Baada ya kugawa dozi ya 5G, Simba SC yapiga zoezi la nguvu

NA DIRAMAKINI

KIKOSI cha Klabu ya Simba kimefanya mazoezi leo baada ya mapumziko ya siku mbili ikiwa ni maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Mazoezi hayo yamefanyika katika dimba lao la Mo Simba Arena liliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Wachezaji wote wamefanya mazoezi isipokuwa Jimmyson Mwanuke na Israel Patrick ambao bado ni majeruhi ambapo Novemba 9, mwaka huu klabu hiyo itakutana na Singida Big Stars.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka klabuni hapo, wachezaji walipewa ruhusa ya kwenda kukutana na familia zao baada ya ushindi wa mabao 5-0 waliopata Jumapili ya Oktoba 30, 2022.Wakiwa wenyeji, Simba SC iliwashushia kipigo hicho Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanange wa nguvu uliopigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC yalifungwa na viungo, Mzawa Muzamil Yassin dakika ya 38, Msenegal Pape Ousmane Sakho mawili dakika ya 48 na 90 na mshambuliaji Mzambia, Moses Phiri mawili pia, dakika ya 63 na 73.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news