MASOMO MAKUU QATAR-4: 2022 vigogo wamepigika, Morocco ikiinuka

NA LWAGA MWAMBANDE

"Morocco ilifungua milango kwa kutinga nusu fainali mwezi huu na nina imani taifa moja wapo la Afrika litaenda mbali zaidi kwenye Kombe lijalo la Dunia. Mafanikio ya Morocco yametufanya Waafrika wote tujione wa kipekee na wenye uwezo. Mwanga wa soka la Afrika una nuru mbele yetu;

Picha na Getty Images.

Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe ameyasema hayo Jumatano ya wiki hii huko jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini wakati akizungumza na wanahabari.

Motsepe ambaye ni raia wa Afrika Kusini aliyechukua nafasi ya Ahmad Ahmad anaamini mafanikio ambayo Morocco imeyapata kwenye fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022 ni dalili kuwa kuna mambo mazuri yanakuja mbeleni.

Kwenye fainali za Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) 2022 nchini Qatar, Morocco walivunja rekodi ya Ghana waliofika robo fainali kwa wao kufika nusu fainali ya mashindano hayo.

Bosi huyo wa CAF anasema, timu ya Morocco kufanya vizuri kwao kutazipa ari timu nyingine barani humo kuamini zinaweza kusonga mbele hususani mwaka 2026.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, kupitia Kombe la Dunia nchini Qatar, imedhirisha wazi kuwa, Afrika tumepiga hatua kubwa katika soka. Endelea;


1:Tumeshakua Afrika, tena tumeerevuka,
Hatua tuliyofika, kwa kweli ya kusifika,
Morocco walivyowika, tubakie tunacheka,
Hii nusu fainali, ya Morocco ni hamasa.

2:Kumbukumbu zahusika, hatujawahi kufika,
Mahali pale twafika, robo ndiyo tulicheka,
Ila sasa Afrika, nusu fainali deka,
Hii nusu fainali, ya Morocco ni hamasa.

3:Tena hajabahatika, mpira umepigika,
Vigogo wamepigika, Morocco ikiinuka,
Kweli tumefarijika, jinsi tulivyoinuka,
Hii nusu fainali, ya Morocco ni hamasa.

4:Spain walipigika, virago wakaondoka,
Ureno yakawafika, nao wakachoropoka,
Ubelgiji wakachoka, na wao wakaondoka,
Hii nusu fainali, ya Morocco ni hamasa.

5:Mine ijayo miaka, timu tisa zitafika,
Muda wa kuchakarika, kwa timu za Afrika,
Morocco ilipofika, tena tukaweze fika,
Hii nusu fainali, ya Morocco ni hamasa.

6:Morocco vema kufika, yao yakaeleweka,
Vipi hapo wamefika, jinsi walivyojiweka,
Na wengine Afrika, wafwate nyayo kufika,
Hii nusu fainali, ya Morocco ni hamasa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news