Simba SC kufunga mwaka na Tanzania Prisons leo

NA MWANDISHI WETU

KIKOSI cha Simba SC leo kitashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambao utakuwa wa mwisho kwa mwaka huu.
Baada ya mchezo wa leo hawatatukuwa na mchezo mwingine hadi 2023 ambapo, wekundu hao wataanzia Visiwani Zanzibar kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Simba wamesema, wanaingia kwenye mchezo wa leo wakiwa na lengo moja la kuwafurahisha mashabiki kwa kuonyesha kandanda safi pamoja na kupata alama tatu.

MGUNDA AFUNGUKA

Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema, maandalizi ya mchezo yamekamilika na kikosi kipo kwenye hali nzuri, morali ya wachezaji ipo juu tayari kuipigania timu.

Mgunda ameongeza kuwa, mchezo utakuwa mgumu kwani wanaiheshimu Prisons, lakini wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanafunga mwaka kwa ushindi pamoja na kuonyesha kandanda safi.

“Maandalizi yote ya mchezo yamekamilika wachezaji wapo kwenye hali nzuri, tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tupo tayari kupambana,”amesema Mgunda.

ATOA NENO

Kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael amesema kila kitu kipo sawa kwa upande wao na yeyote atakayepata nafasi ya kucheza atakuwa tayari kuitumikia timu.

“Sisi wachezaji tupo tayari kwa mchezo, morali zipo juu. Tunawaheshimu Prisons ni timu nzuri, lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi zote,”amesema Gadiel.

NJOONI WOTE

Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kwa kuwa ndio mchezo wa mwisho katika mwaka 2022 na wapo nyumbani hivyo itakuwa vizuri kushangilia ushindi pamoja.

“Tunahitaji kuweka rekodi ya mapato kwenye mchezo wa leo na kuondoa dhana kuwa ili kujaza uwanja lazima tucheze na timu kubwa za Dar es Salaam.

“Mashabiki leo ndiyo siku yetu kubwa ya kukutana uwanjani kuwashangilia wachezaji wetu na kufunga mwaka, tunajua wachezaji watatulipa kwa ushindi,” amesema Ahmed.

WALIFUNGA

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Septemba 14 Simba SC walifanikiwa kupata ushindi wa bao moja.

Kwenye mchezo huo, bao la Simba SC lilifungwa dakika za majeruhi na kiungo mkabaji, Jonas Mkude.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news