Dkt.Msonde atoa maagizo kwa wajumbe wa timu za usimamizi Mradi wa BOOST

NA ANGELA MSIMBIRA

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde amewaagiza Wajumbe wa Timu za Usimamizi wa Utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa miundombinu ya Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Ametoa agizo hilo leo Desemba 23, 2022 wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa timu za utekelezaji wa Mradi wa Boost kwa Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.

Dkt.Msonde ameonya vikali tabia ya kufanya maamuzi kinyume na taratibu kwa kuwa kufanya hivyo kutafelisha utekelezaji wa afua zilizowekwa na mradi, hivyo kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo kutasaidia kupunguza hoja za wakaguzi katika utekelezaji wa mradi huo.
Pia amewataka wajumbe hao kutokubadilisha maeneo ya utekelezaji wa mradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule au mradi uliopangwa kutekelezwa bila kupata kibali kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kufanya kinyume na maagizo kutaleta dosari kwenye mradi.

"Kumekuwa na tabia ya kubadilisha maeneo ya ujenzi wa shule na miradi mingine, hilo halikubaliki katika utekelezaji wa mradi wa Boost, mradi huu ukipangiwa kufanya kazi katika eneo fulani la ukarabati au ujenzi, hapo ndipo pajengwe kama kutahitaji mabadiliko ni lazima kupata kibali kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI,”amesisitiza Dkt. Msonde.
Amesema kuwa, maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati na kujengwa yamefanyiwa tathmini na imetolewa katika vitabu, hivyo haitakiwi kubadilishwa bila kupata kibali kutoka serikalini.
Dkt.Msonde amewaagiza wajumbe hao kuhakikisha katika afua zote nane walizopitishwa wanaziwekea mkazo kwa kutumia nguvu, akili na utashi kwa kuhakikisha afua zote zinatekelezwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Aidha, amewataka kudumisha ushirikiano kwenye utekelezaji wa mradi wa Boost kila mmoja kwenye kada yake kwa kuhakikisha wote wanaongea lugha nmoja ili ufanisi wa mradi huo uweze kutokea.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Mara, Benjamin Oganga ameishukuru Serikali kwa kuamua kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo timu za Usimamizi za Utekelezaji wa Mradi wa Boost nchi nzima kwa lengo la kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa weledi na kutoa matokeo chanya kwa jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news