Kileo awauma sikio wanafunzi wa vyuo kuhusu matumizi salama ya mtandao

NA DIRAMAKINI

MTANZANIA ambaye ni Mtaalam na Mbobezi wa Usalama Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Kidigitali, Yusuph Kileo amewataka wanafunzi wa Vyuo Vikuu na vyuo vya kati nchini kuwa makini na kutunza taarifa zao binafsi na kuwa na matumizi salama ya mtandao.
Ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki katika Chuo cha Uhasibu jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa elimu kuhusu sheria mpya ya ulinzi wa taarifa binafsi na matumizi ya mtandao nchini.

"Neno likiitwa neno siri, inamaanisha hili ni la kwako wewe peke yako, haturuhusu mtu a-share kwa mtu mwingine kwa sababu zozote zile, isije baadaye ikatokea watu wameshindwa kuelewana na wewe umeshare password vitu vyako ama taarifa zako zikaanza kupatikana mtandaoni huku na kule.
"Baadaye ukaanza kulalamika wakati wewe mwenyewe ulifanya makosa ya kushare neno siri kwa mtu ambaye ulikuwa ukimpenda ama mzazi wako au yeyote,"amesema Kileo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa wizara hiyo, Mhandisi Steven Wangwe amesema kuwa, kumekuwepo na baadhi ya watu wenye tabia ya kudhalilisha wengine katika mitandao ya kijamii kwa kutumia taarifa za watu au kuingilia akaunti za mitandao ya kijamii ambapo amesema njia pekee ya kuondokana na hali hiyo ni kuwa na matumizi sahihi na salama ya teknolojia.
"Tunashauri chochote wanachokiingiza kwenye mtandao iwe ni picha au video au maudhui yoyote, wahakikishe sio yale ambayo yatawafanya wadhalilike au yatasababisha baadaye wasipate kazi au ajira au fursa ya kuwa na heshima kwa jamii,"amesema Mhandisi Wangwe.

Aidha, washiriki mbalimbali wa mafunzo hayo wameshukuru hatua hiyo na kuomba mafunzo hayo yazidi kutolewa ili kuwafikia wengi zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent Mungi amesema, mafunzo hayo ni mkakati wa wizara hiyo wa kutoa elimu ya usalama wa mitandao kwa makundi mbalimbali katika jamii.

"Tunaendelea kutoa elimu ikiwa ni moja ya majukumu ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Tekenolojia ya Habari kutoa elimu hiyo sehemu mbalimbali ili kuhakikisha tunapokwenda kwenye uchumi wa kidigitali wale ambao wanautekeleza uchumi huo wawe wanapata elimu hii muhimu ya usalama wa kimtandao,"amesema Mungi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news