KOMBE LA DUNIA: QATAR NDIYE BINGWA WETU 2022

NA LWAGA MWAMBANDE

PENGINE Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) akirejea matamshi yake ya awali kuhusu Qatar kutokuwa na hadhi ya kuandaa Kombe la Dunia 2022 anaweza kujiona mtu wa ajabu au wa hovyo sana.

Hivi karibuni Sepp Blatter alisema uamuzi wa kuipa nafasi Qatar kuhodhi michuano ya Kombe la Dunia la 2022 ulikuwa kosa.

Sepp Blatter mwenye umri wa miaka 86, alikuwa rais wa FIFA wakati Qatar ilipotunukiwa kandarasi ya kuhodhi mashindano hayo mwaka 2010.

"Nchi ni ndogo sana. Kandanda na Kombe la Dunia ni kubwa mno,"Sepp Blatte aliliambia gazeti la Uswisi la Tages Anzeiger.

Kombe la Dunia la Qatar ni la kwanza kuandaliwa Mashariki ya Kati katika historia ya miaka zaidi ya tisini ya michuano hiyo.

Pia ni kombe la kwanza wakati wa majira ya baridi kali ya Ukanda wa Kaskazini ambalo limefanyika kuanzia Novemba 20 hadi Desemba 18, 2022.

Licha ya Qatar kuondolewa katika hatua za awali ndani ya michuano hiyo, wengi wanakiri kuwa, wao ndio mabingwa wa Kombe la Dunia 2022, ingawa ndoo imeenda nchini Argentina.

Ni kutokana na ukweli kwamba, taifa hilo dogo katika ukanda wa Ghuba limeandika historia ya maandalizi bora zaidi ya kombe hilo pamoja na kusimamia kile ambacho wanaamini kuwa, kikitendwa katika ardhi yao ni dhambi kubwa ambayo itakwenda kuangamiza kizazi baada ya kizazi.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa, suala la kulinda imani zetu na tamaduni kwa kuyapa kisogo mahusiano ya watu wa jinsia moja na mambo mengine ya hovyo ni heshima kubwa, endelea;

1.Sisi wa Imani zetu, Qatar ndiye bingwa wetu,
Kalinda Imani zetu, pia na vitabu vyetu,
Kweli Qatar ni mwenzetu, kwenye hizi dini zetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

2.Argentina ni wenzetu, wabeba kombe la watu,
Messi mchezaji wetu, amemalizia vitu,
Ila wa Imani zetu, Qatar ndiye bingwa wetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

3.Duniani kuna watu, na tena kuna viatu,
Watu wanafanya vitu, kwa Maulana ni kutu,
Wanafura ka kifutu, kutetea mambo butu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

4.Mungu aliumba watu, toka kwa mababu zetu,
Ndoa ya kwanza ya watu, kweli ilikuwa kwatu,
Adamu Hawa ni watu, kwa ndoa wakawa watu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

5.Livyomwema Mungu wetu, ajaza dunia yetu,
Sio wa kiume tu, bali wa kike ni wetu,
Dunia bado msitu, kuijaza kazi yetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

6.Katika vitabu vyetu, adhabu ni wazi kwetu,
Litufunza Mungu wetu, walofanya wale watu,
Ya Sodoma funzo kwetu, ya Gomora pia yetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

7.Dunia hii ni yetu, tuyafanye mambo yetu,
Tena huyu Mungu wetu, katuacha huru watu,
Lakini uhuru wetu, tusifanye yenye kutu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

8.Ulevi si bora kwetu, vyasema vitabu vyetu,
Qatari wale wenzetu, msimamo wao kuntu,
Hao ni mabingwa wetu, twawasifu roho kwatu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

9.Qatar huyu bingwa wetu, amekonga nyoyo zetu,
Yake ni makubwa kwetu, kukataza mambo butu,
Sodoma isije kwetu, yakiona macho yetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

10.Kombe la Dunia letu, mwaka huu mwaka wetu,
Atukuzwa Mungu wetu, yale maamuzi yetu,
Kutowaruhusu watu, kunajisi huku kwetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

11.Kumi na sita si yetu, wanakoshindana watu,
Hata robo siyo yetu, kombe tayari ni letu,
Roho zetu ziko kwatu, Qatar amefanya yetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

12.Kwenye histori yetu, limeshaingia kwetu,
Kwamba dunia ya kwetu, kumuenzi Mungu wetu,
Aliyokataka kwetu, yabaki kwao si kwetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

13.Hongera mabingwa wetu, Qatar mmefanya yetu,
Ingelikuwa ni kwetu, siijui nguvu yetu,
Lakini kwa raha zetu, ubingwa huu ni wetu,
Tutarudiarudia, habari iwaingie.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news