Simba yatamba kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC

NA MWANDISHI WETU

SIMBA SC ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kumaliza mchezo wake wa 15 katika duru ya kwanza ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa kuvuna ushindi mnono wa mabao 3-0.
Ni baada ya kuitandika Coastal Union ya jijini Tanga jumla ya mabao hayo wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Mkwakwani jijini humo.

Katika mchezo huo uliopigwa Desemba 3, 2022 kwenye majira ya saa 10:00 kulikuwa na ushindani mkubwa hasa katika kipindi cha awali ambapo wenyeji Coastal Union walionekana kuwa wabishi kuchaniwa nyavu zao kwa muda wote wa dakika 45 za kwanza.
Aidha, hali ilibadilika mara baada ya timu hizo kurejea katika kipindi cha pili ambapo zilipita dakika 12 kwa timu ya Simba SC kuwa imeandika bao la kuongoza.

Bao likifungwa na Moses Phiri baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa kiungo Clatous Chota Chama aliyepiga pasi mpenyezo iliyomkuta Phiri naye hakufanya makosa akapachika nyavuni.
Aidha, dakika ya 64 Moses Phiri aliwarejesha kati, kwa mara ya pili baada ya kufunga goli kwa penati iliyotokea baada ya mlinzi wa Coastal Union kumfanyia madhambi beki kiraka wa Simba, Shomari Kapombe ambapo mwamuzi aliamuru mkwaju wa penati.

Zaidi ya dakika 90, kwa maana ya dakia za lala salama, Chama alipenyeza bao la tatu lililowafanya Coastal Union kukata tamaa ya kutafuta walau bao la kufutia machozi.

Kocha wa Coastal, Union Yusuph Chipo akizungumza baada ya mtanage huo wa nguvu amesema,timu yake ilizidiwa hasa katika nusu ya pili.
Chipo amesema, katika kipindi cha kwanza walifanikiwa kuwadhibiti Simba kikamilifu. Aliongeza kuwa, mchezo wa mpira wa miguu ni wa makosa, mmoja anapofanya makosa ndipo mwingine anapata nafasi ya kushinda hivyo wachezaji wake walijisahau wapinzani wakawadhibu.

Naye Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda, alisema alipomaliza kipindi cha kwanza alikuwa amewasoma Coastal Union, hivyo muda wa mapunziko alienda kuwaelekeza wachezaji wake nini cha kufanya.
Lengo likiwa ni kuweza kupata matokeo kwenye mchezo huo. Jambo ambalo anashukuru wachezaji wake walilifanya kwa umakini mkubwa hatimaye kufanikisha adhima yao ya kukamilisha duru ya kwanza kwa kukusanya alama 6 kwenye mechi mbili.

Wakati huo huo, mchezo wa mapema uliopigwa majira ya saa 8:00 mchana ukiwakutanisha Dodoma Jiji na Ruvu Shooting, timu ya Dodoma Jiji ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 2-1. Ni kwenye mchezo uliochezwa katika dimba la Liti Mjini Singida.

Wafungaji wa magoli kwenye mchezo huo walikuwa ni Salum Kipaga dakika (04), Hassan Mwaterema (24) na Ally Mwale dakika ya (75).

Matokeo hayo yanaifanya Dodoma Jiji kufikisha alama 15 huku Coastal Union wao wakibakia na na alama zao 12 wakati Simba inafikisha alama 34 katika mchezo wa 15 na kupanda kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania Bara ikiwazidi alama mbili mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.

Mbali na hayo, katika mchezo kati Singida Big Stars na Namungo FC uliopigwa Disemba 2, 2022 kwenye uwanja wa Liti mjini Singida ulimalizika kwa wenyeji kuandika rekodi mpya ya ushindi wa zaidi ya mabao mawili baada ya kufanikiwa kufunga jummla ya mabao 3-0.
Ushindi huo ulikuwa ni wa kwanza kwa SBS tangu ipande Ligi Kuu ya NBC ambapo kumbukumbu zinaonesha kuwa, ushindi mkubwa iliyowahi kuupata timu hiyo ni ule wa bao 2-1 iliyoupata katika uwanja wake wa nyumbani.

Awali timu hiyo yenye makao makuu yake mjini Singida ilikuwa ikipata ushindi wa bao moja moja, tofauti na mchezo huo dhidi ya Namungo FC.

Mabao ya Singida Big Stars yalifungwa na Said Ndemla dakika ya 27, Meddie Kagere dakika ya 66 na Amis Tambwe dakika ya 90 na ushee.
Ushindi huo wa bao 3-0 unaifanya timu hiyo kuendelea kushikilia nafasi ya nne ikiwa na alama 27 baada ya kucheza michezo 14 huku ikisubiri mchezo wa kukamilisha duru ya kwanza kwa matumaini makubwa.

Kocha wa timu hiyo, Hans van der Pluijm alisema, amefurahishwa na matokeo hayo na kwamba anawapongeza wachezaji wake kwa jitahada zao.

Pia kocha Pluijm alidai kuwa, ligi bado ni ngumu na kwamba wao wana mpango mahsusi wa kuhakikisha wanakusanya alama zaidi katika kila mchezo ili kujihakikishia kushika nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Naye kocha msaidizi wa kikosi cha Namungo FC, Shedrack Nsajigwa alieleza kuwa, wachezaji wake walijitahidi kutafuta matokeo, lakini hali haikuwaendea vyema kama walivyotarajia.

Kocha huyo aliwapongeza wapinzani wao akisema kuwa walicheza vizuri na kuwazidi hatimaye kuweza kupata matokeo.

Mchezo wa pili uliopigwa kwenye dimba la Kaitaba mjini Bukoba, timu ya Kagera Sugar ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhdi ya Ihefu FC kutoka Mbarali mkoani Mbeya. Wafungaji wa mabao ya Kagera Sugar walikuwa ni Erick Mwijage dakika 67 na Hamis Kiiza dakika ya 83.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news