KOMBE LA DUNIA: MASOMO MAKUU QATAR-3

NA LWAGA MWAMBANDE

NOVEMBA 24, 2022 kupitia mwendelezo wa michuano ya Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Dunia (FIFA) 2022 nchini Qatar, Dunia ilishuhudia Wajapan wakionesha tabia njema ya kudumisha usafi wakiwa ndani na hata nje ya Taifa lao.

Ni baada ya mashabiki kuamua kusherehekea ushindi wao baina ya Samurai Blue dhidi ya Ujerumani ambayo walichakazwa ka mabao 2-1 ndani ya Dimba la Kimataifa la Khalifa lililopo Doha nchini Qatar kwa kufanya usafi.

Usafi huo ulikuwa na umuhimu wa kipekee ikizingatiwa kuwa, baada ya mechi maeneo mengi ya dimba huwa yamejaa mabaki ya vyakula taka na vikombe vya plastiki vya vinywaji vinavyoachwa na mashabiki wakati wakiendelea kushangilia mechi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, kilichofanywa na Japan siku ile lilikuwa somo kubwa si kwa Dunia tu, bali pia kwa Watanzania kuhakikisha wanadumisha usafi iwe nyumbani, maeneo ya kazi na popote walipo kwa muda wote. Endelea;


1:Kuacha safi uwanja, kumbe inawezekana,
Si kwa kutumia kwanja, ni kwa kushirikiana,
Ya Japan tumeonja, na tena tumewaona,
Kuyatunza mazingira, hiyo kazi yetu sote.

2:Mara nyingi uwanjani, mambo mengi tunaona,
Mashabiki uwanjani, wengi ni wachafu sana,
Wala wanatupa chini, takataka nyingi sana,
Kuyatunza mazingira, hiyo kazi yetu sote.

3:Lakini Qatar Japan, somo vema tumeona,
Ukiisha uwanjani, mpira wao waona,
Kuokota taka chini, kubakie safi sana,
Kuyatunza mazingira, hiyo kazi yetu sote.

4:Si pale waliposhinda, kwamba ni furaha sana,
Hata wengine kushinda, napo wao tuliona,
Uchafu hawakupenda, kusafisha tuliona,
Kuyatunza mazingira, hiyo kazi yetu sote.

5:Sasa na viwanja vyetu, bora nasi tukaona,
Zikiisha mechi zetu, takataka tukiona,
Tutumie muda wetu, hali iwe njema sana,
Kuyatunza mazingira, hiyo kazi yetu sote.

6:Japan heshima kwenu, tumewaelewa sana,
Lakini tabia yenu, wapi tutakoiona,
Yaweza kubaki kwenu, jinsi watu twawaona,
Kuyatunza mazingira, hiyo kazi yetu sote.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news