Malimbikizo ya madeni yavitesa vyombo vya habari

NA GODFREY NNKO

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amesema, miongoni mwa changamoto kubwa ambayo vyombo vya habari nchini inapitia licha ya sheria ambazo zipo katika hatua za maboresho ni pamoja na malimbikizo makubwa ya madeni ya vyombo vya habari.

Balile ameyasema hayo leo Desemba 17, 2022 katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 linaloendelea ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamnhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan la wadau wa vyombo vya habari kukutana ili kujadiliana kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Siku za karibuni,wamiliki wengi wa vyombo vya habari nchini yakiwemo magazeti waliamua kusitisha uzalishaji au kutoa huduma ya moja kwa moja kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha au malimbikizo ya madeni ambayo wanayadai kwa muda mrefu bila kulipwa.

Hatua ambayo ilichangia idadi kubwa ya wafanyakazi kupoteza ajira, kuacha madeni makubwa kwa waajiri wao ambayo hayajalipika hadi sasa, hivyo kuwafanya wadau hao wa habari kupoteza mwelekeo na wengine kukata tamaa ya maisha.

Balile amesema, licha ya juhudi kufanywa, bado taasisi za serikali zikiwemo halmashauri hazijalipa madeni yao kwa vyombo vya habari.

“Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, madeni ambayo vyombo vya habari vinadai kwa serikali na taasisi zake ni shilingi bilioni saba.Ukijumuisha na deni la Gazeti la Daily News la Serikali (shilingi Bilioni 11), jumla ya deni ni shilingi bilioni 18 na zaidi.

“Halmashauri wana roho ngumu, hawajalipa mpaka leo licha ya kuandikiwa barua na TAMISEMI (Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambayo kwa sasa ipo chini ya Ofisi ya Rais). Tunaomba Mheshimiwa Waziri (Nape) liwekee mguu chini, utusaidie,”amesema Balile.
 
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itavilipa vyombo vya habari deni la zaidi ya shilingi bilioni sita baada ya kufanya uhakiki wa deni hilo ambalo ni moja ya mambo yaliyosababisha kufa kwa baadhi ya vyombo hivyo nchini.

Rais Samia alitoa ahadi hiyo Juni 28, 2021  jijini Dar es Salaam wakati akijibu swali la Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile aliyemuomba Mheshimiwa Rais kutimiza ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ya kulipa deni hilo kabla ya Juni 30, 2021.

Alisema Serikali itafanya uhakiki wa madeni hayo ya vyombo vya habari, kisha itaanza kulipa kidogo kidogo mpaka deni hilo liishe.

“Nitafanya kazi na Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba tunalipa madeni haya kidogo kidogo, lakini lazima tuyafanyie uhakiki kisha tuweze kulipa, hatutaweza kulipa kwa mkupuo,”alisisitiza Mheshimiwa Rais.

Aidha, kuhusu katazo la Serikali kutangaza kwenye vyombo vya habari, Rais Samia alisema tangu ameingia ofisini, hajaona kama kulikuwa kuna katazo hilo hata hivyo katika utawala wake hakutakuwa  na katazo hilo.

“Wakati wangu huu sitakataza matangazo kwenye vyombo binafsi, kwa hiyo ni jukumu letu kutafuta matangazo hayo,” alisema Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news