Siku 12 kabla ya wadau wa habari, Serikali kukutana, nao wabunge waonesha nia njema

NA DIRAMAKINI

IKIWA zimebaki siku 12 kabla ya wadau wa habari na Serikali kufanya hitimisho la makubaliano ya mapendekezo ya Sheria ya Habari kwa ajili ya kuyapeleka ngazi nyingine,baadhi ya watunga sheria wameahidi kulichukulia jambo hilo kwa upekee ili kuwezesha tasnia ya habari nchini kutekeleza majukumu yake kwa uhuru.
Wameyasema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Wadau wa Haki ya Kupata Habari nchini (CoRI), kwa lengo la kuongeza ufahamu kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.

Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma leo Novemba 10, 2022 ambapo kiliongozwa na mmoja wa wajumbe wa CoRI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.
Hayo yanajiri ikiwa ni siku moja imepita baada ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye kusema kuwa, Novemba 22, mwaka huu wanatarajia kukutana na wadau hao.

Mheshimiwa Nape ameyasema hayo Novemba 9, mwaka huu wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) jijini Dodoma.

Amesema,Serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo, lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutano kutoka kwa wadau wa habari.

Kwenye kikao hicho na CoRI, Waziri Nape amesema,Serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya Sheria ya Habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali kitakachofanyika Novemba 22, 2022, jijini Dar es Salaam.

‘‘Serikali tupo tayari kupeleka mabadiliko ya sheria ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho. Baada ya kikao hicho tutakubaliana tuliyokubaliana na ndio yataenda,"amesema Nape.
Amesema, haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.

‘‘Sisi kama serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema. Isingefaa kwenda na mabadishano bungeni. Mpaka sasa kuna maeneo ambayo bado hatujakubaliana na kikao hicho cha mwisho ndio kitatoa mwelekeo wa mapendekezo yote.

‘‘Sisi kama tupo happy (tunafuraha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’amebainisha Waziri Nape.

Wadau

Aidha, katika kikao cha leo Novemba 10, 2022 James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), pamoja na Balile waliwapitisha wabunge hao kwenye baadhi ya vipengele vya Sheria ya Habari ya mwaka 2016 na mapendekezo ya wadau wa habari.

Pia wabunge hao walipata nafasi ya kuuliza maswali ambayo baadaye yalitolewa ufafanuzi kutoka kwa Balile na Marenga.
Wabunge hao walieleza kufurahishwa na umoja wa wadau wa habari ulioundwa kwa ajili ya kusukuma mbele mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.

Baada ya kukabidhiwa nakala za mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari, waliahidi kuendelea kufanyika kazi na hatimaye kuwa na uelewa wa juu ya jambo hilo litakapofikishwa mbele yao, wapate kuishauri serikali kwa malengo mapana ya taifa.

Kwa nini?

Wadau wa habari wanaeleza licha ya nia njema ya Serikali kuja na sheria hizo,Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari, 2016 inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 5, 2016 na kuridhiwa na Rais Novemba 16, 2016.

Wanadai kuwa, baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza, pia vinakiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi.

Ibara ya 18 inatoa haki kwa kila mtu kuwa na uhuru wa maoni na kueleza fikra zake, kutafuta, kupokea habari bila ya kujali mipaka ya nchi, uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano hayo.
Aidha, Katiba pia inatoa haki kwa kila mtu kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu katika jamii.

Wamesema, dhamira ya Serikali ya kutunga sheria na kanuni za kusimamia sekta ya habari ni njema kwa lengo la kuongeza ufanisi na ustawi bora, lakini kupitia sheria nne zinazosimamia habari zinahitaji maboresho katika baadhi ya vifungu ili kuepuka migongano ya maslahi, upendeleo, urasimu na wakati mwingine manyanyaso kwa wadau wa habari nchini.

Mbali na Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016,pia kuna Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 ambayo inasimamia radio, TV na Mitandao ya Kijamii, Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 zikiwemo kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 ziliyogawanywa katika vipengele mbalimbali.

"Kifungu cha 5 cha Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016, kipengele hiki kina vifungu viwili ambavyo vinaleta shida kidogo. Kuna kifungu cha 5( l) na kifungu cha 5 (e) kifungu cha 5(e) kinampa Mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kusajili magazeti na hapa tumeona tatizo kubwa katika kusajili magazeti.
"Tulisema mwaka 2014, 2015 na mwaka 2016 wakati sheria hii ipo kwenye mchakato wa kupitishwa kwamba kifungu hiki kina nia ovu hatukueleweka. Lakini tumeshuhudia jinsi magazeti ya Mawio, Mwanahalisi, Mseto na Tanzania Daima yalivyofungiwa na wakati mwingine kunyang'anywa leseni kabisa yasifanye biashara na hapa tunasema kwamba kifungu hiki kifutwe, kirejeshwe kama ilivyokuwa zamani ambapo mtu akisaji gazeti linakuwa la kudumu isipokuwa asipochapisha ndani ya miaka mitatu ndipo leseni yake inakuwa inajifuta.

"Sasa kwa kufanya hivi unapofuta leseni au unasitisha unakuta unaathiri mawasiliano kati ya wasomaji na chombo cha habari kilichofungiwa, lakini sio hiyo tu kuna wafanyakazi wengi ambao wanafanya kazi kwenye magazeti kwenye radio na kwenye TV nao pia wanaathirika,"anasema Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Deodatus Balile.
Marega ametolea mfano vifungu vya 4(2), 5(2), 6(2), 7(1) (g), 7(2)(b), 7(3)(b), 8(2), 9(b), 10(2), 11(2), 12(2), 13(2),14(2)(a), 14(2)(b), 15(2), 16, 17(2), 18(2), 19(2), 20(2), 21(2), 22(1), 22(2), 23(2), 24 (2)(a), 24(2)(b), 26(3), 27, 29 na 45(3) ambavyo amesema kuwa, vimebebwa na neno "Not Less Than" likimaanisha 'Si Chini Ya' ambavyo kwa tafsri ya haraka vinaonekana kuwa ni changamoto.

"Mapungufu haya ya kutumia 'not less than' yanafungua milango kwa wale ambao wanatoa maamuzi kwa mfano mahakimu au majaji wakati mwingine kuweka adhabu kubwa zaidi na asiweze kutoa adhabu ambayo inalingana na kosa lililotendwa, au adhabu zingine wanazoona, tunasema sheria inapaswa ioneshe ukomo wa adhabu, mfano maneno kama 'not more than' (si zaidi ya) yanaweza kutumika ili kutenda haki na usawa,"amesema.

Kwa nyakati tofauti, waandishi na wadau mbalimbali katika wameieleza DIRAMAKINI kuwa, panapotokea tofauti baina ya wamiliki wa vyombo vya habari na Serikali, hadi kusababisha vyombo husika kufungiwa, waathirika wakubwa ni wafanyakazi ambao sehemu hiyo imekuwa ikiwapa kipato cha kuendesha familia zao.
"Awali ya yote, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameonesha kutujali sana wanahabari na tasnia hii kwa ujumla.

"Ule moyo tu wa kuonesha utayari wa tasnia hii kuthaminiwa zaidi katika Serikali yake inatupa majibu kuwa, hata kasoro ndogo ndogo ambazo zinaonekana katika vifungu vya sheria hizo zitafanyiwa maboresho na tutafanya kazi kwa uhuru na vyombo vya habari thamani yake itarudi kwa kasi,"anasema mmoja wa wadau wa habari katika mazungumzom na DIRAMAKINI.

Pia amefafanua kuwa,panapotokea hatua ya vyombo vya habari kukosa biashara au kunyimwa matangazo kunachangia wamiliki wengi kuamua kusitisha biashara na hata wakati mwingine wanashindwa kulipa malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi na kodi mbalimbali za Serikali.

"Ni shauku yetu kuona siku moja kila chombo cha habari ambacho kina leseni halali nchini, kinapewa biashara na taasisi yoyote ya umma au binafsi bila kujali ukubwa au udogo wake, hii inamaanisha nini? Wakipata biashara inachochea kasi ya uwekezaji, fursa za ajira na hata kuwa na mwamko wa kulipa kodi kwa wakati serikalini, hivyo kuwezesha ustawi wa uchumi wetu. Sekta ya habari ni muhimu sana,"amesema.

Katika hatua nyingine, Wakili wa Kujitegemea James Marenga anasema, hatua ya kosa la kashfa kugeuzwa jinai, inaongeza hofu na sintofahamu kwa wanahabari nchini.

“Vifungu vya 35, 36, 50(1)(a)(ii) vinafanya kosa la kashfa kuwa ni kosa la jinai badala ya kuwa ni kosa la madai. Tunapendekeza kuwa, mashauri yote yatakayotokana na kashfa yaendeshwe kama kesi za madai sio jinai,” ameeleza Marenga.

Amesema, madhumuni ni kuhakikisha vikwazo katika uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza vinaondolewa.

Mwanasheria huyo amesema, kugeuza kashfa kuwa ya jinai kunaleta hofu na kufifisha haki ya kujieleza na kutoa maoni.
“Kifungu cha 37 kinasema kwamba, uchapishaji wa kashfa ni kosa la jinai isipokuwa kama jambo lililochapishwa ni la kweli na limechapishwa kwa manufaa ya umma; pia kama uchapishaji huo umetolewa kama upendeleo wa kutoshitakiwa (privileged) kwa kashfa na ulikuwa ni manufaa kwa umma,” amesema.

Baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vinavyolalamikiwa ni pamoja na 7 (2) (b) (iii) (iv) and (v), 7 (3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i), (j),8, 13, 14, 19, 20, 21, 24, 25, 26, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54 58 na 59 vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari Na. 12 ya 2016.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news