Rais wa zamani wa Urusi atabiri vita Ulaya, Marekani 2023 huku bei ya mafuta ikipaa zaidi, haya hapa mambo 10 aliyotabiri

NA DIRAMAKINI

RAIS wa zamani wa Urusi, Dmitry Anatolyevich Medvedev ambaye kwa sasa ni Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Urusi ametabiri vita kati ya Ujerumani na Ufaransa mwaka ujao.
Sambamba na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani ambavyo vitasababisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Twitter, Elon Musk kuwa rais.

Medvedev aliwahi kuwa rais kwa kipindi cha miaka minne nchini Urusi kati ya 2008 na 2012 wakati Vladimir Putin alipowajibika kama Waziri Mkuu na mwaka 2012 hadi 2020 alirejea tena kama Waziri Mkuu.

Katika orodha yake ya utabiri wa 2023, iliyochapishwa kwenye akaunti yake binafsi ya Telegraph na Twitter, pia Dmitry amesema Uingereza itajiunga tena na Umoja wa Ulaya, ambapo umoja huo nao utanvunjika.

Dmitry ambaye ni kiongozi mtiifu kwa Rais Putin amewasilisha utabiri wake wa mwaka mpya wa 2023 unaojumuisha hatima mbaya kwa Merekani na Umoja wa Ulaya, ambazo zimekuwa kwenye mzozo mkali na Urusi tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, Februari 24, 2022.

Miongoni mwa mambo makubwa zaidi katika utabiri huo ni kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani.

Amesema, majimbo ya California na Texas yatajitenga na kuwa mataifa huru, ikiwemo kuanzishwa kwa Muungano wa Texas na Mexico.

Pia amezungumzia uanzishwaji wa kile alichokitaja Reich ya Nne itakayojumuisha Ujerumani na nchi washirika wake, na kwamba Poland na Hungary zitatwaa na kukalia kwa mabavu maeneo ya Magharibi ya Ukraine ya zamani.

Pia Medvedev amekwenda mbali zaidi na kutabiri kuzuka vita kati ya Ufaransa na Reich ya Nne, na mgawanyiko wa Ulaya.

Utabiri huo pia unajumuisha ongezeko la bei ya pipa moja la mafuta hadi dola 150, na bei ya mita za ujazo elfu moja za gesi kufikia dola 5,000.

Katika hatua nyingine,Dmitry amesema, miongoni mwa mambo anayotazamia kuwa yatatokea mwaka mpya wa 2023 ni kukataliwa kwa Euro na Dola kama sarafu za akiba za kimataifa.

Sambamba na kuhamishwa masoko makuu ya hisa na shughuli za kifedha kutoka Marekani na Ulaya hadi kwenda barani Asia.

Huu hapa utabiri wa mambo 10 kutoka kwa Rais wa zamani wa Urusi,Dmitry Anatolyevich Medvedev ambaye kwa sasa ni Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Urusi

1. Bei ya mafuta itapanda hadi $150 kwa pipa, na bei ya gesi itakuwa juu $5.000 kwa kila mita za ujazo 1.000.

2. Uingereza itajiunga tena na EU

3. EU itaanguka baada ya kurudi kwa Uingereza, Euro itaachwa kutumika kama sarafu ya zamani ya Umoja wa Ulaya

4. Poland na Hungary zitamiliki maeneo ya Magharibi ya Ukraine iliyokuwepo hapo awali

5. Reich ya Nne itaundwa, ikijumuisha eneo la Ujerumani na satelaiti zake, yaani Poland, majimbo ya Baltic, Czechia, Slovakia, Jamhuri ya Kiev, na waasi wengine.

6. Vita vitatokea kati ya Ufaransa na Reich ya Nne. Ulaya itagawanywa, Poland itagawanywa tena katika mchakato huo

7. Ireland ya Kaskazini itajitenga na Uingereza na kujiunga na Jamhuri ya Ireland

8. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vitazuka Marekani, California na Texas yatakuwa majimbo huru. Texas na Mexico zitaunda nchi washirika. Elon Musk atashinda uchaguzi wa urais katika majimbo kadhaa, baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

9. Masoko yote makubwa ya hisa na shughuli za kifedha zitaondoka Marekani na Ulaya na kuhamia Asia

10. Mfumo wa usimamizi wa fedha wa Bretton Woods utaanguka, na kusababisha mpasuko katika Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia. Euro na Dola zitaacha kuzunguka kama sarafu ya hifadhi ya kimataifa. Badala yake sarafu za kidijitali zitatumika kikamilifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news