MISIBA MIWILI:Mwanakwetu alishangazwa na kina cha shimo la kaburi hilo japokuwa lilichimbwa eneo gumu

NA ADELADIUS MAKWEGA

DESEMBA 2 na 3, 2022 majirani wawili wa mwanakwetu walikumbwa na msiba, kama jirani yao alijaribu kujitahidi kuweza kushiriki misiba yote miwili na kwa bahati nzuri msiba wa kwanza maziko yalikuwa Desemba 2, 2022 na msiba wa pili maziko yalifanyika Desemba 3, 2022.

Msiba wa kwanza ulihudhuriwa na waombolezaji wengi kuliko msiba wa pili na alipojaribu kujiuliza hilo alibaini kuwa, msiba wa kwanza aliyefariki alikuwa ni mwenyeji na mkazi wa Chamwino Ikulu na hapo walikuwepo watoto, wajukuu. vitukuu, vining’inila na vilembwe.
Misiba yote miwili waliofariki walikuwa ni akina mama wenye umri mkubwa na walizaliwa Chamwino Ikulu, lakini huu msiba wa pili marehemu alikuwa anaishi huko Hombolo kwa ndugu zake.

Kwa kuwa msiba wa pili maziko yalifanyika Jumamosi, mwanakwetu alijaribu kushiriki kwa karibu mno, Walipokuwa nyumbani kwa marehemu yalipokuwa makazi ya wazazi wake miaka zaidi ya 100 iliyopita ambapo sasa wanakaa watoto wa kaka zake.

Hapo alisimama msomaji wa wasifu akisema kuwa mama huyu alizaliwa mwaka 1920 na hadi anafariki alikuwa na miaka 102.

Msomaji wa wasifu alisema kuwa mama huyu aliolewa mara moja, lakini ndoa yake haikudumu na hakujaliwa kupata watoto hadi anafariki dunia.

Msomaji wa wasifu huo alisema bayana kuwa hadi maiti inafika hapo jeneza lililipiwa na wanakijiji cha Hombolo huku gharama za usafiri na gharama nyingine zilizokuwa zinadaiwa hadi msiba unafanyika zilikaribia laki nne.

Msomaji wa wasifu alisema wazi kuwa bado wanakusanya michango hadi mwishoni wakishazika itafahamika pesa iliyopatikana ni kiasi gani na kama itaweza kulipa deni hilo au la.

Kwa kuwa mwanakwetu alikuwa kando na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Talama, Andasoni Makolokolo alisikia akisema kuwa wao wanazo pesa, lakini makubaliano pesa hizo zinatumika tu kuzikana kwa wanakikundi hai wanaochangia kila mwezi mama huyu hakuwa mwanakikundi.

Mwanakwetu alijiuliza swali moyoni je aliyemuoa mama huyu yu hai, je kama alioa tena huyo mwanaume alipata watoto? Je kuna ushiriki wake au nduguze? Kwa hekima za mwanakwetu alibaini kuwa mama huyu aliolewa muda mrefu sana wa kuyajibu maswali yake angepatikana, lakini ingeleta kero msibani, hekima ilikuwa kubaki nalo moyoni.

Muda huo wachungaji wanangojwa na chakula kilianza kugawiwa kwa waombelezaji wote wakala. Baada ya chakula hicho mtani mmojawapo wa Wagogo, Msukuma akachukua ndoo ya maji akisema,

“Jamani eee wale wale wote tuliokula chakula naomba tuchangie msiba huu, sasa napita kuchukua pesa hiyo.” Maneno haya yalisema kwa matamshi ya Kisukuma. Akaanza kuzunguka kwa mtu mmoja baada ya mwingine akifika kwako unaweka pesa katika ndoo, ukikosa pesa anaondoka na viatu, simu, saa, vilemba na na kadhalika. Kijana huyu aliifanya kazi hiyo huku viatu, saa, simu, vilemba na khanga,vitenge na kofia vikikusanywa.

“Mtani ninaomba simu yangu bwana, nipe nikatoe pesa nikupe pesa yako.” Mama mmoja alisikika akisema na Msukuma.

Kwa kuwa mwanakwetu alikuwa kando ili kukwepa aibu hiyo alitoa pesa mfukoni na kugawana na majirani zake wawili wa kushoto na kulia kukwepa aibu kwa kupokonywa simu au makubazi yao msibani.

Wachungaji walifika wakasali na kutangulia kanisani na ukabebwa mwili hadi ibadani Kanisa la Anglikhan la Mtakatifu Luka Chamwino Ikulu. Ibada ilipokwishwa mwili ulibebwa hadi makaburini na ibada ya mazishi ikiendelea kwa sala na nyimbo.

“Mwamba wenye imara, kwako nitajificha, maji hayo na damu, yaliyotoka humo, hunisafi na dhambi, hunifanya Mshindi.”

Mwanakwetu waombolezaji waliendelea kuweka udogo kaburini wakipokezana machepe na majembe, waimbaji nao wakiimba kwa nguvu zote na mandhari ya mabakurini ilipambwa na nyimbo na sauti ya chachachacha…udongo ikiingia kaburini.

“Nikungojapo chini, nakwenda kaburini, Nipaapo mbinguni, nakukuona enzini, Roho yangu na iwe, rahani mwako wewe.”

Waombolezaji wakiwa na huzuni kubwa, wengine wakiikunja mikono yao na kushika tama nao akina mama waliojifunga khanga na vitenge na vilemba kichwani.

Naye Mwanakwetu huku fulani na suruali yake nyeusi vikiwa vimetapakaa vumbi la makaburini, akamuuliza mtu aliyekuwanaye jirani jina la wimbo huo akanijibu kuwa unaitwa, Mwamba Wenye Imara.-Rock of Ages.

Ibada ya mazishi iliendelea vizuri huku akibaini kuwa zoezi la kuuweka udongo kaburini lilitumia muda mrefu sana kuliko mazishi ya msiba wa kwanza, lakini waombolezaji waliendelea na kazi hiyo huku nyimbo za msiba ziliendelea kuimbwa.

“Tuonane paradiso, tuonane paradiso,tuonane paradiso, kwenye mji wa raha,na taji tutavikwa, na taji tutavikwa, na taji tutavikwa, kwenye mji wa raha, na Yesu tutamwona, na Yesu tutamuona.”

Wakati wimbo huu unaanza kuimbwa mwanakwetu hakuusikia vizuri maana alikuwa anauchota mchanga na chepe kuutupa kaburini kwa hiyo alipoinuka akausikia vizuri, naye ndugu yake jirani alimuuliza tena jina la wimbo huu wa pili alimjibu kuwa unaitwa Tuonane Paradiso-See You in Paradise.

Ibada ya mazishi ilikwisha na ndugu wa marehemu waliagiza wambolezaji wote turudi nyumbani kwao kuna matangazo muhimu, kweli waliitikia wito huo.

Wakiwa njiani rafiki yake mwanakwetu ambaye ni Msukuma akamwambia kuwa katika mila za Kiafrika kwa baadhi ya makabila kama aliyefarika alioa au kuolewa halafu hakuwahi kujaliwa kupata mtoto basi huwa kaburi lake linakuwa na kina kirefu likimaanisha kwa kuwa vizazi vingine vya ukoo huo visije kupatwa na hali kama hiyo.

Tangu awali mwanakwetu alishangazwa na kina cha shimo la kaburi hilo japokuwa lilichimbwa eneo gumu, lakini lilichimbwa kwa ustadi mkubwa na kiasi alipita jambo jipya kichwani mwake.

Walipofika hapo nyumbani ilisomwa michango yote iliyokusanywa kwa kila mmoja aliyepewa daftari, kuiwasilisha na kusomwa huku mtani yule wa Kisukuma akikusanya karibu shilingi 175,000 na zikakusanywa fedha zote na kulipa madeni yote ya msiba huo na mwanakwetu kurudi nyumbani kwake.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news