Rais Nabii Dkt.Joshua afunguka kuhusu maono ya mitume na manabii Tanzania mwaka 2023

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amesema, mwaka 2023 wanachama wa umoja huo nchini wanatarajia kuyaendea maono yao ya kuhakikisha injili na neno la Mungu linasonga mbele nchini.
Ameyasema hayo Desemba 29, 2022 kupitia hotuba yake ambayo ameitoa ikitoa tathimini, dira na mwelekeo wa umoja huo katika siku zijazo. Endelea na hotuba kamili hapa chini;

”Amani iwe nanyi mitume na manabii, Februari 19, 2022 chini ya usimamizi makini wa mzee Baba yetu Mtume Mkuu wa Taifa letu Mheshimiwa Dunstan Haule Maboya,Mzee Ndalima, Mzee Bendera na wazee wengine.

"Tulifanikiwa kufanya uchaguzi uliopelekea kuwapata viongozi wa Kamati Kuu ya Mitume na Manabii Tanzania, miezi mitatu baadaye hadi mwezi Mei, 2022 tulifanikiwa kuunda kamati za uongozi kwa asilimia 80 kote nchini Tanzania Bara.

"Juni, 2022 kwa pamoja tulifanikiwa pia kufanya mkutano mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania mkoani Morogoro.

"Oktoba, 2022 kwa mafanikio makubwa tuliadhimisha wiki ya mitume na manabii na kuigusa jamii kubwa sana kwa kutoa misaada mbalimbali kwa watu binafsi, mashirika na taasisi mbalimbali za Serikali.

"Tunaishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia wakuu wa mikoa walioshiriki nasi kwenye wiki hiyo ya maadhimisho ya mitume na manabii Tanzania.

"Hata hivyo, wakati yote hayo yanaendelea tulifanikiwa kuwasilisha maombi ya usajili ya taasisi yetu serikalini na hatua za usajili zinaendelea vizuri sana ndani ya miezi 10 wana wa Mungu tumefanya mambo hayo yote zikiwemo ziara za kamati kuu ambazo niliziongoza mimi mwenyewe kama Rais wa Mitume na Manabii Tanzania na tulifanikiwa kuwafikia mitume na manabii ambao hawajawahi kufikiwa tangu nchi hii inaumbwa. Hakika jina la Bwana libarikiwe sana.

"Ndugu zangu mitume na manabii, mimi kama Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii ninawashukuru sana viongozi wa kamati kuu, halmashauri kuu na wanachama wote wa huduma tano kwa ujumla wenu maana bila ushiriki wenu katika majukumu haya tusingefika hapa tulipo.

"Ndugu zangu mitume na manabii sasa ni mwisho wa mwaka, tunaisubiri asubuhi ya mwaka 2023 uzoefu unaonesha kabla jogoo hajawika Petro alikuwa amekwisha kumkana Kristo, hivyo ikitokea kabla ya Januari, mtu yeyote miongoni mwetu akaukana umoja wetu tusihofu juu ya jambo hilo.

"Maana huo utakuwa ni udhaifu wake tu, lakini moyoni mwake anaupenda sana umoja, na mwakani kama hatutazimia moyo atakuwa mmoja wetu.

"Ndugu zangu mitume na manabii kwa kuwa tunasafari ndefu ya kuujenga umoja wetu na kurudisha heshima ya Kanisa la Kitume na Kinabii katika Taifa letu ni lazima yafuatayo yawe nguzo na dira yetu.

"La kwanza, upendo wa Kristo miongoni mwetu, la pili umoja wa Kristo miongoni mwetu la tatu mpaka sasa uwe ni umoja unaozingatia kwamba upendo miongoni mwetu ni nguzo kuu kwa sababu juu ya upendo hakuna hatia.
"Ndugu zangu mitume na manabii, ninaomba tusisahau kuwa huduma zetu za kitume na kinabii zipo kwenye tishio kubwa sana la kushambuliwa na mafarisayo wa kisasa ambao wanaamini kuwa bila wao nchi yetu ya Tanzania haiwezi kuwa na amani.

"Kwa sababu hiyo, lazima tujitambue wenyewe kwanza na tulifumbue macho taifa litambue amani ya nchi yetu inatutegemea sote kama raia wema wa nchi yetu. Ndugu zangu Mitume na Manabii kwa unyenyekevu wote nawaomba tusiache kuwaombea wenye mamlaka na kuombea amani ya nchi yetu ya Tanzania ili idumu milele na milele.

"Maono yetu ya mwaka ujao wa 2023 tunataka kila mtume na Nabii awe salama na atimize wito wake Mkuu kwa mafanikio makubwa kupitia umoja wetu. 

"Mwisho mwaka 2023 kama Bwana Yesu atakuwa hajarudi tuelekeze nguvu zetu zote kuijenga na kuulinda umoja wetu wa Mitume na manabii Tanzania Mungu awabariki asanteni kwa kunisikiliza,"amehitimisha Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news