HII HALI SIYO NZURI:Hebu tucheze kwa utu

NA LWAGA MWAMBANDE

TUNAKARIBIA kuukaribisha mwaka 2023, na kuuaga rasmi mwaka 2022 ambao katika soka ulikuwa na mambo mengi ya kujivunia ikiwemo soka safi lililoshuhudiwa nchini Qatar.

Ni Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Tumeona namna ambavyo vipaji katika soka vinalipa na watu wanaishi maisha bora na kuyaendea malengo yao kupitia vipaji hivyo.

Tukirejea hapa nyumbani, kuna mengi mazuri tumeyashuhudia katika ligi na klabu au timu zetu, kila mmoja ameona namna ambavyo soka letu linaendelea kukuwa kwa kasi.

Hilo ni jambo la heri na hakika ni maombi ya kila mmoja wetu kuona Mungu anawasaidia vijana wetu kung'arisha vipaji vyao, soka lizidi kuwatunza kwa maana ya wanaume kwa wanawake.

Licha ya jitihada hizo, Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema, mara kwa mara katika dakika 90 za michezo yetu mengi yamekuwa yakijiri, miongoni mwao ni changamoto ya kuchezeana ndivyo sivyo na kupelekea kuumizana na hata kupeana majeraha ya kuwekana kando ya mechi kwa kipindi cha uangalizi.

Amesema, tulishuhudia ile migongano ya hapa na pale na na wengi waliendelea kusisitiza huu sio muda wa kuendelea kuumizana tena na badala yake ni muhimu kila mmoja akawa mlinzi wa mwingine. Endelea;

1.Ni wachezaji watatu,
Wameumizwa na watu,
Bila ya kufanya kitu,
Hii hali siyo nzuri.

2.Wachezaji muwe watu,
Mpira ni mchezo tu,
Msipigane viatu,
Hii hali siyo nzuri.

3.Mpira ni kazi yetu,
Twapata kipato chetu,
Kuumizana si utu,
Hii hali siyo nzuri.

4.Kwatuaneni viatu,
Vile vya kimichezo tu,
Vinginevyo mwawa butu,
Hii hali siyo nzuri.

5.Ni kama timu chache tu,
Zinapaniwa na watu,
Vile vibaya viatu,
Hii hali siyo nzuri.

6.Mpira ni kazi yetu,
Tena burudani yetu,
Hebu tucheze kwa utu,
Hii hali siyo nzuri.

7.Na nyie marefa wetu,
Msifumbie macho tu,
Wakiumizana watu,
Hii hali siyo nzuri.

8.Toa kadi nyekundu tu,
Wakome wasona utu,
Kinga wachezaji wetu,
Hii hali siyo nzuri.

9.Chama cha mpira wetu,
Anzisha uchunguzi tu,
Ni vipi hivi viatu?
Hii hali siyo nzuri.

10.Sasa wachezaji wetu,
Ambao afya ni butu,
Kwa sababu ya viatu,
Mjaliwe hali nzuri.

11.Takuwa furaha yetu,
Kuchezea timu zetu,
Tufike malengo yetu,
Hali hii siyo nzuri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news