TRA yatoboa siri, yasema hakuna kutumia mabavu

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Uledi Abbas Mussa amesema kitendo cha kulipa kodi bila shuruti ni uzalendo wa hali ya juu na ndiyo maana mamlaka hiyo imekuwa ikionesha ufanisi katika makusanyo mara kwa mara.
"Kitendo cha kulipa kodi bila shurti ni uzalendo wa hali ya juu na sisi ndugu wanahabari mtakumbuka Mheshimiwa Rais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan) alituelekeza kwamba tujenge utamaduni wa kukusanya mapato ya Serikali bila kutumia mabavu na ndio maana tunawaelekeza maafisa wetu kukusanya mapato bila kutumia mabavu.

"Tunataka walipa kodi wajisikie huru kabisa, tunataka tukae nao, wenye matatizo tukubaline jinsi gani malimbikizo ya kodi zao watayalipa bila kuathiri biashara zao.

Mussa ameyasema hayo leo Novemba 15, 2022 wakati wa kikao kazi baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini.

"Haiwezekani hata siku moja, mmewashawahi kukuta mfugaji anamchinja kuku aliyeatamia au anayetaga mayai mimi sijawahi kumkuta hata kama ni sikukuu ya Krismasi au mwaka mpya yuko radhi akanunue mbuzi mwingine au kuku mwingine siyo anayetaga.

"Kwa hiyo walipa kodi tunawangalia kwa macho yote mawili ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kufanya biashara zao ili waweze kuendelea kuwa walipa kodi wazalendo na waaminifu."amesema.

"Wahariri na waandishi wa habari kwa ujumla ninyi ni wadau muhimu sana, katika jukumu letu la ukusanyaji mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
"Kwa hiyo, leo ni siku muhimu sana kwetu, ikizingatiwa sisi TRA ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Shukrani kwa Mlipa Kodi kwa mwaka 2022. Aidha kwa dhati kabisa napenda kuupongeza uongozi mzima wa TRA kwa kuja na wazo hili na namna ya kipee kabisa na kuwashukuru na kuwatambua walipa kodi.

"Hatua hii inadhihirisha TRA inathamini mchango wa walipa kodi katika makusanyo ya mapato ya Taifa letu ambayo yanaiwezesha Serikali yetu kutekeleza mambo mbalimbali ya kuhudumia jamii.

"Mambo hayo ni pamoja na ulinzi na usalama, afya, elimu na uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi sote tunafahamu kuwa kila mara TRA imekuwa ikitangaza mafanikio ya makusanyo na hivi karibuni tumeshuhudia makusanyo yakiongezeka kwa kiasi kikubwa sana, ukiwauliza viongozi wa TRA chimbuko la mafanikio haya watakujibu kuwa sababu ya mafanikio ya ukusanyaji wa mapato ni elimu kwa walipa kodi.

"Ni elimu waipatayo na wanayoendelea kuipata kupitia ninyi waandishi wa habari na wahariri, kwani mmekuwa kiungo kikubwa kati ya TRA na walipakodi. Walipakodi wanapata elimu na hamasa ya ulipaji kodi bila shurti kupitia vyombo vyenu vya habari. Hongereni sana.

"Aidha, kipekee naomba kutumia fursa hii kutoa pongezi za dhati kabisa kwa walipa kodi wote nchini kwa ulipaji ulio mzuri hata kuisababishia TRA kukusanya mapato ya jumla ya shilingi trilioni karibu sita katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba,mwaka huu wa fedha, kiasi hicho cha makusanyo sawa na ufanisi wa asilimia 99.1 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 6.1.

"Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 14.6 ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita.

"Kwa maneno mengine mwaka huu wa fedha tulijiwekea lengo kubwa zaidi la kukusanya mapato ya Serikali ikilinganishwa na mwaka uliopita, vinginevyo tungeendelea na lengo la mwaka huo kwa vyovyote vile tungeshindwa kutimiza lengo lililowekwa.

"Kwa sababu hili ongezeko la asilimia 14.6 ukilinganisha na mwaka uliopita maana yake tungesema kwamba kama tungesema tujiwekee lengo lile lile la mwaka jana, mwaka huu tungekuwa tunakusanya kwa kiwango cha chini kwa hiyo mara nyingi takwimu ambazo TRA inazitoa ukizichambua sana utaona kwa kipindi hiki kuna hatua kubwa sana ambazo zimefanywa na wadau wetu na ninyi wanahabari mna mchango mkubwa sana.

"Tukaona kwa nini tusikutane na ninyi leo tuzungumze, tupeane mawazo inawezakana baadhi ya hatua tunazozichukua zinahitaji maboresho,lakini pili ninyi pia ni sehemu ya TRA ingawa hampo katika ofisi zetu.

"Vitendo vyenu havina tofauti na watumishi waliopo TRA, kwa maana hiyo tunawashukuru sana. Kwa mwezi Septemba TRA imekusanya takribani kiasi cha shilingi trilioni 2.3 ikilinganishwa na lengo la makusanyo ya shilingi trilioni 2. 2 makusanyo haya bado yanaonesha ufanisi wa asilimia 100. 5 ya lengo tulilojipa maana yake ni kwamba kuna dalili nzuri sana ya ukusanyaji wa mapato huko tunakoelekea na tumepata mafanikio haya tukiwa katika mazingira magumu sana Kimataifa.

"Sote tunajua kulikuwepo janga la Corona kabla halijapoa janga hivi sasa tuna cita kati ya Urusi na Ukraine. Mambo haya mawili yameathiri uchumi wa Dunia ikiwemo Tanzania, lakini pamoja na mazingira hayo magumu unalikuta Taifa ketu linaendelea kwa kushirikiana na wananchi wake kukusanya mapato ya kuridhisha kwa ajili ya maendeleo.
"Sasa kwa nini tusiwashukuru walipakodi kwa hili kwa ajili ya Taifa letu, kwa nini tushiwashukuru wahariri na waandishi wa habari makundi hayo mawili ndugu Mwenyekiti (Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF) naomba niseme kwamba tuendelee na ushirikiano huu kati yenu na Mamlaka ya Mapato Tanzania,"amefafanua Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa, ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na vyombo vya habari ni fursa moja wapo ya kutunisha makusanyo ya Serikali kutoka kwa walipa kodi mbalimbali nchini.

"Nikushukuru kwa kuelewa kwamba wahariri wanaanzia kwenye vyombo vya habari, niseme kuna haja ya TRA kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari.

Tuandae utaratibu wa kuwa na kikosi maalum cha wahariri na waandishi watakaopata mafunzo maalumu sio tu kuhudhuria semina, tuandae semina, wafundishwe waandishi masuala ya kodi ili waweze kufuatilia nchi nzima.

"Tukishafanya hivyo tutakuwa na ushirikiano mzuri na habari za TRA na kodi zitaongezeka ninakuhakikishia wahariri na waandishi wa habari wakifanya kazi kwa ufasaha katika hicho mnachokikusanya kuongeza trilioni tano nyingine si ajabu.

"Kwa sababu watawajulisha watu haki na wajibu wa kulipa kodi na watu wakishajitoa kwa wingi kodi zikalipwa kwa wakati na ongezeko litakuwa kubwa.

"Kwa kweli TRA mnafanya kazi nzuri ila nina shida moja kwenye mifumo ya kitaasisi kwa sisi ambao tunalipa pay as you earn, SDL, na VAT zile tarehe 7 na 20 ni kichomi kweli imefika wakati tunaamka saa 8:00 usiku, tunaamsha watu wetu wa akaunti ili waweze kupeleka kusudi tusipate faini.

"Na mmeona mara kadhaa ninyi wenyewe TRA mnaongeza muda siku tano hadi siku 10. Tuombe sana hii mifumo izungumze vizuri kiasi kwamba hata mtu kupitia kishikwambi au simu yake ya nkononi aweze kufanya hizo ritani kwa wakati asipate usumbufu.

"Kuna wakati nilifika kwenye ofisi zenu. Kuna wakati ukifika huu muda wa kulipa kodi unakuta watu wengi kwenye korido na maafisa wenu wanasema wewe nenda ujaribu, lakini anajua ikishafika saa 6:00 usiku hiyo tarehe 20 hiyo kujaribu itakuja na faini. Tunaomba sana kama ni uwekezaji mjaribu kuufanya.

"Mimi sitaki kuamini kama kunaka kahujuma kanapita ndani humo, kwamba makusanyo yamekuwa makubwa yanataka yashuke kidoge, sasa sijui mnaweza mkahujumiana wenyewe ndani kwa ndani.

"Mkienda angalieni, lakini hizo zinazungumzwa kuna taasisi moja..ilikuwa saa ya kulipa wanazima swichi kwa hiyo wanahangaika malipo hayaendi wikiendi,baadaye wanalalamika watu wanakuja wanaiwasha Jumatatu kwa hiyo na ninyi angalie inawezekana hayo mafanikio sio wote wanayafurahia kunaweza kuwemo kati yenu mmoja au wawili badala ya kukusanya trilioni 2.3 muishie kukusanya trilioni moja.

Wakati huo huo, Balile amesema, kwa muda mrefu vyombo vya habari hususani magazeti wamekuwa wakitozwa faini ya kutotumia mashine katika uuzaji magazeti.
"Mwenyekiti embu fikiria wauza magazeti kwenye barabara wanavyokimbizana na wateja, kisha huyo huyo muuza magazeti ashike mashine za EFDs za kila gazeti ili mteja anaponunua amkatie risiti hii ni ngumu na haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani popote,"amebainisha Balile.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi TRA ameongeza katika kuadhimisha Wiki ya Mlipa Kodi,Novemba 17, mwaka huu TRA inatarajia kuwatambua walipa kodi bora ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango wao kwani pia wamekuwa ni chimbuko la mafanikio katika makusanyo ya kodi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TEF, Bakari Machumu amepongeza jitihada zinazofanywa za kuweka mazingira mazuri ya kulipa kodi hilo linatia moyo.

Machumu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) amesema, kila mmoja akiwa na uelewa wa pamoja na shirikishi hata mapato yataongezeka.

Aidha,katika kikao kazi hicho baadhi ya wahariri walielezea kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabiashara na kuwa kero kwao na hata kukwamisha zoezi la ulipaji kodi kwa hiari ikiwemo utozwaji wa ushuru mkubwa kwenye magari bandarini.

Pia walieleza kuwepo kwa kero ya gharama za ununuzi wa mashine za EFDs ambapo wameshauri mashine hizo zigawiwe bure na TRA ili kazi yao iwe kukusanya kodi tu, hoja mbalimbali zilizojitokeza mamlaka hiyo imeahidi kuzichukua kwa ajili ya kwenda kuzifanyia kazi ili kuongeza ufanisi.

Post a Comment

0 Comments