Barbara Gonzalez ataja sababu mbili za kujiuzulu Simba SC

NA DIRAMAKINI

AFISA Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Bi.Barbara Gonzalez ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo katika klabu hiyo kubwa ndani na nje ya Tanzania huku akitaja sababu kuu mbili.

Uamuzi huo ameufikia leo Desemba 10, 2022 kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma akielezea kuhusiana na hatua hiyo aliyoifikia.

"Leo (Desemba 10, 2022) nimeandika barua ya kujiuzulu wadhifa wangu kama Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC kuanzia Januari, mwakani (2023), nimetoa notisi ya mwezi mmoja ili nishiriki kuhakikisha kipindi kizuri cha mpito na makabidhiano na menejimenti mpya,"amefafanua Afisa Mtendaji Mkuu huyo.

Amebainisha kuwa, kwake ni fahari chini ya uongozi wake kwa kushirikiana na Rais wa Heshima, Mwenyekiti wa Klabu, Bodi ya Wakurugenzi, wafanyakazi wenzake, wachezaji wa klabu, benchi la ufundi, wanachama, mashabiki, wafadhili na wadau wao ambapo klabu ilipata mafanikio makubwa ndani na nje ya klabu.

"Ikiwemo kutwaa mataji, kuvutia wafadhili na kuanza kuheshimika kama moja wapo ya vilabu vikubwa vya soka barani Afrika.

"Nimechukua uamuzi huu kwa sababu kubwa mbili, mosi, kutoa nafasi kwa Bodi Mpya ya Wakurugenzi itakayochaguliwa kwenye uchaguzi ujao kupata fursa ya kuchagua Mtendaji Mkuu na Menejimenti mpya itakayoendana na dira yao. Pili kujipa nafasi ya kutimiza ndoto na fursa nyingine kwingineko.

"Nitumie nafasi huu, kipekee kabisa, kuwashukuru wote tuliosafiri pamoja katika ndoto ya kuifanya Simba SC iwe kubwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma, Ni uamuzi mgumu sana kuacha kazi unayoipenda na uliyoifanya kwa moyo wote, lakini ni ukweli pia kwamba mambo yote mazuri huwa na mwisho.

"Simba itabaki ndani ya moyo wangu na kama sehemu ya familia yangu, Ninaahidi kuwa nitaendelea kuwa mwana Simba kindakindaki na balozi mwaminifu wa klabu popote nitakapokuwa. Asanteni sana,nawatakia mafanikio mema! SIMBA#NguvuMoja,"

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news