambo dhidi yako, ndiyo maana waswahili wanasema, mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu.

“Nimewasikia vizuri sana, huyo aliyewaagiza mjulisheni kuwa uteuzi wangu haujatenguliwa.”

Vijana hawa wakasema, watu wakiondolewa katika nafasi huwa wanachanganyikiwa kabisa, hapa siyo bure, huyu ni miongoni mwao. Wakaufikisha ujumbe kwa simu wakiwa katika makazi hayo muda huo huo. Wakaambiwa kuwa asiwasumbue huyo, kachanganyikiwa huyo, chukueni magari vunjeni geti, ondokeni nayo mara moja na agizo hilo lilitekelezwa sasa hivi.

Unapokuwa na cheo chochote kile katika hii dunia tambua kuwa watu wanakiheshimu kile cheo chako na siyo wewe. Walio wengi wanajidanganya kuwa zile heshima ni zao, zile bakishishi ni zao, hilo mwanakwetu nakuuma sikio kuwa si kweli heshima na bakishishi zote ni za kile cheo unachokikalia kwa wakati huo.

Vijana hawa walipokamilisha zoezi hilo na kwenda zao, sasa ikabaki kazi ya kumuondoa katika nyumba hiyo kiongozi huyo aliyepigwa ngwara.

Wakati wanakwenda kumuondoa katika makazi hayo mahakama ikaingilia kati zoezi hilo na zoezi la uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi mpya wa taifa hilo. Hoja ilikuwa kuondolewa kwake kulikuwa haramu na taratibu hazikufuatwa, kwa hiyo likawekwa zuio la mahakama.

Mwanakwetu sifahamu kama ndugu huyu aliyepigwa ngwara alikwenda mahakamani akaweka zuio au ilikuwa vinginevyo, ninalolifahamu ni kuwa ndugu huyu baada ya kupigwa ngwara tu vijana walimfuata nyumbani wakampokonya magari na kutaka kumuondoa katika nyumba ya serikali kwa nguvu na hapo hapo katazo la mahakama likafika.

Wakati haya yanaendelea mie (mwanahabari) nikawa nafuatilia tukio hilo kwenye hili taifa, kwa bahati mbaya taifa hili wanazungumza mno Kiingereza. Je ninapataje taarifa ya ukweli wa mambo kutoka kwa mzungumzaji mzuri wa Kiswahili?.

Mwanakwetu nikakumbuka wakati ninasoma pahala fulani nilikuwa na rafiki zangu wawili kutoka taifa jirani na Tanzania wakitoka makabila hasimu ya taifa hilo, huku wakilipiwa karo chuoni hapo na shirika moja la dini.

Vijana hawa walikuwa Wakatoliki wazuri mno, japokuwa walilipiwa karo na fedha zingine za matumizi chuoni hapo na shirika hilo la dini, lakini ule utafauti wa makabila yao uliwatenganisha mno na kushindana baadhi ya mambo, kwa kuwa walikuwa rafiki zangu wa karibu hilo nililibaini mapema sana katika mafunzo hayo ya ujuzi chuoni.

Wakati tunasoma muda mwingine pesa zao zilikuwa zinachelewa kidogo katika mifumo ya kibenki huku mimi tayari nilikuwa mtumishi, nina mshahara tukawa tunasaidiana na ndugu hawa na pesa zao zikiingia katika akaunti zao wananirudishia. Wakawa wanakuja kwangu nilipopanga, tunapika chakula, tunakula pamoja na maisha yaliendelea na kila Jumapili tunasali pamoja.

Mmoja kati ya hawa vijana wawili waliporudi kwao akawa mwanadiplomasia wa taifa lake katika taifa lingine la Afrika, taifa hili lingine la Afrika ndilo lililompiga ngwara katibu wake.

Nikamtafuta ndugu yangu huyu kwa kuwa sisi sote ni ndugu, kwa maana ni mtu ninayezungumza naye sana, rafiki yangu wa karibu, mtu niliyetoka naye mbali, niliyesaidiana naye chuoni na hawezi kunificha jambo liwe baya au zuri. Ndugu yangu huyu hakuupingua urafiki wetu katika hili, akaniambia maneno haya,

“Mahakama katika taifa hili ina nguvu yake vizuri sana, Mahakama inapotekeleza majukumu yake serikali inawajibu wa kutulia tu na hicho ndicho kinachoendelea.”

Akaongeza kusema kuwa hapa kabla kiongozi hajafanya maamuzi yoyote dhidi ya mtu yoyote yule lazima ajiulize mara mbilimbili kuogopa migogoro.

Jambo hilo linasaidia mno viongozi kukaa pamoja na kuzungumza madhaifu yao kabla ya umma kufahamu lolote lile.Katika hili kiongozi huyu alifanya tofauti na ndiyo maana kuna kelele nyingi hadi nyinyi mmefahamu.

“Kwa mfumo huu wa kuhoji maamuzi ya rais kwa mataifa yetu, hapa tunaweza kusema inakuwa kazi kuendesha serikali yake, kwa mifumo ilivyowekwa na ndiyo maana mambo yako hivyo, lakini wao wenyewe wamezoea na sisi tunashangaa hilo tumeliona na tumeshauri hata nyumbani kwetu.”

Jambo hilo linasadia mno kupunguza viongozi wenye nyadhifa za juu kufutwa kazi kila mara na kujenga uimara wa serikali akiongeza kuwa, “Tabia ya kufutana kazi si nzuri sana kwa kuwa inajenga tabia ya wananchi kuzoea hali hiyo na kuona ni jambo la kawaida na wanaweza hata kutamani kumfuta kazi hata kiongozi mkubwa wa taifa lao katika chaguzi zao kwa kuona ni jambo la kawaida kawaida tu.”

Ndugu yangu huyu aliomba nisitumie sauti yake kama ilivyo bali niiwekee mawimbi ili msikilizaji asitambue ni nani aliyekuwa akizungumza na mwanakwetu. Kweli hilo lilifanyika na majukumu yangu yalitekelezwa kwa kutumia sauti yenye mikwaruzo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news