NATAFUTA FORODHANI:Kwa Mungu twataka nini?

NA LWAGA MWAMBANDE

UKIWA jijini Zanzibar kama haujafika bustani ndogo kwenye Mji Mkongwe maarufu kama Bustani za Forodhani ni wazi kuwa,utakuwa haujafaidi yaliyomo visiwani humo.

Bustani za Forodhani zipo kando ya Mtaa wa Mizingani unaopita ukingo wa bahari wa Mji Mkongwe, mbele tu ya majengo ya House of Wonders (Jumba la Maajabu) na Old Fort (Ngome Kongwe).

Eneo hilo lina historia ndefu, pia ni moja ya maeneo yanayokusanya watu wengi kutoka ndani na nje licha ya udogo wake, hasa nyakati za jioni visiwani Zanzibar.

Aidha, upekee wa bustani hii ni uwepo wa vyakula vya aina mbalimbali, vikiwemo vya asili. Kwa maana nyingine, hapa ni kama kioo cha uso wa Zanzibar na taswira ya visiwa hvyo.

Watalii na wenyeji hukusanyika hapo kula chakula cha jioni wakifurahia vyakula vitamu kama vile dagaa wa baharini,mihogo,viazi vitamu na hata urojo. 
 
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,pia fursa za namna hiyo zimetapakaa katika maeneo mengi Tanzania Bara, hivyo yafaa kufanya maamuzi yenye tija ili kuweza kuwaleta pamoja wazawa kwa wageni kufurahia yanayopatikana Forodhani, endelea;

1.Natafuta Forodhani,
Kama kule Visiwani,
Tubarizi ufukweni,
Hivi tunakwama wapi?

2.Huku mwao midomoni,
Watafuna vya tumboni,
Kwa furaha na Amani,
Hivi tunakwama wapi?

3.Kutoka Chongoleani,
Hadi kule Mikindani,
Natafuta Forodhani,
Hivi tunakwama wapi?

4.Samaki wa baharini,
Na mazao ya shambani,
Vyote viko mikononi,
Hivi tunakwama wapi?

5.Miundombinu mjini,
Ya kufika ufukweni,
Yote tunayo jamani,
Hivi tunakwama wapi?

6.Na Forodhani ziwani,
Kwani tunakwama nini?
Maziwa yamesheheni?
Hivi tunakwama wapi?

7.Mwanza kuwe Forodhani,
Na Bukoba Forodhani,
Musoma na Forodhani,
Hivi tunakwama wapi?

8.Kigoma na Forodhani,
Kibirizi Ufukweni,
Migebuka mlo ndani,
Hivi tunakwama wapi?

9.Pale Kabwe bandarini,
Kipili na Forodhani,
Kasanga iwemo ndani,
Hivi tunakwama wapi?

10.Twende Nyasa ufukweni,
Kyela Itunge ndani,
Mbamba Bay Forodhani,
Hivi tunakwama wapi?

11.Mito mikubwa nchini,
Na samaki kusheheni,
Tuanzishe Forodhani,
Hivi tunakwama wapi?

12.Au hatujiamini,
Kwamba nasi tutawini,
Kama kule Forodhani,
Hivi tunakwama wapi?

13.Twende kozi Visiwani,
Hasa pale Forodhani,
Yao yakae kichwani,
Hivi tunakwama wapi?

14.Mandhari ya Forodhani,
Siyo nyumba kusheheni,
Peupe ka uwanjani
Hivi tunakwama wapi?

15.Wenzangu jiulizeni,
Na tena tafakarini,
Iko wapi Forodhani?
Hivi tunakwama wapi?

16.Bila hii Forodhani,
Pamoja na ndefu pwani,
Kwa Mungu twataka nini?
Hivi tunakwama wapi?

17.Ukienda Forodhani,
Ajira nyingi ka nini,
Na nyingine pembezoni,
Hivi tunakwama wapi?

18.Mapishi ya Forodhani,
Ona uko darasani,
Na wewe fanya nyumbani,
Hivi tunakwama wapi?

19.Juisi miwa mjini,
Yajaa iko pomoni,
Mazao ya baharini,
Hivi tunakwama wapi?

20.Mie nenda Forodhani,
Urojo wende tumboni,
Na juisi mkononi,
Hivi tunakwama wapi?

21.Forodhani sikieni,
Biashara panueni,
Hata Bara kuna pwani,
Jiongeze au vipi?

22.Mje kule anzisheni,
Brand yenu onesheni,
Na pesa zifaidini,
Jiongeze au vipi?

23.Tunasema karibuni,
Wawekezaji mjini,
Mfanye yale makini,
Jiongeze au vipi.

24.Bagamoyo anzieni,
Sisi tutawafwateni,
Coco Beach sogeeni,
Jiongeze au vipi?

25.Na sisi changamaneni,
Elimu ije kichwani,
Ni Muungano jamani,
Jiongeze au vipi?

26.Mkifika kule Pwani,
Au kule Mikindani,
Mtaongeza thamani,
Jiongeze au vipi?

27.Mfanyayo Forodhani
Kafanye Pongoleani,
Tubarizi ufukweni,
Jiongeze au vipi?

28.Chakula hapa nchini,
Kama kote duniani,
Chaenziwa kama dini,
Kila mtu au vipi?

29.Ukiingia kazini,
Kuanzisha Forodhani,
Pesa kwako tasheheni,
Hivi tunakwama wapi?

30.Nimeingia shuleni,
Nione kikaangoni,
Zanzibar pizza mekoni,
Hivi tunakwama wapi?

31.Nikishinda mtihani,
Nitatoka hadharani,
Niwalishe barazani,
Hivi tunakwama wapi?

32.Asanteni Forodhani,
Mwafaa sana jioni,
Vilaji vyenda tumboni,
Sisi tunakwama wapi?

33.Hujafika Forodhani,
Hujafika Visiwani,
Ni utalii wa ndani,
Hivi tunakwama wapi?

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news