Viongozi wa dini waguswa na ufanisi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA)

NA MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashekhe ya Maadili Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kuwataja hadharani watu wanaodaiwa kujishughulisha na biashara hiyo haramu.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya.

Askofu Mwamalanga ametoa pongezi hizo siku chache baada ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya kujitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya tisa ambapo wanadaiwa kukutwa na kilo 34.89 za heroine jijijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Waliokamatwa ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Dar es Salaam, Kambi Zuberi Seif, Muharami Sultan (40) na John John, maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kwenye kituo hicho.

Wengine ni Said Matwiko, mkazi wa Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule, Rajabu Dhahabu (32) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24), mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (24) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa Kongowe.

“Sisi viongozi wa dini tunaona huu ni ushindi mkubwa kuwahi kutokea hongera sana mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya nchini kwani kwa muda mrefu sasa Watanzania wamekuwa wakipiga kelele juu ya kuibuka upya biashara hiyo haramu,” amesema.

Mwamalanga amesema, kuibuka kwa biashara hiyo kumekuwa kukihusihwa na vyombo vya michezo na baadhi ya madhehebu ya dini, hivyo kuishauri mamlaka hiyo kuongeza nguvu katika mapambano.

Amesema,miaka ya nyuma viongozi wa dini wakiwamo Mashekhe na Maaskofu walitoa orodha ndefu ya waingizaji wakubwa wa dawa za kulevya nchini, lakini hakikufanyika chochote.

“Ndiyo maana tuipongeza mamlaka hii kwa kuthubutu. Hakika tukuombea dua ya ulinzi Kamishna Kusaya kwa Mwenyezi Mungu aendelee kukupa ulizni wa kufanya kazi yako kwa weledi, katika kulilinda Taifa dhidi ya dawa za kulevya.

"Tunahimiza viongozi wakuu wa michezo nchini kujisafisha na kusafisha timu zao ili zisitumike na wahalifu wachache kuliangamiza Taifa kwa tamaa zao za utajiri wa haraka bila baraka,” amesema.

Aidha, Askofu Mwamalanga amesema wanamuomba Kamishna Kusaya kuisafisha mamlaka hiyo kwa kuwaondoa baadhi ya watendaji ambao wanatajwa kuficha wahalifu pindi wanapowakamata kwa kupewa rushwa kubwa za magari na pesa.

“Ni vema chombo kikafanya kazi zake kwa uwazi, bila kulinda wahalifu wanaotumia dini na michezo kusafirisha dawa za kulevya...sisi tumejipa jukumu la kukemea na kutoa ushirikiano wa kila siku kwa mamlaka, ili Tanzania bila dawa za kulevya isomeke kwa vitendo,” amesisitiza.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. 

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. 

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news