TETEMEKO INDONESIA:Mvulana miaka sita aokolewa hai baada ya kukaa kwa siku mbili chini ya vifusi

NA DIRAMAKINI

MTOTO wa kiume mwenye umri wa miaka sita ametolewa kwenye vifusi vilivyoporomoshwa na tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watu wengi nchini Indonesia, baada ya kukaa kwa siku mbili chini ya vifusi bila chakula wala maji.
Uokoaji huo ambao unatajwa kuwa wa miujiza juzi, unakuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya tetemeko hilo kupiga katika mji wa Cianjur Magharibi mwa Java.

Pia uokoaji huo ulifufua matumaini kwamba walionusurika bado wanaweza kuondolewa kutoka kwenye mabaki hayo siku chache baada ya tetemeko hilo kubwa ambalo lilipiga siku ya Jumatatu, na kuua takribani watu 271.

"Tulipogundua kuwa Azka yuko hai kila mtu aliangua kilio, nikiwemo mimi," mfanyakazi wa kujitolea wa eneo hilo Jeksen Kolibu mwenye umri wa miaka 28 aliiambia AFP siku ya Alhamisi. "Lilikuwa ni jambo la kusisimua sana, ilionekana kama muujiza."

Video ilionesha waokoaji wakimtoa mtoto Azka kutoka katika nyumba iliyoharibiwa katika wilaya iliyoathirika zaidi ya Cianjur, Cugenang akiwa amevalia shati la buluu na suruali.

Mwanamume aliyemtoa kwenye kifusi alimkumbatia kwa mikono yote miwili, huku mfanyakazi mwingine wa uokoaji akiwa amevalia kofia ngumu ya rangi ya chungwa akiwakimbilia kumshika mtoto huyo mkono, picha zilizotolewa na utawala wa wilaya ya Bogor ya Java Magharibi zilionesha.

Azka ambaye jina lake la mwisho bado halijajulikana, kisha alionyeshwa akinywa kinywaji kwa utulivu, kilichoshikiliwa na askari huku mfanyakazi mwingine wa dharura akimfuta nywele zake.

Mama yake alikufa katika tetemeko hilo la ardhi na mwili wake ulipatikana saa chache kabla ya uokoaji wa Azka, mfanyakazi wa kujitolea aliiambia AFP siku ya Alhamisi. "Kisha mvulana huyo alipatikana karibu na bibi yake aliyekufa,"Kolibu alisema.

"Hatukutarajia angekuwa hai baada ya saa 48, ikiwa tungejua tungejaribu zaidi usiku uliopita," alisema. "Kwa miaka yote tangu niwe mfanyakazi wa kujitolea, sijawahi kuona kitu kama hiki.

"Azka hakutoa sauti, hakulia kuhitaji msaada hata kidogo," Kolibu alisema. "Hata alipotolewa kwenye vifusi bado alikuwa na fahamu na hakusema lolote. Alionekana kuchanganyikiwa sana.”

Kwa mujibu wa mamlaka huko Indonesia, wengi wa waliokufa katika katika tetemeko hilo walikuwa watoto shuleni na majumbani mwao wakati tetemeko hilo lilipopiga.

Aidha,mamlaka zilisema kuwa, takribani watu 40 bado hawajulikani walipo, kwani waokoaji walicheleweshwa na mvua inayonyesha na uwezekano wa kusababisha vifo. Lakini juhudi za kuwatafuta wale ambao bado hawajulikani waliko ziliendelea.

Post a Comment

0 Comments