BUNDI WA GAMBOSHI YA SEHEMU 61

NA WILLIAM BOMBOM

Ghafla BUNDI WA GAMBOSHI alitema mate kwenye ule moto ukazimika, kumbe ule haukuwa moto bali ilikuwa ni nguvu ya madawa. Pale kiwanjani kulikuwa na kundi la wachawi waliokuwa wakifanya shughuli zao.
Kitendo cha kutua eneo hilo kiliwashitua kidogo, kwani kwa upande wao ndio ilikuwa mara ya kwanza kumuona BUNDI WA GAMBOSHI alikuwa ni ndege mkubwa kuliko ndege wote. Hata hivyo madawa aliyokuwa nayo mwilini mwake yalimfanya kila mtu kumuogopa kila alipoonekana.

Tulishuka miguuni mwa BUNDI WA GAMBOSHI kisha tukaanza kutembea kuelekea kwenye majengo ya kambi hiyo.

Kwa usalama wetu tuliamua kumuacha BUNDI WA GAMBOSHI kiwanjani hapo ili kama litatokea lolote iwe rahisi kutusaidia.

Tulipopiga hatua tatu mbele tulikutana na popo wawili waliokuwa wamekaa wanapiga soga. Walikuwa wakizungumza kwa lugha ya binadamu ingali wao ni popo.

Ghafla popo hao walituuliza, "Ninyi ni kina nani?" bila kupoteza muda THE BOMBOM nikawajibu swali lao.

Waliuliza lengo la kuwepo kambini hapo na kama tulikuwa na miadi ya kufika kambini hapo. Nilitamani kuwashughulikia popo hao, lakini nikakumbuka kuwa subra yavuta heri.

Mara yule popo mmoja aliruka na kupanda mgongoni mwa popo mwenzake, punde si punde akapotelea mwilini mwa popo mwenzake.

Yule popo aliyebakia alituomba tusubiri ili wafanye mawasiliano na makao makuu yao, baada ya muda tuliona kundi kubwa la wachawi wakija maeneo tuliyokuwa.

Kumbe yule popo aliyeingia mwilini mwa popo mwenzake ilikuwa ni njia ya kwenda kwa mkuu wao kumtaarifu ugeni uliokuwepo.

Kundi lile lilikuwa na wachawi wapatao kumi, walipofika walituchukua na kutupeleka kwa mkuu wao. Kiongozi wao alikuwa ni mwanamke wa makamo, alionekana kutotufahamu hata kidogo.

Tulijitambulisha kwake lakini hakutuelewa, hatukujua kama ilikuwa ni dharau au laa. Maana kambi yetu ilikuwa ni kambi kubwa kuliko kambi yeyote ukanda huo. Iweje asitufahamu! Mkuu huyu alionekana kuwa na kiburi kwa kumwangalia tu. Alituuliza shida yetu iliyotupeleka kambini kwake, bila hiana tulimwekeza kwa kina.

Alitaka kujua faida ambayo angeipata baada ya kujiunga na kambi yetu. Ni nafasi gani ambayo yeye angekabidhiwa katika muungano huo?.

Miongoni mwa faida ambayo angeipata katika ushirika huo ilikuwa ni kuendelea na uhai wake. Pia angeendelea kufanya kazi za kichawi katika kambi ya kisasa pasipo na bugudha.

Maelezo yetu yalimuudhi na kuanza kutufokea, alituona sie ni wapuuzi sana hivyo akawa anatuchimba mkwala.

THE BOMBOM na wasaidizi wangu tukanywea. Lengo ni kumsikiliza mpaka mwisho wake, aliendelea kutuchimba mkwala. Mwishowe tukachoka na mkwala wake, tukamuaga tuondoke lakini akagoma.

Tayari alikuwa ameshaita wasaidizi wake, tukaamua kuondoka eneo hilo tukajipange namna ya kurudi kumshughulikia.

Kufumba na kufumbua tulipotea machoni mwao, walipojaribu kumwaga madawa ya kutuona tulikuwa tumeshafika uwanjani kule kwa BUNDI WA GAMBOSHI.

Hao tukapanda ndani ya vidole vya bundi huyo kisha tukaondoka. Wakati tunaondoka uwanjani hapo tulibahatika kumuona, mkuu huyo wa kambi na wenzake wakija kwa kasi.

BUNDI WA GAMBOSHI aliruka na kuwaacha wachawi hao wakishangaa, niliamini muda si mrefu tungerudi kuwashughulikia.

Jambo pekee lililonifurahisha kambini hapo, ilikuwa ni kuona idadi ya misukule wengi. Katika kambi hiyo kulikuwa na misukule zaidi ya mia tatu na thelathini.

Endapo tungeiteka kambi hiyo ingekuwa rahisi kuwachukua misukule hao. Kwa mbali tuliwaona wachawi hao wakipotea kwenye upeo wa macho yetu, hii ilitokana na kasi ya BUNDI WA GAMBOSHI.

Wakati huo ilikuwa ni saa tano za usiku, tukaamua kwenda kushuka kwenye kambi ya kichawi ya Mganza. Kabla hatujatua kambini hapo tulibaini uwepo wa mvua kubwa iliyokuwa ikinyeesha kwa nguvu.

Tukaamua kupitiliza mpaka mji wa Mtegowanoti ambao upo mbali kidogo na mji wa Mganza. Hata huko pia tulikuta mvua imepamba moto, wenzangu wakashauri turudi kule Mganza, lakini nikagoma.

Niliwaambia bora tuanze na eneo hilo, tulienda kutua kwenye majengo ya shule ya msingi Mwangaza katika mji huo wa Mtegowanoti.

Ndugu msomaji hapa niseme kidogo, ni mara chache sana kwa mvua kuzuia shughuli za kichawi. Zipo dawa ambazo hutumika kwa ajili ya kuzuia mvua eneo fulani.

Dawa hizo huwa tunachukua kucha za watoto mapacha, uchafu wa kichaa wa kiume, maziwa ya mbwa mweusi tii na mizizi ya miti fulani.

Baada ya kuchanganya mchanganyo huo huwa anapatiwa mtu yeyote ambaye alizaliwa mmoja kwenye tumbo la mama yake ili anuia kitu.

Kama atakosekana mtu wa sampuli hiyo basi dawa hizo hupewa mtu mwenye ulemavu wa ngozi yaani albino kunuia.

Mvua hata iwe kubwa kiasi gani itasimama kunyesha eneo lililonuiwa, mtaendelea na shughuli zenu mlizokusudia. Madawa haya hutumiwa pia kwenye mikutano, sherehe za nje na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Bahati nzuri miongoni mwa wasaidizi wangu, mmoja alikuwa amezaliwa pekee tumboni mwa mama yake.

Hivyo tulimtumia yeye katika kunuia kusimama kwa mvua eneo hilo, baada ya sekunde chache mvua ilisimama.

Tulielekea kwenye kambi ya kichawi iliyokuwa nyuma ya soko la mji huo wa Mtegowanoti. Kabla hatujafika eneo hilo, tulisikia sauti nzito ikitukaribisha katika himaya ya kambi ya kichawi hiyo.

Tulifurahia kupokelewa kwa heshima katika kambi hiyo. Wakati huo tulikuwa tumemuacha BUNDI WA GAMBOSHI kwenye viwanja vya shule ya msingi Mwangaza.

Ghafla tuliwaona paka watatu weupe wakitufuata mbele yetu, walikuwa ni paka wadogo lakini vichwa vyao vilikuwa vikubwa zaidi ya vile vya mbwa.

Walipotukaribia walituita kwa majina, tukabaki tukishangaa kwa paka hao kutufahamu. Kimsingi paka hao hawakuwa paka wa kawaidi bali walikuwa ni binadamu waliokuwa wamechukua maumbile ya paka.

Walituchukua na kutupeleka makao makuu ya kambi hiyo ya kichawi, kule kambini tulikutana na mkuu wa kambi ambaye alitupokea kwa furaha.

Tulizungumza mambo mengi hatimaye tukamuelezea lengo letu, pasi na shaka yeye alikubaliana kuungana na kambi yetu.

Tulizungumza mambo mengi hatimaye tukamuaga kisha tukaondoka, alitusindikiza mpaka shule ya Msingi Mwangaza kisha tukaachana naye.

Tulikwenda kutua kwenye kiwanja cha shule ya msingi Mganza, wakati huo ilikuwa ni saa sita na mvua ilikuwa imekatika.

Tulikwenda taratibu hadi kwenye kambi ya kichawi iliyokuwa kwenye miembe mikubwa iliyopo kwenye mji huo.

Kabla hatujafika kwenye malango makuu ya kuingia kambini hapo, tulikutana na nyuki wa ajabu walioanza kutushambulia.

Nikamwaga dawa wale nyuki wakapukutika kisha tukasonga mbele. Tukaingia kwenye malango ya kambi hiyo, hakukuwa na binadamu hata mmoja katika eneo hilo. Kulikuwa na chura wengi waliokuwa wakiendelea na shughuli zao. Cha ajabu chura hao walikuwa ni wakubwa mithili ya jogoo.

Tuliingia kambini hapo kwa kujiamini, tulipowavuka vyura hao kwa mbele tulikutana na mijusi wengi sana.

Mijusi hao walikuwa na rangi mbili nyekundu na bluu. Kila mjusi alikuwa na shughuli zake, wapo waliokuwa wamebeba mapipa huku wengine wakiwa wanatwanga unga wa mhogo kwenye vinu.

Haya yalikuwa ni mageni sana kwangu, yaani katika kambi hakukuwa na msukule binadamu zaidi ya vyura na mijusi!.

Ndugu msomaji simulizi hii inaelekea mwisho, tafadhali usichoke kufuatilia ili kujua hatima yake.

Mpendwa msomaji kuanzia tarehe 1/1/2023 nitatambulisha simulizi mpya ya KANISA LA KICHAWI itakayokuwa inatoka kila baada ya siku moja.

Ni hadithi ya kusisimua yenye vitisho na taharuki nyingi. Hebu jiandae kuisoma simulizi hiyo itakayokuacha kinywa wazi. Sanjari na hiyo jiandae kusoma simulizi ya KABURI LA RAIS WA HOVYO.

BHUKEBHUKE
THE BOMBOM

Post a Comment

0 Comments