Wafugaji Kasulu watakiwa kupeleka ng'ombe kwenye ranchi

NA RESPICE SWETU

MKUU wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Isack Mwakisu amewataka wafugaji wa ng'ombe wilayani Kasulu kuwapeleka ng'ombe wao kwenye ranchi ya kulishia mifugo iliyoandaliwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo.

Amesema kuwa, serikali imetenga ranchi yenye eneo la ukubwa wa hekta elfu hamsini ili wafugaji wapeleke mifugo yao badala ya kuingiza mifugo kwenye hifadhi na kwenye mashamba ya wakulima.

Ameongeza kuwa, ili kuepusha migogoro hiyo serikali imetenga ranchi yenye ukubwa hekta elfu hamsini ambapo mfugaji anaweza akapata eneo la heka moja kwa gharama ya shilingi elfu tatu na mia tano tu badala ya kuendelea kukinzana na serikali.

"Mimi siamini kama kweli kuna mfugaji anayeshindwa kulipia gharama hiyo na kuwapeleka ng'ombe wake kwenye eneo maalumu lililoadaliwa, sielewi ni kwa nini wafugaji hawataki kupeleka mifugo yao huko,"amesema.

Akizungumza kwa hisia kuhusu migogiro ya wakulima na wafugaji, Kanali Mwakisu aliyekuwa akitoa salaam za serikali kwenye kikao hicho aliwatahadharisha wajumbe wa kikao hicho kuwa, kama jambo hilo halitafanyika kuna dalili ya kutokea migogoro hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho wakulima wameanza kupanda mazao ambayo wafugaji wanaweza kupitisha mifugo yao.

"Nilishasema kuwa sitaki kuona damu inamwagika kwenye Wilaya yangu, nawaombeni sana viongozi wenzangu kawaambieni ukweli wafugaji mnaoishi nao huko hakuna eneo la hifadhi litakaloruhusiwa kulishia mifugo wanatakiwa wawapeleke ng'ombe wao kwenye ranchi,"amesisitiza.
Mwakisu alikitumia kikao hicho pia kutoa onyo kwa baadhi ya viongozi wanaotumia jina lake kupokea rushwa na kuwarubuni wafugaji kuwa waendelee kuwepo katika maeneo yasiyoruhusiwa.

"Ninazo taarifa za watu hao mpaka kiasi cha pesa walichochukua, suala hili lipo na linafanyiwa kazi, nawaombeni tufanye kazi pamoja kwa kuzingatia sheria, najua hata kuna shule zilizojengwa ndani ya maeneo ya hifadhi serikali itatoabmaamuzi.," amesema.

Mwakisu aliitaja Shule ya Msingi Katoto iliyopo Kata ya Kagerankanda na shule za msingi za Kacheli na Rugufu Relini zilizopo za Kata ya Rusesa kuwa ni shule zilizo ndani ya hifadhi.

Post a Comment

0 Comments