VIFAFIO yapeleka elimu ya ukatili wa kijinsia Rusoli kupitia tamasha

NA FRESHA KINASA

KATIKA kutokomeza vitendo vya ukatili wa Kijinsia Shirika lisilo la kiserikali la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Musoma mkoani Mara limeendesha tamasha katika Kata ya Rusoli lililohusisha ngoma za asili, zeze, kwaya, na mchezo wa mpira wa miguu uliozikutanisha timu ya Kata ya Rusoli na Kata ya Msanja wilayani humo kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya mapambano ya vitendo hivyo.
Tamasha hilo limefanyika Novemba 4, 2022 katika kata hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wananchi ambapo pia umefanyika mjadala wa hadhara. Ambapo wananchi wamepata fursa ya kutoa maoni yao na kuuliza maswali mbalimbali kuhusiana na suala zima la ukatili wa kijinsia.

Hatua hiyo, ni sehemu ya majukumu ya mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia maeneo ya mialo unaotekelezwa na Shirika hilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Musoma ambao umeanza kutekelezwa mwezi septemba 2022, hadi Aprili 2023 chini ya ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society.
Akizungumza na wananchi waliofika katika tamasha hilo, Meneja wa Shirika la VIFAFIO, Majura Maingu amewataka wananchi wa kata hiyo na Halmashauri ya Musoma kwa ujumla, kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia katika mifumo ya kijamii ikiwemo viongozi wa dini, wazee wa mila na mifumo ya kiserikali kwa hatua za kisheria.

Maingu amewataka pia wanananchi kutambua viashiria vya ukatili wa kijinsia na kuchukua tahadhari mapema kabla ya matukio kutokea, kwani yanapotokea yamekuwa na madhara katika familia na katika jamii ikiwemo kuchangia mmomonyoko wa maadili, ulemavu na kurudisha nyuma maendeleo.
Maingu amesema kwamba, vitendo vya ukatili havipaswi kufumbiwa macho katika jamii bali vidhibitiwe, na kwama jukumu hilo linapaswa kufanywa na kila mmoja ndani ya jamii na wahusika wa vitendo hivyo wafichuliwe.

Pia, amewataka wazazi, walezi na jamii kuungana kwa pamoja kusimamia malezi kwa watoto na kuwapa mahitaji yao ya msingi sambamba na kuwajibika kusimamia haki zao katika kuwaandaa kuja kuwa msaada kwa jamii na taifa kwa siku za usoni.
Aidha, ameiomba jamii kuachana na mila mbaya ambazo hazina faida katika jamii, huku akihimiza kuendelezwa kwa mila nzuri zenye kujenga jamii na kudumisha Mahusiano mema.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Vincent John amewahimiza wananchi hao kuachana na tabia ya kujichukulia hatua mkononi kinapotokea kitendo cha ukatili kwani kufanya hivyo ni kinyume kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Likitokea tukio la ukatili taarifa zitolewe Polisi, Ofisi za watendaji wa kata, vijiji, mitaa, Dawati la Jinsia na Watoto na Ofisi za maendeleo ya jamii na katika mashirika ambayo yanapambana na ukatili hii itasaidia sana," amesema Vicent John.
Boazi Nyeura ni Diwani wa Kata ya Rusoli amelishukuru Shirika la VIFAFIO kwa kuendesha tamasha hilo, ambalo amesema limekuwa na faida kwa wananchi ikiwemo kuwaelimisha kwa kina madhara ya ukatili wa kijinsia, kuwahimiza ushiriki wao katika kutomeza vitendo hivyo na hatua za kuchukua pindi wanapoona matukio hayo.

Mariam Peter mkazi wa Rusoli amesema kuwa, wanaweke wamekuwa wakikumbana na ukatili wa vipigo kutoka kwa waume zao jambo ambalo ni unyanyasaji na ni ukatili usiofaa kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Unakuta mwanaume ameondoka nyumbani anarudi usiku wakati huo hajaacha hata hela ya matumizi mwanamke amepambana na kazi ndogo ndogo amelipwa hela kidogo amenunua chakula watoto wamekula na pia ameacha chakula cha mwanaume. Amekaa amengoja hadi saa nne usiku mwanaume hajarudi anakwenda kulala, mwanaume akija anakuwa amelewa anabisha mlango mwanamke akikawia kufungua mlango tu kidogo anapewa kipigo na matusi huo ni ukatili ambao katika maeneo yetu upo wanaume wanaufanya," amesema Mariam Peter.

Janeth Peter amesema kwamba, wanaume wamekuwa wakifanya maamuzi bila kuwashirikisha wanawake hasa uuzaji wa rasilimali mbalimbali katika familia yakiwemo mazao na mifugo na kutumia fedha zote.

"Mnalima pamoja mazao, mnafuga mifugo katika familia, lakini mwanaume anapotaka kuuza mfugo baadhi yao hawaulizi wake zao au kushirikisha watoto wanauza tu kwa kujiamulia. Mwanamke akiuliza anakumbana na kupigwa au kusimangwa kwamba mali hazimhusu wakati ameshiriki mwanzo mwisho katika uzalishaji huo. Anakaa kwenye ndoa kwa kunyanyasika anaona akiondoka watoto watapata mateso," amesema Janeth Peter.
Jackline Amony amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakifanya ukatili kwa watoto wao kwa kutoa adhabu zisizo endana na umri wao na kosa pindi wanapokosea na hivyo kupelekea baadhi ya watoto kuhama kwao na kwenda kuishi mitaani kitendo ambacho huwafanya wajihusishe na vitendo vya udokozi na tabia hatarishi. Huku wengine wakitumikishwa kufanya biashara ndogo ndogo wazazi wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news