Jopo kubwa lashuhudia DCEA ikiteketeza dawa za kulevya tani mbili na nusu

NA DIRAMAKINI

JOPO kubwa la wataalam na viongozi kutoka taasisi mbalimbali wakiwemo wanahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini wameshuhudia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kelevya (DCEA) ikiteketeza zaidi ya tani mbili na nusu za dawa za kulevya.
Miongoni mwa dawa hizo ni zaidi ya kilo 584.55 zinazojumuisha kilo 569.25 za heroin na kilo 15.3 za cocaine huku tani mbili zikiwa ni za bangi na mirungi.

Uteketezaji huo umefanyika leo Desemba 21, 2022 katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga (Tanzania Portland Cement Company Limited-TPCC) kilichopo Tegeta Wazo jijini Dar es Salaam.

Zoezi la uteketezaji limekuwa likifanyika katika viwanda vya saruji nchini kwa lengo la kuepuka dawa hizo kuharibu mazingira na kuathiri afya za watu.
Veronica Matikila akizungumza kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Gerald Kusaya amesema, uteketezaji huu ni wa kawaida na huwa unafanyika baada ya mashauri ya dawa za kulevya kukamilika mahakamani.

"Leo tarehe 21 Desemba 2022 tunateketeza jumla ya kilo 584. 55 za dawa za kulevya zinazojumuisha kilo 569.25 za heroin, Cocaine kilo 15.3 na tani mbili za bangi na mirungi.
"Uteketezaji huu umefanyika kufuatia kumalizika kwa mashauri ya dawa za kulevya katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na Mahakama za Hakimu Mkazi Kisutu na Kibaha Pwani pamoja na Mahakama za Wilaya ya Kinondoni, Ilala, Temeke na Kigambani.
Matikila amesema, dawa za kulevya zilizoteketezwa leo zimehusisha mashauri ya kuanzia mwaka 2009 hadi 2022. "Hii ni Mara ya pili kwa mwaka huu wa 2022 uteketezaji wa dawa za kulevya unafanyika.

"Uteketezaji wa mara ya kwanza ulifanyika mwezi Fabruari ambapo jumla ya kilo 250.7 ziliteketezwa katika kiwanda cha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara,"amefafanua.
Pia amefafanya kuwa, kwa mwaka 2021 uteketezaji ulifanyika mkoani Mtwara ukihusisha kilo 355 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine. Aidha, hekari 41 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa katika mikoa ya Pwani, Arusha na Kilimanjaro.

"Tangu kuanzishwa kwa Mamlaka mwaka 2017 hii ni mara ya tatu kufanya uteketezaji katika kiwanda cha Saruji cha Twiga, mara ya kwanza uteketezaji ulifanyika tarehe 8, Oktoba 2019, ambapo kilo 120.91 za heroin, kilo 70. 96 za cocaine ziliteketezwa.

"Mara ya pili ulifanyika tarehe 12 Novemba 2020 ambapo kilo 118.174 za heroine, kilo 3.932 za Cocaine na kilo 120 za bangi ziliteketezwa,"amefafanua kwa niaba ya Kamishna Jenerali.
Amesema, uteketezaji wa dawa za kulevya hufanyika kwa namna ambavyo hulinda afya na kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira. Pia zoezi hili hushuhudiwa na mahakama, pamoja na taasisi nyingine zinazojihusisha na udhibiti wa dawa za kulevya ambazo zimeainishwa kwenye kanuni za sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
"Wadau hao ni Hakimu au Jaji, Kamishna Jenerali, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka, Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Usalama wa Taifa, Baraza la Taifa la Mazingira na wadau wengine watakaoalikwa na Kamishna Jenerali.

Aidha, zoezi la utekelezaji wa dawa za kulevya ni zoezi endelevu ambalo hufanyika pale panapohitajika. Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya itaendelea kutoa taarifa kwa umma juu ya zoezi la uteketezaji wa dawa za kulevya ili kuwapa taarifa wananchi kuhusu hatua hii muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
"Kipekee shukrani ziwaendee Majaji wa Mahakama, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashtaka, Idara ya Usalama wa Taifa, Baraza la Taifa la Mazingira, Waandishi wa Habari na Wadau wengine walioshiriki kufanikisha zoezi hili muhimu la uteketezaji.

"Aidha, Shukrani zimwendee Mwekezaji wa Kiwanda cha Twiga kwa kuendelea kutupatia ushirikiano na kuhusu zoezi hili kufanyika kiwandani kwake,".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news