Rais Dkt.Samia apeleka shangwe Musoma Vijijini, aridhia kufufuliwa mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji Bonde la Bugwema

NA FRESHA KINASA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la kuendeleza Mradi wa Bugwema uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini leo Desemba 30, 2022 ambapo taarifa hiyo imesema kuwa;

"Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikusudia kuanzisha kilimo kikubwa cha umwagiliaji ndani ya Bonde la Bugwema, hii ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 70.
Binde la Bugwema ni kubwa mno, eneo lililokusudiwa kulimwa wakati huo ilikuwa ni ndani ya hekta 10,000. Bonde lenyewe likichukuliwa kwa ujumla wake lina zaidi ya ukubwa wa hekta 20,000.

"Miundombinu ya umwagiliaji ilijengwa miaka hiyo, lakini utekelezaji wake ukasimama. Mazao makuu yanayolimwa ndani ya bonde hilo ni mahindi, mpunga, alizeti dengu na pamba."
Hatua hiyo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Hassan inakuja kufuatia ombi ambalo lilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo wakati Mhe. Rais Dkt. Samia Hassan alipotembelea Musoma Vijijini akizindua Mradi wa ujenzi wa Bomba la Maji la Mugango-Kiabakari-Butiama Februari 6, 2022.

Pia Mheshimiwa Prof.Muhongo Mbunge wa Jimbo hilo la Musoma Vijijini alirudia kutoa ombi hilo kwenye Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma, tarehe 7 hadi 8 Desemba, 2022
Ambapo Alhamisi ya Desemba 29,2022, Timu ya Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitembelea Bonde la Bugwema. Timu hiyo iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt.Raymond Mndolwa. Huku pia viongozi kadhaa wa Musoma Vijijini waliambatana na Timu hiyo ya Wataalamu.

Miongoni mwao alikuwepo Mbunge wa Jimbo hilo, Prof. Sospeter Muhongo, Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Bugwema, Ezekiel MacGudo,Diwani wa Kata ya Bugwema, Mhe Clliford Machumu na Mtendaji wa Kata ya Bugwema, Joseph Phinias.
Taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ni kwamba matayarisho ya utekelezaji wa Mradi wa Bugwema yanaendelea vizuri kwa ajili ya kuanza kufanya upembuzi yakinifu.

"Wananchi wa Musoma Vijijini wanaendelea kutoa shukrani nyingi sana kwa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuendeleza Mradi wa Kilimo kikubwa cha umwagiliaji ndani ya Bonde la Bugwema.
"Pia, wanashukuru upatikanaji wa chakula kingi cha bei nafuu kinasaidia kushusha mfumuko wa bei kwenye soko la chakula." imeeleza taarifa hiyo.
Picha za juu zinaonesha Timu ya Wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakiwa ndani ya Bonde la Bugwema, Musoma Vijijini. Baadhi ya Viongozi wa Musoma Vijijini walishiriki kwenye ziara hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news