Serikali yatoa maagizo kwa Shirika la Mawasiliano nchini (TTCL)

NA IMMACULATE MAKILIKA-MAELEZO

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetakiwa kuhakikisha linatatua kero ya mawasiliano inayowakabili wananchi wa Vijiji vya Mlengu na Kigala vilivyopo katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kukamilisha ujenzi wa minara itakayosaidia kutoa huduma ya mawasiliano ya simu kwa wananchi.
Akitoa agizo hilo jana katika Kijiji cha Kigala wilayani Makete wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miundombinu mbalimbali ya watoa huduma za mawasiliano katika wilaya hiyo, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma za mawasiliano sambamba na kutumia fursa hiyo kwa kufanya biashara na hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla na hivyo kuiagiza TTCL kukamilisha ujenzi wa mnara uliopo kijijini hapo.

“Tulianza kujenga huu mnara mwaka 2019 lakini haukukamilika kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Uviko-19 kwa vile vifaa vinavyotumika hapa vinaagizwa kutoka nje ya nchi, hata hivyo kwa sasa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati hivyo nawaagiza TTCL kuwa ifikapo Disemba 26, 2022 kuhakikisha wamekamilisha ujenzi wa mnara huu na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kigala,” amesema Naibu Waziri Kundo.

Aidha, Naibu Waziri Kundo amebainisha kuwa msingi wa ziara yake ni pamoja na kubaini uwepo wa minara ya huduma za mawasiliano pamoja na ubora wa kiwango cha huduma kinachotolewa sambamba na kuwaeleza watoa huduma kutatua changamoto zitakazojitokeza.

Kwa upande wake, Meneja wa TTCL Mkoa wa Iringa na Njombe, Chavala Matona amesema mradi huo ambao umefadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unalenga kutatua changamoto ya mawasiliano kijijini hapo wameanza ujenzi wa mnara unaogharimu shilingi milioni 300 na kuwa vifaa vyake vyote vipo tayari “Tutahakikisha kuwa ujenzi wa mnara huu unakamilika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, pia nitakutaarifu kuwa mnara huu umeanza kutoa huduma kwa wananchi hawa”.

Naye, Afisa Tarafa ya Ikuo, Albert Luwondo ameeleza kuwa kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto ya mawasiliano kwa kipindi kirefu sasa hivyo ameishukuru Serikali kwa dhamira yake ya kwa kutatua changamoto hiyo.

“Tunafurahishwa sana kuona Serikali kupitia Wizara inatuletea mnara wa mawasiliano ni matumaini yetu changamoto hizi za mawasiliano zitaisha hapa kwetu na sisi tutanufaika kwa kuwasiliana pamoja na kufanya biashara zetu za mbao kwa kuwa sasa tutakuwa na mawasiliano ya uhakika,” amesisitiza Luwondo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news