Wasiojulikana wafukua kaburi na kunyofoa moyo, ulimi, jicho na titi mkoani Mbeya

NA DIRAMAKINI

WATU wasiojulikana wanadaiwa kufukua mwili wa mwanamke, Neema Mlomba (26) na kunyofoa baadhi ya viungo vyake ikiwemo moyo, ulimi,jicho na titi moja.

Tukio hilo limetokea Novemba 7, 2022 katika makaburi ya Kamasuru yaliyopo Kijiji cha Kilasi Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo iliyopo mkoani Mbeya.

Kufuatia tukio hilo la kikatili na aibu katika jamii, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Juma Homera ameagiza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi mkoani humo kufanya uchunguzi wa haraka ili kuwabaini watu waliohusika kutenda tukio hilo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo limetokea Novemba 7, 2022 katika makaburi hayo.

Amesema, baada ya kufukuliwa kaburi hilo baadhi ya viungo vya mwili wa Neema vilinyofolewa vikiwamo moyo, figo, jicho, ulimi na titi moja huku sehemu ya tumbo ikiwa imechanwa pia.

Kamanda huyo amesema, taarifa za awali zimeeleza kuwa Neema alifariki Novemba 5, 2022 katika Hosptali ya Rufaa Kitengo cha Wazazi Meta muda mfupi baada ya kujifungua na maziko yake yakafanyika Novemba 6, 2022.

Pia amesema, ilipofika Novemba 7, 2022 asubuhi, Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu kuhusiana na mwili wa ndugu yao kufukuliwa na kisha baadhi ya viungo kunyofolewa na watu wasiojulikana

Amesema, baada ya kupata taarifa waliambatana na madaktari mpaka makaburini ambapo walikuta mwili wa huo na walipofanya uchunguzi walibaini baadhi ha viungo vimenyofolewa huku chanzo cha tukio hilo kikihusishwa na imani za kishirikina.

Post a Comment

0 Comments