Kumjengea Mungu kanisa ni sawa na kuwekeza-Mchungaji Swide

NA DIRAMAKINI

MCHUNGAJI wa Kanisa la Fire of God Ministry, Swide Mlay, lililopo Njia Panda ya Tegeta A jijini Dar es Salaam, amewasihi watanzania kuendelea kutangaza habari za Mungu, zaidi sana amewaasa wasiogope gharama za ujenzi wa kanisa maana Mungu ndiye atawaongoza namna ya kumjengea makanisa.
Aidha, amesema Mungu ndiye mwenye fedha na dhahabu na anajua namna ya kuelekeza hizo mali zilipo ili wale wanaotaka kufanya kazi yake wamjengee mahali pake pa ibada.

"Ninawashauri wote wenye wito wa kumtukia Mungu wasione kama ni kazi ngumu,hivyo ukiamua kumtumikia Mungu mtumikie kweli kweli,"alisema.

Ameyasema hayo kwenye ibaada maalum ya ufunguzi wa kanisa lake ambalo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 82 na limejengwa kwa muda wa miezi sita tu huku gharama zake zikiwa zimekusanywa kwa maajabu ya Mungu.
Askofu Justus Rutashobya ndiye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo iliyofanyika kanisani hapo,ikihusisha waumini na wageni mbalimbali.

Mchungaji Swide aliongeza kuwa baraka za Mungu zinawaendea wale watu wanaomtolea Mungu, kwahiyo Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa kumtolea Mungu ili kuujenga ufalme siyo kupoteza fedha na mali zao bali ni sawa kuwekeza.

Ni nani hasa Mchungaji Swide?Maajabu yake yapi?

Akimuelezea Mchungaji Swide, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo,Thomas Ole-Kuyan amesema Mchungaji Swide ni Kuhani wa Mungu mwenye uwezo wa kuona matatizo na shida za watu wanaomuendea Mungu kupitia kwake ambapo anawatajia shida hizo pasipo hata kumsimulia.
"Mchungaji huyu ana utaratibu wa kuonana na mtu mmoja mmoja ofisini kwake siku ya kila Alhamis na hapo ndipo kwa uwezo wa Mungu anakutajia matatizo yako yote na kukuombea na yote yanaisha,"anasimulia Bwana Ole-Kuyan.

Anasema awali Mchungaji huyo alikuwa anafanyia ibaada kwenye kabisa la mabati eneo la Goba Njia Nne.

Alisema baada ya kuona waumini wanazidi kuongezeka,mwezi Aprili 2022, aliamua kununua eneo hilo hapo Njia Panda Tegeta A ili aweze kujenga kanisa lenye kumpa Mungu utukufu zaidi na kweli ndoto hiyo imefanikiwa.

Akifafanua alisema Mchungaji Swide alianza kumtumikia Mungu kwa kuanzisha kanisa rasmi mwaka 2018.
"Kabla ya hapo Mchungaji huyo ambaye Daktari wa Binadamu alikuwa ni Mwajiriwa wa Hospitali za Serikali kama tabibu,na alipoitwa kumtumikia Mungu alipumzika utumishi wa umma,"alisema Bwana Ole-Kuyan, na kuongeza kuwa mbali na kuhubiri injili Mchungaji huyo anamili zahanati zake mbili ambapo zinampa kipato na pia huzitumia kutibu watu wanaomuendea kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu ambayo kiuhalisia yanahitaji tiba za kidaktari ambapo wanatibiwa pasipo malipo.

Naye Katibu wa Kamati ya ujenzi wa kanisa hilo Deogratius Masawe ameongezea kuwa dhumuni la kanisa hilo ni kuwaelimisha watu hususani vijana kufuata njia ipasayo kumtumikia Mungu.
"Unajua vijana wengi siku hizi hawajui dhumuni la maisha yao hapa duniani,wanaishi pasipo malengo,usishangae wengi wanajiingiza katika mambo mengi yasiyofaa.

"Kanisa hili limekuja kuziba pengo hilo kwa msaada wa Mungu,"alisema Bw.Massawe.

Kwa huduma ya maombi na maombezi Mchungaji Swide anapatikana kwa namba ya simu hizi hapa: 0718905595 au 0744236070.

Post a Comment

0 Comments